Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutoka kipindupindu mpaka mifumo ya maji na usafi wa mazingira iliyoimarishwa

Mwanachama wa timu ya utoaji huduma ya kijijini akitoa elimu kuhusu mbinu sahihi za kunawa mikono katika soko la Bariadi. Katika Halmashauri 4, timu 10 za utoaji huduma za kijijini ziliundwa na kupewa mafunzo ili kuimarisha uwezo wa jamii na kuhamasisha usafi kupitia shughuli za uhamasishaji zinazotekelezwa na jamii.


Aristarico Shedrack, Afisa Afya mazingira katika Wilaya ya Itilima, bado anakumbuka jioni moja iliyobadili mtazamo wake kuhusu kazi ya afya ya mazingira. Ilikuwa saa moja na nusu jioni.

Akiwa amewasili nyumbani, alipokea simu kutoka kwa mwanamke aliyekuwa akilia kwamba mume wake alikuwa anatapika na kuharisha maji maji yenye rangi kama maji ya mchele.

Kwa haraka, Aristarico alifika katika nyumba hiyo, alitoa msaada wa haraka kwa kumpa mgonjwa maji chumvi maalumu za kurejesha maji mwilini (ORS). Huku akisaidiana na mama huyu walimkimbiza kwenda kituo cha afya kilicho karibu. Hata hivyo, saa chache baadaye, mgonjwa huyo alifariki dunia.

“Tukio lile halitafutika kichwani mwangu,” anasema Aristarico. “Kama Afisa wa afya, unapokea mafunzo, lakini hakuna mafunzo yanayokutayarisha kikamilifu kukabiliana na kifo. Tukio lile linanikumbusha kuwa hii si nadharia; ni maisha ya watu.”


Huduma ya maji na usafi wa mazingira katika mkoa wa Simiyu

Kwa miaka mingi, Mkoa wa Simiyu umekabiliwa na milipuko ya mara kwa mara ya kipindupindu. Hali hiyo imehusishwa na changamoto za usafi wa mazingira, upatikanaji wa maji salama na mitazamo ya kijamii juu ya magonjwa yanayotokana na uchafu wa mazingira hasa ugonjwa wa kipindupindu.

Kufikia Januari 2024, Mkoa wa Simiyu ulikuwa umeripoti visa 824 vya ugonjwa wa kipindupindu na kufikia Desemba 2024, Simiyu ilitajwa kuwa miongoni mwa mikoa iliyoathirika zaidi kitaifa, huku asilimia 61 ya visa vilivyoripotiwa mkoani humo vikitoka katika wilaya za Bariadi na Itilima.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 72 ya wagonjwa yalikuwa kundi la wanawake, watoto na wazee. Hii ni kutokana na majukumu ya kila siku, yakiwamo malezi, utafutaji wa maji, utayarishaji wa chakula, ushiriki katika mazishi, masoko na mikusanyiko ya kijamii. Mazingira haya yaliweza kuongeza uwezekano wa baadhi ya makundi kukutana na mazingira yenye hatari ya maambukizi.

Simiyu ina maeneo mengi ya vijijini yenye makazi yaliyotawanyika. Katika baadhi ya jamii, kaya hutegemea visima vifupi na chemchemi zisizo salama, huku changamoto za kipato, msongamano wa kaya na upatikanaji mdogo wa huduma salama za usafi wa mazingira zikiongeza udhaifu wa mfumo.

Changamoto hizo za kimuundo ziliongezwa na uhaba wa watumishi, mfano, kabla ya mlipuko, wilaya ya Itilima, yenye kata 22, ilikuwa na Maofisa Afya na Mazingira watatu pekee. Hali hiyo iliweka shinikizo kubwa katika ufuatiliaji wa magonjwa, uhamasishaji wa usafi, ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa na ushirikishwaji wa jamii.

Aristarico anakitaja kipindi hicho kuwa miongoni mwa vipindi vilivyokuwa na msongo mkubwa zaidi katika kazi yake.

“Kabla ya mlipuko, kazi yangu ilihusu zaidi ukaguzi na ufuatiliaji wa kawaida,” anasema. “Kipindupindu kilipotokea, nililazimika kutekeleza majukumu mengi kwa wakati mmoja: ufuatiliaji, uhamasishaji, usimamizi wa mazishi na hata kutoa msaada wa kisaikolojia.”


Kutoka mlipuko mpaka mfumo ulio imara

Wakati wa wimbi kubwa na ugonjwa wa kipindupindu katika ya mwezi wa nane na kumi na mbili 2024. Halmashauri ya wilaya ya Bariadi na Itilima tayari zilikuwa sehemu ya programu ya WASH Systems for Health (WS4H), inayotekelezwa na SNV Tanzania.

