Waziri Mkuu azindua Chuo cha CUoM baada ya kupandishwa hadhi na TCU
Mbeya. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametangaza rasmi kukipandisha Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya (CUoM) kinachomilikiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).
Chuo hicho kilianzishwa na mwaka 2013 kama Kituo cha Sauti (SAUT Mbeya Centre) kikiwa ni zao la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT).
Julai 2020, kilipandishwa hadhi na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kuwa Chuo cha Ndaki ya Mbeya, baada ya TCU kujiridhisha kuwa kina hadhi na kuitwa Chuo Kikuu Kishiriki Katoliki Mbeya (CUoM).
Katika taarifa iliyotolewa na uongozi wa Chuo mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu Mkuu wa Chuo imeeleza kuwa mwezi Mei, 2023, TCU ilifanya ukaguzi ili kuona kama kinastahili kupandishwa hadhi ya ngazi ya juu zaidi.
Oktoba 26 mwaka jana, TCU ilikipandisha hadhi Chuo hicho na kuwa Chuo Kikuu kamili ambapo utekelezaji wake uliamuliwa kuanza Januari Mosi 2024.
Baada ya kupanda hadhi
Mwaka 2013 kilipoanzishwa kilikuwa na idadi ya wanafunzi 339 na mpaka kimepandishwa hadhi kimedahili wanafunzi 10,167 wanaosoma programu mbalimbali za shahada ya juu katika elimu, shahada, stashahada na astashahada.
Chuo hicho kina wafanyakazi 177, kati ya hao, wanataaluma ni 131 na wafanyakazi wa upande wa utawala ni 46. Pia wapo maprofesa watano, madaktari wa shahada za uzamivu 21 wahadhiri wasaidizi 81 na wakufunzi 25.
Programu zinazofundishwa
Wakati Chuo kinaanzishwa kilikuwa kinatoa fani mbili; Shahada ya Ualimu na Shahada ya Usimamizi wa Biashara. Kozi nyingine ni Stashahada ya Uzamili katika Elimu.
Katika mwaka wa masomo 2023/24, Chuo kimekuwa kikitoa mafunzo ya shahada sita ambazo ni Shahada ya Sanaa katika Elimu, Shahada ya Uongozi wa Biashara, Shahada ya Sanaa na Mipango katika Miradi ya Maendeleo ya Jamii na programu ya muda mfupi kwa ajili ya kuhudumia wahitaji wanaotuzunguka.
Masomo mengine ni Shahada ya Uhasibu na Fedha, Shahada ya Rasirimali Watu, Shahada ya Sheria, Stashahada na Astashahada katika fani za Teknolojia Habari na Mawasiliano (Tehama), Uongozi wa Biashara, Uhasibu, Ugavi, Manunuzi, Maendeleo ya Jamii, Maktaba na Utunzaji wa Kumbukumbu.
Shughuli za Chuo
Ni kifundisha, kufanya utafiti na kutoa huduma kwa jamii na Chuo hicho kimejiwekea mipango endelevu ya kupanua wigo wa utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia ubora na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuisadia Serikali kuhakikisha inafikia malengo katika kuchangia maendeleo ya dunia kupitia maarifa.
Mafanikio
Pamoja na ongezeko la udahili wa wanafunzi mwaka hadi mwaka, Chuo kimeendelea kuajiri wahadhiri mahiri wenye sifa za kutoa elimu bora kulingana na vigezo vilivyowekwa na Serikali kupitia TCU.
Katika kipindi cha miaka kumi ya kuanzishwa kwake, Chuo kimepata mafanikio makubwa. CUoM ilikuwa na majengo machache kulingana na mahitaji ikiwamo; ukumbi mmoja mkubwa wa mihadhara na kumbi nyingine tano, vyumba vya majadiliano ya kitaaluma vitano na maabara ya kompyuta mbili.
Kwa sasa Chuo kina kumbi kubwa sita za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 400 mpaka 1050 kwa wakati mmoja, kumbi tisa za kawaida zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 100 mpaka 400 vyumba vya majadiliano vya kitaaluma 15, maabara za kisasa zenye kompyuta moja kila moja na maktaba kubwa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja.
