Wanaharakati: Ahadi zinazotekelezwa ipasavyo muhimu kwa mabadiliko

Mtu mwenye ulemavu wa miguu akiwa kwenye baiskeli maalumu za walemavu

Muktasari:

Leo, katika siku ya kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu, wanaharakati wanatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kutoa ahadi za kudumu kwa watu hao kwa kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa wen ye ualemavu.

Leo, katika siku ya kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu, wanaharakati wanatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kutoa ahadi za kudumu kwa watu hao kwa kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa wen ye ualemavu.

Mkutano huo, unaotarajiwa kufanyika Februari 2022 nchi Norway, unalenga kushughulikia mahitaji ya watu wenye ulemavu na kuhakikisha wanaunganishwa kwa vitendo katika utungaji na utekelezaji wa sera na sheria.

Mkutano huu ni kusanyiko kubwa zaidi duniani la watu wenye ulemavu, Serikali, mashirika ya kimataifa, mashirika ya kutoa misaada na viongozi wa kibiashara na ni fursa muhimu kwa Serikali na mashirika katika kuunga mkono juhudi za utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD).

Kampeni ya Equal World (dunia iliyo sawa) inayoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Sightsavers kwa ushirikiano na Sense International na ADD International, inazingatia tukio hilo muhimu na kutoa wito kwa Serikali kutumia fursa hiyo kwa kuhudhuria na kutoa ahadi zinazotekelezeka.

Mkurugenzi wa Sightsavers Tanzania, Godwin Kabalika anasema“Tunatoa wito kwa Seri-kali kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa walemavu na kutoa ahadi zinazotekelezeka ipasavyo ambazo zitaleta mabadiliko ya kweli. Ili kufanikisha hili, mawaziri lazima washirikiane na watu wenye ulemavu na mashirika yao ya uwakilishi kabla na wakati wa mkutano huo.”Aliongeza kuwa“Watu wengi wenye ulemavu duniani na Tanzania wanakumbana na ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu.

Aidha, janga la Uviko-19 limeongeza ukosefu wa usawa husuani kwa wasichana na wanawake wenye ulemavu.”Mkurugenzi wa Sense International Tanzania, Naomi Lugoe anasema “hii itakuwa fursa nzuri kwa Tanzania kupitia upya na kwa pamoja utekelezaji wa ahadi za awali na kutoa ahadi mpya zenye nguvu na zinazotekelezeka kuelekea ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu.”

Mkurugenzi wa ADD International Tanzania, Rose Tesha alisisitiza kuwa, “huu utakuwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2015 ambapo Tanzania pamoja na nchi nyingine, iliahidi kujenga dunia ya usawa ambapo hakuna atakayeachwa nyuma.Ushiriki wa watu wenye ulemavu katika mchakato wa kutoa ahadi huongeza dhamira za kisiasa za kutomwacha mtu nyuma. Hapa nchini, mashirika hayo matatu kwa sasa yanafanya kazi na Serikali kusaidia watu wenye ulemavu“kufurahia haki yao ya asili ya kuishi kwa usawa na wengine.”

Mkutano wa kwanza wa kimataifa wa watu wenye ulemavu uliofanyika mwaka 2018 ulikuwa wakati muhimu wa kutambua haki za kundi hilo duniani kote pamoja na kuonyesha utayari wa kisiasa, kuleta usawa kwa ulemavu katika jukwaa la kimataifa.

Pamoja na maendeleo hayo, ahadi zake nyingi bado zinahitaji kufikiwa ili kuhakikisha kwamba haki za watu wenye ulemavu, hasa kutoka katika makundi yaliyotengwa, zinalindwa na kutekelezwa duniani kote.

Kabalika anasema, “mkutano wa mwaka ujao ni fursa kwa Serikali kupaza sauti yake na kujidhatiti katika kutetea haki za walemavu kwa Watanzania. Hivyo ndivyo kampeni yetu ya dunia yenye usawa inataka.”

