Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sekta ya mifugo Zanzibar inavyopaa chini ya Idara ya Maendeleo ya Mifugo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi na mke wake, Mama Mariam Mwinyi akikagua miundombinu kwenye Shamba la Ufugaji wa Kuku la Zan Breed Limited.

Sekta ya mifugo ni moja ya nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa jamii. Kwa Zanzibar, sekta hii imeendelea kukua na kuimarika kutokana na juhudi za Serikali pamoja na taasisi zake mbalimbali, hususani Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar.

Idara hii imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha ufugaji unakuwa wa kisasa, wenye tija na unaochangia kwa kiwango kikubwa ustawi wa wananchi pamoja na maendeleo ya uchumi wa visiwa hivyo.

Katika mahojiano maalum na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar, Asha Zahran Mohammed alieleza kwa kina hatua mbalimbali ambazo sekta ya mifugo imepitia, mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo pamoja na mikakati ya kuifanya sekta hiyo kuwa moja ya vyanzo vikuu vya mapato kwa wananchi na Serikali.


Sekta ya mifugo Zanzibar: Ilipotoka, ilipo na inapoelekea

Akizungumzia historia ya sekta ya mifugo Zanzibar, Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa miaka mingi ufugaji ulikuwa ukifanyika kwa njia za asili na kwa kiwango kidogo, huku wafugaji wengi wakitumia mifugo kwa matumizi ya familia pekee kama vile chakula na kipato kidogo.

“Kwa muda mrefu ufugaji ulikuwa unafanyika kwa mfumo wa jadi. Wafugaji walikuwa wachache na hawakuwa na teknolojia wala utaalamu wa kisasa wa kuboresha mifugo yao,” alieleza.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi na mke wake, Mama Mariam Mwinyi akikagua miundombinu kwenye Shamba la Ufugaji wa Kuku la Zan Breed Limited.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko makubwa kutokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia taasisi zake mbalimbali, ikiwemo Idara ya Maendeleo ya Mifugo.

Serikali imeweka mikakati ya kuboresha mifugo, kui-marisha huduma za ugani, kudhibiti magonjwa ya mifugo na kuwasaidia wafugaji kuongeza uzalishaji. Kwa sasa, sekta ya mifugo Zanzibar imeanza kuonesha dalili za kukua kwa kasi, huku idadi ya wafugaji na mifugo ikiongezeka.

Aidha, matumizi ya mbinu za kisasa za ufugaji yanaendelea kuongezeka, jambo ambalo linaongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, nyama na bidhaa nyingine za mifugo. Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, malengo ya baadaye ni kuifanya sekta ya mifugo kuwa ya kisasa zaidi, ya kibiashara, yenye ushindani na inayoweza kukidhi mahitaji ya soko la ndani na hata la nje.


Historia ya Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar

Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar ilianzishwa kwa lengo la kusimamia na kuendeleza sekta ya mifugo katika visiwa vya Zanzibar. Tangu kuanzishwa kwake, idara hiyo imekuwa na jukumu la kuratibu shughuli zote zinazohusiana na ufugaji pamoja na kuhakikisha kuwa wafugaji wanapata msaada wa kitaalamu unaohitajika. Kwa miaka mingi, idara imeendelea kupanua wigo wa shughuli zake kwa kuanzisha programu mbalimbali zinazolenga kuboresha ubora wa mifugo, kuimarisha afya ya mifugo na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za mifugo.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa kadri miaka ilivyopita, idara imekuwa ikibadilika ili kuendana na mahitaji mapya ya sekta ya kilimo na maendeleo ya uchumi.


Majukumu na Kazi za Idara ya Maendeleo ya Mifugo

Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar ina majukumu makubwa katika kuhakikisha sekta ya mifugo inaendelea kukua na kuwa na tija. Mojawapo ya majukumu yake makuu ni kutoa huduma za ugani kwa wafugaji ili kuwasaidia kutumia mbinu bora za ufugaji.

Aidha, idara inasimamia udhibiti wa magonjwa ya mifugo kwa kutoa chanjo na huduma za tiba kwa mifugo. Kazi hii ni muhimu katika kulinda afya ya mifugo na kuhakikisha uzalishaji hauathiriki.

Pia, idara inahusika katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika ufugaji pamoja na kuwasaidia wafugaji kupata mifugo bora yenye uwezo mkubwa wa uzalishaji na masoko kwa ajili ya mazao ya mifugo.

Majukumu mengine ni pamoja na kukusanya na kuchambua takwimu za sekta ya mifugo, kuandaa sera na mikakati ya maendeleo ya sekta hiyo pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuboresha ufugaji.


Mchango wa Idara ya Maendeleo ya Mifugo katika uchumi

Sekta ya mifugo ina mchango mkubwa katika sekta ya kilimo na uchumi wa Zanzibar kuliko sekta zote zilizopo chini ya wizara ya Mifugo ambapo kwa sasa sekta hiyo inachangia asilimia 10.5 katika sekta ya mifugo ambayo ni mhimili mkubwa wa uchumi wa Zanzibar ikichangia asilimia 24.3 ya pato la Taifa kwa mwaka 2024.

