Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TEAGTL yaandika historia bandari ya Dar es Salaam, yavunja rekodi ya kuhudumia shehena ya makasha

Kampuni ya Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL) imeweka rekodi mpya ya kihistoria katika Bandari ya Dar es Salaam baada ya kufanikiwa kuhudumia kiwango cha juu zaidi cha shehena ya makasha kuwahi kufanyika ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Ndani ya mwezi Mei 2026 pekee, kituo hicho kimehudumia jumla ya TEUs (futi 20) 85,243, hatua inayotajwa kuwa ni kielelezo cha mabadiliko makubwa ya kiutendaji na ufanisi yanayoendelea katika lango hilo kuu la biashara nchini.

Mafanikio hayo hayakuja ghafla, kwani takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Mei 2026, kumekuwa na ongezeko la shehena kwa asilimia 10.25 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025. Tangu ilipoanza kufanya shughuli zake, TEAGTL imekuwa ikitekeleza mkakati unaolenga watu, wateja na ufanisi wa kiutendaji.

Kupitia uwekezaji mkubwa katika kuwaendeleza wafanyakazi, kuimarisha ushirikiano na wateja, kurahisisha taratibu za kazi na kutumia ubunifu wa kiteknolojia, kampuni hiyo imefanikiwa kuongeza tija katika kituo hicho, kupunguza muda wa meli kuhudumiwa na kuimarisha uhakika wa huduma.

Aidha, kuna maboresho ya kiteknolojia ambayo yamehusisha matumizi ya mfumo wa kisasa zaidi wa uendeshaji wa kituo (TOS), huku mifumo ya kidijitali kama vile ufuatiliaji wa makasha na ratiba za moja kwa moja za meli zikiwawezesha wateja kufuatilia mizigo yao kwa wakati husika.

TEAGTL pia inatekeleza taratibu za kimataifa za ubora, ikiwemo mfumo wa ‘Fixed Berthing Window’ (FBW), ambao umeongeza uaminifu wa huduma na kupunguza muda wa meli kusubiri kuhudumiwa. Kupitia mkakati wake unaoweka kipaumbele kwa wafanyakazi na kuongozwa na teknolojia, sambamba na maboresho ya michakato na matumizi ya mifumo ya kidijitali, kampuni hiyo imekuwa ikipandisha viwango vya utendaji wa bandari na kuongeza tija katika mnyororo wa usambazaji wa bidhaa kikanda.

Takwimu hizi zinazidi kuimarisha nafasi ya Bandari ya Dar es Salaam kama lango kuu la kimkakati kwa Tanzania na kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati, hali inayochochea ukuaji wa biashara na maendeleo ya kiuchumi ya kikanda.

Akizungumzia mafanikio hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TEAGTL, Kapteni Jeyaraj Thamburaj amesema mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano, weledi wa wafanyakazi, na imani ya wadau wa sekta hiyo. “Kuhudumia makasha 85,243 ndani ya mwezi mmoja isingewezekana bila jitihada za wafanyakazi wetu ambao kila siku wanapambana kuhakikisha tunafikia malengo yetu,” alisema Kapteni Thamburaj huku akiishukuru Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wateja wao kwa imani waliyonayo kwa kampuni hiyo.

“Naishukuru TPA na mamlaka nyingine kwa ushirikiano wao pamoja na wateja wetu kwa imani yao kubwa waliyonayo kwetu. TEAGTL imejiandaa vyema kuwa mshirika wa sekta za uingizaji na usafirishaji wa bidhaa (EXIM) nchini na kuunga mkono harakati za ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia uharakishaji wa usafirishaji wa mizigo, muunganiko bora wa huduma na ushirikiano katika biashara ya kimataifa,” alisema Kapteni Thamburaj.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa ameipongeza TEAGTL akibainisha kuwa ufanisi huo ni matunda ya maono ya Serikali ya kujenga mfumo wa bandari wa hadhi ya kimataifa kupitia ushirikiano na sekta binafsi (PPP).

“TPA imejizatiti katika kuweka mazingira wezesha yanayovutia uwekezaji na ubunifu. Ushirikiano huu na TEAGTL umeongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam na kusaidia azma ya ukuaji wa uchumi wa nchi. Natoa pongezi kwa TEAGTL kwa kufikia hatua hii ya kihistoria. Mafanikio haya ni kielelezo cha mabadiliko makubwa yanayoletwa na ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kusukuma mbele vipaumbele vya kitaifa,” amesema Mbossa.

Mbali na uwekezaji katika rasilimali watu, siri ya mafanikio hayo imetajwa kuwa ni matumizi ya teknolojia ya kisasa, ikiwemo mfumo wa uendeshaji wa kituo (TOS) na huduma za kidijitali zinazomwezesha mteja kufuatilia mzigo wake popote ulipo. Aidha, mfumo wa ‘Fixed Berthing Window’ (FBW) umesaidia kupunguza muda wa meli kusubiri na kuongeza uhakika wa huduma.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tanzania (DOWUTA), Ernest Gao amesema mafanikio hayo ni fahari kwa kila mfanyakazi wa kituo hicho akisisitiza kuwa uwekezaji katika mafunzo na usalama kazini umechochea tija hiyo.

“Hatua hii ya kihistoria ni fahari kwa kila mfanyakazi katika kituo hiki. Nyuma ya mafanikio haya ya kuhudumia shehena ya TEUs 85,243, kuna juhudi za dhati za wafanyakazi wetu ambao wanajituma kila uchao kufikia malengo ya taasisi,” amesema Gao.

Amesema, pia wanathamini dhamira ya uongozi katika kuwekeza kwa rasilimali watu kupitia mafunzo na uendelezaji wa ujuzi pamoja na kutilia mkazo ujenzi wa mazingira salama na yenye tija ya kufanyia kazi. Kwa niaba ya DOWUTA, nawapongeza wafanyakazi wote, uongozi wa TEAGTL na washirika wetu wa TPA kwa mafanikio haya makubwa.

Hatua hii inazidi kuimarisha nafasi ya Bandari ya Dar es Salaam kama kitovu muhimu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku ikirahisisha usafirishaji wa mizigo na kuunganisha Tanzania na masoko ya kimataifa.

UFUATILIAJI WA KONTENA

RATIBA YA MELI