Tunatarajia kufanya kazi na Serikali ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu ili kuhakikisha sauti za watu wenye ulemavu zinasikika kupitia mashauriano na warsha katika wiki na miezi ijayo kuelekea mkutano huu muhimu.”Mkutano wa Kimataifa wa Walemavu utafanyika Februari 15-17, 2022 na unaandaliwa na Serikali za Norway, Ghana na Shirikisho la Kimataifa la Wenye Ulemavu.

Kuhusu Sightsavers

Sightsavers ni shirika la kimataifa linalofanya kazi katika nchi zaidi ya 30 ili kuondoa vizuizi vinavyoweza kuepukika katika kupigania haki za watu wenye ulemavu. Dira yake ni kuwa na ulimwengu ambao hauna vikwazo vinavyowauzia watu wenye ulemavu kushiriki kwa usawa katika jamii. Sightsavers imekuwa ikifanya kazi Tanzania tangu miaka ya 1970.

Inapigania haki za walemavu kwa kufanya kampeni kwa ajili ya usawa na kupaza sauti za watu wenye ulemavu kwa kushawishi sera za maendeleo ya kitaifa na kimataifa kuwajumuishi watu wenye ulemavu na kwa kusaidia watu hao na mashirika yanayowawakilisha kupitia programu zake za afya na ushirikishwaji.

Jiunge na kampeni ya“Dunia yenye Usawa” kwa ajili ya kukomesha ubaguzi wa watu wenye ulemavu. www.sightsavers.org/equalworld

Kuhusu Sense International

Hii ni sehemu ya Sense International, shirika la kutoa misaada lililosajiliwa Uingereza ambalo linasaidia watu wenye ulemavu wa kutosikia na kuona na aina nyingine za ulemavu katika nchi mbalimbali ambazo zina uhaba wa rasilimali kama; India, Bangladesh, Kenya, Uganda, Peru, Nepal na Romania.

Tangu mwaka 2008, Sense International Tanzania imetekeleza miradi kadhaa katika maeneo ya uchunguzi wa mapema wa mifumo ya fahamu, elimu jumuishi na kuboresha maisha ya watu wenye upofu na uziwi na familia zao.

Watu wenye upofu na uziwi kote ulimwenguni mara nyingi hawajumuishwi katika elimu, huduma za afya na kazi, kwa hiyo, wen-gi huishi maisha mafupi na ya kujitenga.Kwa usaidizi sahihi watu wenye changamoto hiyo wanaweza kuwasiliana, kupata elimu bora na huduma za afya, kujitegemea na kupata kazi. Badala ya kutengwa, wanaweza kustawi na kuishi maisha bora.

Sense International inatamani kuwa na ulimwengu ambamo watu wote wenye upofu, uziwi na ulemavu wa aina nyingine wanaweza kuwa wanajamii sawa na wengine. www.senseinterna-tional.org.uk/

Kuhusu ADD International

Ni mshirika wa harakati za kimataifa za walemavu linalofanya kazi kupigania uhuru, usawa na fursa kwa walemavu wanaoishi katika umaskini barani Afrika na Asia.

ADD International inashirikiana na wanaharakati wa ulemavu barani Afrika na Asia ili kuwasaidia watu hao kupata rasilimali zinazoweza kuwasidia kuendesha maisha yao na usaidizi wanaohitaji ili kuendesha harakati za mabadiliko zenye nguvu.ADD International ilianza kufanya kazi Tanzania tangu 1997 ikipigania ulimwengu ambao walemavu wote hawabaguliwi na wana fursa sawa ndani ya jamii.

Kazi yake inalenga katika kuwawezesha wanaharakati wa ulemavu kujenga mashirika yenye nguvu ambayo husaidia watu wenye ulemavu kufikia ndoto zao.

Inaimarisha harakati za walemavu na kushawishi Serikali, mashirika ya maendeleo ya kimataifa na sekta binafsi kubuni sera na huduma katika kiwango cha kitaifa na kimataifa ambazo zinazingatia watu wenye ulemavu na kutoa masuluhisho jumuishi. www.add.org.uk