Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM Geita yawekeza Sh3.4 bilioni, yajenga vibanda 250 kukuza mapato

Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akikagua mradi wa ujenzi wa jengo la biashara unaotekelezwa na CCM Wilaya ya Geita.

Muktasari:

  • Mradi wa ujenzi wa jengo lenye vibanda zaidi ya 250 unatarajiwa kuiingizia CCM Wilaya ya Geita zaidi ya Sh54 milioni kwa mwezi pindi utakapokamilika.

Geita. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita kinatarajia kutumia zaidi ya Sh3.4 bilioni kutekeleza mradi wa kimkakati wa ujenzi wa jengo la vibanda vya biashara zaidi ya 250, likilenga kuimarisha uchumi wa chama kuanzia ngazi za chini.

Mradi huo unaotekelezwa katika eneo la Sabasaba mjini Geita unatarajiwa kuongeza mapato ya chama hadi kufikia zaidi ya Sh54 milioni kwa mwezi mara utakapokamilika.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Aprili 17, 2026 mbele ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, Katibu wa CCM Wilaya ya Geita, Michael Msuya amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya chama makao makuu ya kujenga uchumi imara wa chama.

Msuya amesema mbali na mradi huo, chama kimefanikiwa kutekeleza miradi mingine ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa ofisi za chama katika ngazi ya kata na wilaya pamoja na mradi uliopo Katoro.

“Tumejenga miundombinu ambayo hata imekuwa msaada kwa vyama vingine vya siasa visivyo na ofisi, kwani tumekuwa tukipokea mawasiliano yao yanapotokea mialiko ya wadau,” amesema Msuya.

Ameongeza kuwa miradi hiyo inasaidia kukiwezesha chama kujitegemea kifedha na kutekeleza majukumu yake bila vikwazo, huku pia ikitumika kama darasa la vitendo kwa viongozi katika usimamizi wa miradi.

“Viongozi wanapata uelewa wa namna bora ya kusimamia miradi, hivyo wanapokwenda kukagua miradi ya Serikali wanakuwa na ujuzi wa kutosha kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa,” amesema.

Kwa upande wake, Kihongosi aliipongeza CCM Geita kwa ubunifu huo na kuitaja kama mfano wa kuigwa na wilaya nyingine nchini.

Amesema mkutano mkuu wa 10 wa CCM uliweka azimio la kuimarisha uchumi wa chama na jumuiya zake, akisisitiza kuwa miradi kama hiyo ndiyo msingi wa kujitegemea kifedha.

“Wapo wanaouliza CCM inapata wapi fedha za shughuli zake, majibu yako kwenye miradi kama hii. Ukiwa na uwekezaji wa aina hii unakuwa na uhakika wa kuendesha shughuli zako kwa ufanisi,” amesema.

Amewataka viongozi wa chama ngazi zote kuendelea kuwekeza katika miradi ya kibiashara ili kupanua vyanzo vya mapato.

Katika hatua nyingine, Kihongosi alikagua kituo cha kupooza umeme cha Mpomvu mjini Geita na kuwataka wananchi kuendelea kuomba kuunganishiwa umeme ili kunufaika na nishati hiyo katika shughuli za kiuchumi.

Alisema kituo hicho kilichogharimu zaidi ya Sh23 bilioni kinapaswa kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na mkoa kwa ujumla.

Awali, Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Geita, Michael Mbwana alisema idadi ya wateja imeongezeka kutoka 15,000 mwaka 2020 hadi zaidi ya 150,000 kwa sasa.

Alisema kuna mipango ya kujenga laini kubwa ya umeme kwenda mgodi wa dhahabu wa GGM ili kuboresha uzalishaji na kuvutia uwekezaji.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba alisema ni vijiji vitatu pekee kati ya vijiji 486 vya mkoa huo ambavyo bado havijapatiwa umeme, huku Serikali ikiendelea na mpango wa kuvifikia kwa njia mbadala.