Mchango wa JICA katika kuendeleza kilimo Tanzania
Heri ya Siku ya Nanenane kwa wakulima wote wa Tanzania wanaofanya kazi kwa bidii
Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japani (JICA) linatambua ari ya wakulima na jukumu muhimu wanalotekeleza katika kulisha taifa na kujenga mustakabali endelevu zaidi.
Tunajivunia kushirikiana na wakulima na Serikali kusaidia maendeleo ya kilimo, kukuza mashirikiano ya ubunifu ili kuwawezesha wakulima. Kaulimbiu ya Nanenane mwaka huu ni “Chagueni viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi inaangazia sana matarajio yetu ya pamoja ya kupata chakula na ustawi wa Tanzania.
Mkutano wa 9 wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika, (TICAD9), utafanyika mwezi huu wa Agosti nchini Japan. Moja ya mada ya TICAD 9 ni “Tomoni Africa” au “Pamoja Africa”. Sambamba na hili, JICA imejitolea kuimarisha zaidi shughuli zetu katika sekta ya kilimo nchini Tanzania, kuongeza tija, kuboresha maisha, na kuzingatia maendeleo ya rasilimali watu kwa kuzingatia ari ya ushirikiano na ukuaji wa pamoja. Sekta ya kilimo ni muhimu kwa utekelezaji wa Dira ya Tanzania 2050 na ukuaji wa baadaye wa Tanzania, hata hivyo, maendeleo yake yanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile mabadiliko ya tabia nchi na usalama wa chakula, hivyo kwa kutumia rasilimali za JICA za muda mrefu za ushirikiano tutakuza zaidi ushirikiano na Serikali ya Tanzania, sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo, wakulima na wadau wengine ili kukuza maendeleo ya kilimo. “Kwa pamoja tujenge ushirikiano imara utakaojenga mustakabali wa kilimo na kuhakikisha ustawi wa vizazi vijavyo.”
Tangu mwaka 1970, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) limekuwa likihamasisha uboreshaji wa uzalishaji kibiashara na ukuaji wa viwanda kupitia sekta ya kilimo ili kuendana na vipaumbele vya nchi, ili kuchangia ukuaji wa uchumi mzima na maendeleo ya jamii ya Tanzania. JICA imetoa msaada kwa nchi nzima katika miradi ya kujenga uwezo wa taaluma na ujenzi wa miundombinu pamoja na sekta ya uvuvi na mifugo kupitia programu kuu mbili zifuatazo.
1. Programu ya kukuza kilimo biashara/viwanda
Mradi wa Uwezeshaji na Kukuza Kilimo Kupitia Matumizi ya Mbinu ya SHEP (TANSHEP2): Aprili 2025-Oktoba 2029
Mbinu ya SHEP ya JICA inawahamasisha wakulima kufanya uchunguzi wa soko kabla ya kuanza kuzalisha ili kuamua ni mazao gani ya kuzalisha, ili wakulima waweze kuongeza mapato yao kwa ufanisi. Kwa dhana ya “Anzia Sokoni, Malizia Shambani, Kwa Kipato Zaidi”, Wizara ya Kilimo (MoA) na Ofisi ya Rais - Utawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa (PO-RALG) kwa ushirikiano na JICA imeanza awamu ya 2 ya mradi huo, ikilenga kusambaza mbinu ya SHEP kote nchini.
Mshauri wa zana za Kilimo: Mei 2024- Mei 2027
JICA imetuma wataalam kusaidia kuhamasisha matumizi ya zana za kilimo huku ikiimarisha kazi saba za AFICAT na uendelezaji wake. Mradi huu unatarajiwa kuchangia katika uboreshaji wa tija ya kilimo nchini Tanzania.
AFICAT (Kituo cha Ubunifu cha Teknolojia ya Kilimo-Afrika) ni mpango wa kukuza Teknolojia ya hali ya juu na utumiaji dhana za kilimo kusini mwa jangwa la Sahara Afrika kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.