Chuo pia kina hosteli za kisasa kwa ajili ya wanafunzi wa kike zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 420 kwa wakati mmoja na maeneo mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi kushiriki michezo ikiwamo; viwanja vya mpira wa miguu, pete, kikapu, wavu vilivyopo eneo la Nzovwe jijini humo.
Changamoto ya umeme
Katika kukabiliana na changamoto hiyo inapojitokeza, Chuo kina jenereta mbili kubwa za dharura, moja ipo makao makuu ya Chuo na nyingine eneo la New Forest.
Hatua hiyo ni kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya kitaaluma kwa ufanisi na kuwezesha wanafunzi kujisomea wakati wote na kwa usalama.
Uwekezaji wa maeneo
Chuo kina maeneo makubwa ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya sasa na upanuzi wa baadaye, huku kikiwa na ekari 148 katika eneo la Nzovwe, ekari 11 (Ilemi), ekari 8 (New Forest) na ekari 4.2 (Makao Makuu).
Mahafari
Novemba 2023, Chuo kiliadhimisha mahafari ya nane tangu kuanzishwa kwake na jumla ya wahitimu 1,600 walitunukiwa Stashahada ya Juu, Shahada na Astashahada katika fani mbalimbali.
“Pamoja na yote, tunapenda kutumia fursa hii kumshukuru Mungu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa kuanzisha Chuo hiki na kukileta mpaka hatua ya kuwa Chuo kikuu kamili,” amesema Mkuu wa Chuo.
Kauli ya Serikali
Akizungumza baada ya kutangaza kukipandisha hadhi, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa Chuo hicho huku akihaidi neema ya upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi na wahadhiri wanaohitaji kujiendeleza.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa Kanisa Katoliki na Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) hivyo kwa mwaka wa fedha 2023/24, Serikali ya Rais Samia imetenga zaidi ya Sh 48 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vikiwemo binafsi,” amesema.
Amesema mbali na mikopo, pia Serikali itaendelea kushirikiana kuhakikisha vyuo hivyo vinaboreshwa ili kutoa elimu bora ya kujiajiri kwa vijana yakiwepo masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) nchini.
“Niagize vyuo vyote vikuu nchini kuanzisha na kuboresha mitaala ya Tehama ambayo itakua chachu kwa vijana kujiajiri pindi wanapohitimu ili kwenda na kasi ya changamoto ya soko la ajira,”ameeleza.
Amesema, Serikali inatambua mchango mkubwa wa uwekezaji wa sekta binafsi kwenye elimu ya vyuo vikuu hivyo tutaendelea kuunga mkono katika swala zima la kuwajengea mazingira wezeshi.
Katika hatua nyingine, Waziri Majaliwa amesema zaidi ya Sh 6.7 bilioni za Mfuko wa Ufadhili wa Rais Samia Suluhu Hassan zitawanufaisha wanafunzi wa masomo ya elimu ya juu, yote hiyo ni kutekeleza ilani ya uchaguzi na kujenga mazingira wezeshi katika sekta ya elimu sambamba na kuboresha mitaala.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameipongeza Serikali kwa hatua ya kukipandisha hadhi CUoM kwani wameujengea heshima mkoa huku akibainisha Serikali imetoa mikopo ya Sh 9.8 bilioni kwa wanafunzi 7,000 katika Chuo hicho.
Naye Mkuu wa Chuo na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu wa Kanisa Kuu Katoliki, Jimbo la Mbeya, Gervas Nyaisonga amesema kuwa maratajio yao kushirikiana na Serikali ni kuhakikisha taaluma na Chuo inawakomboa vijana.
Amesema kuwa tangu mwaka 2013, Chuo hicho kilipoanza na kufikia hatua ya kupandishwa hadhi, idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 339 mpaka 10,167, jambo ambapo linaleta matokeo mazuri.
Nyaisonga ameongeza kuwa sambamba na hilo, pia uwekezaji na uboreshaji miundombinu umepewa kipaumbele tofauti na hapo awali wakati Chuo hicho kinaanza.
Kwa upande wake, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa Chuo hicho kupandishwa hadhi, na ni jambo la kujivunia kwa Mkoa wa Mbeya.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, nikiwa mwakilishi wa wananchi, nipongeze ujio wako katika zoezi la kupandishwa hadhi kwa Chuo hichi cha CUoM ambacho awali kilikuwa ni zao la Chuo cha Mt. Agustino Tanzania (SAUT).