Kupitia juhudi za Idara ya Maendeleo ya Mifugo, uzalishaji wa bidhaa za mifugo umeongezeka na kusaidia kuongeza upatikanaji wa chakula chenye lishe bora kwa wananchi. Bidhaa kama maziwa, nyama na mayai zimekuwa zikizalishwa kwa kiwango kikubwa zaidi, hali inayochangia kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wafugaji.

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa sekta ya mifugo pia inatoa ajira kwa wananchi wengi, hasa vijana na wanawake, kupitia shughuli mbalimbali kama ufugaji, biashara ya bidhaa za mifugo na huduma zinazohusiana na sekta hiyo.

“Sekta ya mifugo si tu chanzo cha chakula bali pia ni chanzo muhimu cha kipato kwa wananchi. Kupitia ufugaji, watu wengi wameweza kuboresha maisha yao,” alieleza.


Ushirikiano na wafugaji na wadau

Moja ya mambo muhimu yanayochangia mafanikio ya Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar ni ushirikiano wake wa karibu na wafugaji p amoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Zanzibar.

Idara imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na wafugaji kupitia mafunzo, mikutano ya uhamasishaji na huduma za ugani. Kupitia programu hizi, wafugaji wanapata elimu kuhusu mbinu bora za ufugaji, lishe ya mifugo na namna ya kukabiliana na magonjwa ya mifugo.

Aidha, idara imekuwa ikiwahamasisha wafugaji kuunda vikundi na vyama vya ushirika ili waweze kushirikiana katika uzalishaji na masoko ya bidhaa za mifugo. Idara pia imnekuwa na ushirikiano na wadau mbalimbali kupitia utekelezaji wa miradi yenye lengo la kuongeza tija katika sekta ya mifugo Zanzibar.

“Kwenye suala la ushirikiano na wadau tumepiga hatua kubwa na umetusaidia katika kupata miradi mikubwa iliyoleta mapinduzi katika sekta ya mifugo Zanzibar,” anasema.


Uwekezaji na miradi ya maendeleo

Katika kuimarisha sekta ya mifugo, Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo.

Idara hiyo kwa sasa iko katika ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambapo wanatekeleza mradi wa miaka 10 wa kukopesha kuku na ng’ombe wa maziwa kwa wafugaji ambapo mpaka sasa zaidi ya wafugaji 246 (93 Unguja na 153 Pemba) wamenufaika na mradi huo.

Pia kuna mradi mwingine unaotekelezwa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ambao unalenga kuwasaidia wafugaji kufunga kisasa pamoja na kuwategenezea fursa za upatikanaji wa masoko ya ndani na nje.

Serikali pia inatekeleza mradi wa kimkakati wa kiwanda cha kuzalisha vifaranga, ikiwa ni pamoja na kituo cha Kwambani chenye uwezo wa kuzalisha vifaranga 30,000 kwa wiki. Mradi huu unalenga kuimarisha sekta ya ufugaji kuku, kupunguza utegemezi wa kuagiza vifaranga nje ya nchi, na kuongeza kipato kwa wafugaji.

Mradi mwingine ni wa Shamba la Ufugaji wa Kuku wa Zan Breed Limited ambao ni wa kimkakati na wa kimataifa unaoonesha uwezo wa Zanzibar kuanzisha na kuendesha miradi mikubwa ya uzalishaji wa ndani.

Mradi huo una mtaji wa Dola za Marekani milioni 10 na unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 1,000 na una uwezo wa kuzalisha kuku 800,000 kwa mwezi, pamoja na huduma za kliniki ya kuku, kiwanda cha nafaka, maabara na mfumo wa kuchakata maji, hatua itakayochochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya mifugo na uchumi wa Zanzibar.

Miradi hiyo na mingine inalenga kuboresha miundombinu ya ufugaji, kuongeza uzalishaji wa mifugo bora pamoja na kuimarisha huduma za afya ya mifugo. Miradi hii imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza tija ya ufugaji na kuboresha maisha ya wafugaji.


Mafanikio ya Idara ya Maendeleo ya Mifugo

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, moja ya mafanikio makubwa ya idara ni kuongezeka kwa uelewa wa wafugaji kuhusu mbinu bora za ufugaji pamoja na kuimarika kwa huduma za afya ya mifugo.

Aidha, idadi ya wafugaji wanaotumia mifugo bora imeongezeka, jambo ambalo limeongeza uzalishaji wa maziwa na nyama. Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa ushiriki wa vijana na wanawake katika sekta ya mifugo, hali inayosaidia kuongeza ajira na kipato kwa wananchi.


Changamoto na mikakati ya baadaye

Pamoja na mafanikio hayo, sekta ya mifugo Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa maeneo ya malisho, magonjwa ya mifugo na ukosefu wa mitaji kwa wafugaji wadogo. Hata hivyo, Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto hizo.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani, kuongeza uwekezaji katika sekta ya mifugo na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika ufugaji. Aidha, idara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya mifugo inaendelea kukua na kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Zanzibar.

Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya mifugo na kuboresha maisha ya wafugaji. Kupitia mikakati yake mbalimbali, idara hiyo imefanikiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya ufugaji na kuweka msingi imara wa maendeleo ya baadaye.

Kadri juhudi hizi zinavyoendelea, sekta ya mifugo ina kila sababu ya kuaminiwa kuwa itakuwa moja ya nguzo muhimu za maendeleo ya kiuchumi katika Zanzibar na chanzo kikuu cha ajira na kipato kwa wananchi.