Coop Bank kutenga Sh10 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wajasiriamali
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Coop Bank Godfrey Ng'urah
Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) imetangaza mpango kabambe wa kutenga kiasi cha Sh 10 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vijana na wafanyabiashara wadogo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kutanua huduma za kibenki na kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi la benki hiyo lililopo Morocco, jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Coop Bank, Godfrey Ng'urah alisema taasisi hiyo inatekeleza mpango wa upanuzi unaolenga kusogeza huduma karibu na jamii ambazo hazijafikiwa na mfumo rasmi wa kibenki, huku ikitoa kipaumbele katika upatikanaji wa mikopo nafuu.
Tawi hilo jipya la Morocco ni la sita kufunguliwa na benki hiyo kwa kipindi kifupi huku ikijiandaa kufungua matawi mengine katika mikoa ya Mtwara, Kagera, Mwanza na Arusha ikiwa ni sehemu ya mpango wa kutanua huduma nchi nzima.
“Hili ni tawi letu la sita ndani ya muda mfupi sana. Hatutanui wigo wa huduma zetu kwa ajili ya kukua tu, bali kuhakikisha Watanzania wanapata huduma zinakidhi mahitaji yao,” alisema Ng'urah.
Aliongeza kuwa, lengo la benki hiyo ni kuwa na zaidi ya matawi 12 ifikapo mwisho wa mwaka huu, ambapo Mbeya, Songea na Katavi ni miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mpango huo wa upanuzi unaolenga katika kutumia mfumo wa ushirika kuziba pengo la ujumuishi wa kifedha.
Kwa mujibu wa Ng'urah, kati ya Watanzania zaidi ya milioni 45 wenye uwezo wa kufanya kazi, ni idadi ndogo tu inayofikiwa na huduma rasmi za kifedha. Benki hiyo inalenga kubadili hali hiyo kwa kutumia vyama vya ushirika kama daraja la kufikia makundi ambayo hayafikiwa na huduma rasmi za kibenki.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na akaunti ya benki ifikapo mwaka 2030, huku tukilenga kuwa na wateja hai milioni 10,” alisema.
Alisema kuwa, Tanzania ina zaidi ya vyama vya ushirika 6,000 vilivyosajiliwa, vikiwemo takriban vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) 2,000 na vyama 4,000 vya ushirika wa kilimo na uzalishaji, vikiwa na jumla ya wanachama zaidi ya milioni nane.
Hivyo basi, benki hiyo inalenga kuhakikisha wanachama wote wa ushirika wanaingia katika mfumo rasmi wa kifedha na kutumia huduma za kibenki kikamilifu ifikapo mwaka 2030.
Katika kuwafikia walengwa, Coop Bank imezindua bidhaa maalum kwa ajili ya vijana, wakulima na wajasiriamali wadogo. Ng'urah alifafanua kuwa, benki hiyo inatoa mikopo nafuu yenye riba ya hadi asilimia tisa pekee kwa ajili ya kusaidia biashara zinazoongozwa na vijana pamoja na zile zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo.
“Hatuwezi kuzungumzia ujumuishi wa kifedha bila kuwashirikisha waendesha bodaboda, mama ntilie, wavuvi na wakulima. Hawa ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu,” alisisitiza.
Ili kupunguza gharama za uzalishaji, benki hiyo imeshirikiana na shirika la Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA) kusaidia upatikanaji wa vifungashio, maghala na pembejeo. Ushirikiano huu unatarajiwa kupunguza gharama za pembejeo kwa vijana wanaojishughulisha na kilimo-biashara kwa hadi asilimia 30.
Benki hiyo pia imeingia makubaliano na Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya vijana ili kutoa elimu ya kifedha na kuimarisha mipango ya uwezeshaji wa vijana. Lengo ni kukuza mifumo ya ushirika miongoni mwa biashara za vijana na kuongeza fursa za kupata mitaji.
“Tunataka waendesha bodaboda wajipange katika ushirika ili waweze kumiliki mali kwa pamoja na kuboresha maisha yao kiuchumi,” alisema Ng'urah.
Aidha, alibainisha kuwa jiji la Dar es Salaam lina mchango mkubwa katika uchumi wa ushirika, likiwa na takriban asilimia 80 ya shughuli za ushirika zinazohusiana na benki hiyo. Inakadiriwa kuwa vyama vya ushirika jijini Dar es Salaam vina amana na uwekezaji wa takriban Sh 1.4 trilioni katika taasisi mbalimbali za kifedha.
Katika hatua nyingine, Coop Bank imetambulisha bidhaa mpya za akiba, ikiwemo akaunti inayotoa faida ya hadi asilimia 13.5 kwa lengo la kukuza utamaduni wa kujiwekea akiba miongoni mwa wanachama wa ushirika.
Ng'urah alihitimisha kwa kusema kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za kifedha, na sekta binafsi ni jambo la msingi katika kufikia malengo ya ujumuishi wa kifedha na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa gharama nafuu nchini.