Mwanamke akisafisha choo katika kijiji cha Budarabujiga, wilayani Itilima, kama sehemu ya juhudi za kuzuia kipindupindu. Hii inaakisi ushirikiano wa WS4H na timu za wilaya, kata na vijiji katika kuhamasisha matumizi ya vyoo, usafi na matengenezo yake katika wilaya nzima.

Wilaya hizo zilichaguliwa kutokana na viashiria duni vya maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi vilivyohitajika kuboreshwa Programu ilirekebisha na kubadili utekelezaji wake wa awali na kwa haraka, ikitumia mlipuko wa kipindupindu kama fursa ya kuunganisha udhibiti wa dharura na uimarishaji wa mfumo wa muda mrefu.

Mtazamo huo ulilenga kuongeza uwezo wa halmashauri katika kupanga, kuratibu, kufuatilia na kuripoti, badala ya kutegemea hatua za muda mfupi pekee.

Kupitia programu hiyo, maofisa Afya na Mazingira wanane (8) walipelekwa katika ngazi ya kata. Walijengewa uwezo na kuunganishwa na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs) pamoja na viongozi wa vijiji.

Jukumu lao halikuishia katika kudhibiti mlipuko; walisaidia kuingiza kinga ya kipindupindu katika mifumo ya kawaida ya wilaya na jamii.


Kuvunja hofu na taarifa potofu

Maofisa afya hawa, walifika wakati jamii ikiwa na hofu na taarifa zisizo sahihi kuhusu kipindupindu. Baadhi ya watu waliuchukulia ugonjwa huo kuwa hali ya kawaida ya msimu, laana au matokeo ya uchawi.

Kwa sababu ya hofu na unyanyapaa, baadhi ya familia zilichelewa kutoa taarifa na kuanza kwa kutumia tiba za jadi. Mazishi na sherehe za kijamii zilikuwa miongoni mwa mazingira yaliyohusishwa na ongezeko la maambukizi, na katika kipindi fulani ziliripotiwa kuchangia visa vipya 20 hadi 30 kwa siku.

Hatua za awali zililenga kuwashirikisha viongozi wa kijamii wenye ushawishi ili kusaidia jamii kuelewa na kukubali taratibu salama za afya ya umma.

Katika moja ya mazishi yaliyokuwa na mvutano mkubwa, familia ilisisitiza kufuata mila zilizoweza kuongeza hatari ya maambukizi. Maafisa afya hawa walishirikiana na wazee wa kijiji walioaminiwa na jamii kueleza hatari na kujadiliana kuhusu njia salama za kuendesha mazishi. Ushirikiano huo ulipunguza mvutano na kuongeza kukubalika kwa hatua za kinga.

Hatua nyingine ilikuwa kuimarisha mfumo wa utoaji taarifa kupitia viongozi wa vijiji, watu wenye ushawishi na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii. Juhudi hizo ziliendelea kupitia mikutano ya jamii, ukaguzi wa maeneo ya umma, ziara za kaya na usimamizi wa afya katika sherehe na mazishi.

Maofisa Afya ya Mazingira waliwajengea uwezo Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 394 katika ufuatiliaji wa magonjwa, matumizi ya ORS, usafishaji wa maji, utoaji wa taarifa na rufaa.

Mtandao huo ulifuatilia wagonjwa 117 waliothibitishwa kuwa na kipindupindu pamoja na watu 1,058 waliokutana nao, ambapo 41 waliripotiwa kuambukizwa, hali inayoonesha umuhimu wa taarifa za mapema, ufuatiliaji wa karibu na kinga zinazoongozwa na jamii.


Sauti za jamii zilizoleta mabadiliko

Katika jamii zenye mila na imani za jadi, mabadiliko yalihitaji uvumilivu, uaminifu na ushahidi unaotokana na uzoefu wa wananchi wenyewe. Ushuhuda wa manusura wa kipindupindu ukawa nyenzo muhimu ya kuhamasisha jamii.

Mmoja wa manusura alieleza jinsi alivyonusurika baada ya matibabu ya muda mrefu yaliyogharimu fedha nyingi. Ushuhuda wake uliisaidia jamii kuelewa kuwa kipindupindu ni ugonjwa halisi, unaweza kusababisha madhara makubwa, lakini pia unaweza kuzuilika kwa hatua sahihi.