Mradi wa kuendeleza Kilimo na Maendeleo vijijini (TSL): Mei 2025- Mei 2030
JICA inashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kutoa mikopo midogo ya muda wa kati na mrefu kwa vikundi vya wakulima na wanufaika wengine. Mradi huo unatarajiwa kuchangia uboreshaji wa tija ya kilimo kupitia upatikanaji wa mtaji wa bei nafuu Mazao lengwa: mpunga, mahindi, ngano, alizeti na mazao ya bustani kwa wanawake na vijana).
Ubia kati ya Sekta ya Umma na Kibinafsi:
JICA pia inalenga kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania kwa kutumia uzoefu na ujuzi wa makampuni binafsi ya Japani ambayo kwa sasa yana ushirikiano na makampuni yanayohusiana na kilimo kama vile Kikkoman Corp na Yamamoto Co., Ltd.
2. Programu ya Kuimarisha Uzalishaji wa zao la Mpunga
Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Mpunga katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” (TANRICE 3): Juni 2023-Juni 2028
Katika miaka ya 1970, JICA ilianzisha Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro (KATC) ili kuimarisha mifumo ya utendaji kazi wa mbinu za mafunzo zinazofaa kwa mashamba ya wakulima. Kisha, kupitia miradi ya ushirikiano wa kiufundi wa TANRICE1 na TANRICE2, JICA imetoa mafunzo ya kiufundi ya kilimo cha mpunga katika maeneo kusudiwa hasa katika maeneo ya umwagiliaji, ambayo yaliongeza tija ya wakulima kutoka 3.2t/ha hadi 4.5/ha.
Katika mradi wa TANRICE 3 unaoendelea, JICA inafanya kazi ili kuboresha uzalishaji wa mpunga kinachotegemea mvua, pamoja na mafunzo katika teknolojia ya kilimo cha mpunga cha umwagiliaji. Inatarajiwa kuwa idadi ya wakulima wanaotumia mbinu za uzalishaji wa mpunga zilizopendekezwa na mradi huu itaongezeka, hali ambayo itasababisha uzalishaji zaidi wa mpunga nchini Tanzania.
Mshauri wa Maendeleo ya Umwagiliaji: Septemba 2023-Septemba 2025
Tangu 2010, JICA imekuwa ikisaidia (NIRC kuandaa miongozo ya kina ya skimu ya umwagiliaji (CGLs), kuandaa mpango kabambe, kujenga miundombinu na kutoa mafunzo kwa maafisa wa umwagiliaji. Kwa sasa, JICA imeajiri Mshauri kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) ili kuboresha zaidi uwezo wa maafisa wa umwagiliaji (hasa waajiriwa wapya).
Mradi wa Kuwezesha Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo Tanzania: Aprili 2023-Juni 2028
JNi mradi wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za kimarekani milioni 70 ambao utasaidia upatikanaji wa pembejeo za kilimo hasa mbegu bora na mbolea, unaolenga kuboresha tija na faida ya mazao ya kipaumbele (ngano, alizeti na mpunga) kupitia ushirikiano wa ufadhili na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Makadirio ya jumla ya wanufaika wa moja kwa moja ni kaya 1,200,000, ambayo ni sawa na watu 4,800,000, ambapo asilimia 40 ni wanawake na vijana.
3. Mengineyo
Mradi wa kutengeneza mkakati wa pamoja wa kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kipaumbele kwa kutumia dhana ya Afya moja, Elimu na Ushirikiano baina ya serikali na Sekta binafsi: Julai 2024-Juni 2029
Mradi huu mpya unalenga kukabiliana na changamoto za magonjwa ya kuambukiza kati ya wanyama na binadamu yaani zoonotiki, yasiyo ya kipaumbele kama bruselosisi na kifua kikuu ambayo yapo kwenye sekta ya mifugo Tanzania. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya vyuo vikuu vya nchini Japani na Tanzania kwa lengo la kuweka mikakati ya kuzuia na kudhibiti magonjwa haya katika mkoa wa Morogoro.