Amina, mmoja wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoka Itilima na mama wa watoto wanne, alijitokeza kuwa sauti muhimu katika kuwahamasisha wanawake.

“Baada ya kuona jirani yangu akimpoteza mtoto wake kutokana na kipindupindu, nilijua lazima tuchukue hatua,” anasema. “Nilianza kuwafundisha wanawake waliokuwa wakichota maji jinsi ya kuyatibu na kutambua dalili za awali. Leo, nao wanawafundisha wengine majumbani na masokoni. Sisi wanawake tunabeba sehemu kubwa ya jukumu la maji na kuhudumia wagonjwa; kwa hiyo, tuna uwezo pia wa kuongoza suluhisho.”

Mazishi na sherehe zilianza kusimamiwa kwa karibu zaidi ili kuhakikisha uwepo wa vituo vya kunawa mikono, utunzaji salama wa chakula, matumizi ya vyoo na maji yaliyotibiwa.


Gharama za mlipuko kwa kaya na huduma za jamii

Mlipuko uliweka mzigo mkubwa wa kifedha kwa kaya. Baadhi ya familia ziliripoti kutumia kati ya Sh milioni 2 na Sh milioni 5 kwa matibabu ya wanafamilia, huku nyingine zikilazimika kuuza mifugo na ardhi ili kupata fedha.

Mahudhurio ya wanafunzi shuleni pia yalipungua kutokana na hofu ya maambukizi. Shule ziliweka vituo vya kunawa mikono nje ya madarasa na kuwataka wanafunzi kunawa mikono kabla ya kuingia darasani.

Wakuu wa shule waliimarisha ushirikiano na Maofisa Afya ya Mazingira katika utoaji wa elimu ya afya na taarifa za haraka kuhusu visa vinavyoshukiwa. Hatua hiyo iliunganisha shule na mfumo mpana wa ufuatiliaji na kinga katika jamii.


Matokeo ya awali

Kutokana na ushirikiano wa maafisa afya, viongozi wa ngazi zote, jamii na kimila, zaidi ya asilimia 85 ya maeneo ya mazishi yaliripotiwa kuwa na vituo vya kunawa mikono na taratibu salama za utunzaji wa chakula.

Kupitia vikao na mafunzo yalitolewa na SNV zilisaidia kuimarisha uwezo wa halmashauri katika kupanga na kutekelezaji mipango ya maji na usafi wa mazingira Halmashauri ya Bariadi na Itilima ziliweza kuandaa dira na mpango kazi wa kuimarisha huduma ya afya na usafi wa mazingira, wenye hatua sahihi za kuondoa jamii kutoka kutokutumia choo na kuweza kuwa na jamii yenye vyoo bora na afya, huku misingi ya ushirikishwaji wa makundi maalumu ya jamii na athari za mabadiriko ya tabia ya nchi zikipewa kipaumbele.

Katika ngazi ya taifa, uzoefu wa programu ya WS4H mkoani Simiyu yaliyochangia katika kuandaa Mwongozo wa Kitaifa wa kutoa huduma ya maji na usafi wa mazingira katika maeneo ya dharula wa mwaka 2025, unaosisitiza usawa wa kijinsia, ujumuishaji wa watu wenye ulemavu, ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ya jamii na ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aristarico anaeleza kuwa kipindupindu ni kipimo cha uwezo wa mfumo huduma ya maji na usafi wa mazingira “Mahali ambapo juhudi zilijikita katika kusambaza vifaa na kusimamia sheria pekee, matokeo yalikuwa ya muda mfupi,” anasema.

“Lakini kinga ilipounganishwa katika shughuli za kila siku za taasisi, miundo ya jamii na uwajibikaji wa viongozi wa maeneo husika, maambukizi yalipungua.”

Kwa mtazamo wake, imani ya wananchi ilijengwa kwa kufanya kazi karibu nao. Maofisa Afya ya Mazingira walifanya kazi ndani ya jamii, wakizungumza lugha inayoeleweka, wakiheshimu mila za wenyeji na kushughulikia changamoto za kila siku kwa ushirikiano.

Kwa Simiyu, mlipuko wa kipindupindu umebaki kama historia iliyoibua uwekezaji katika uwezo wa taasisi, mitandao ya jamii, mifumo ya taarifa na uwajibikaji wa viongozi na hii ndiyo tofauti kati ya kushughulikia mlipuko/dharura na kujenga mfumo unaoweza kuzuia, kugundua na kukabiliana na hatari zinazofuata.


Programu hii inafadhiliwa na Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza (FCDO), na kutekelezwa na SNV kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania.