Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM Mbeya kuomba kura nyumba kwa nyumba, kusikiliza kero

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Ndele Mwanselela (kushoto) akipungiana mkono na makundi mbalimbali wakiwamo Bodaboda, Bajaji, Mama Lishe na Machinga katika mkutano wake wa kuomba kura kwa wagombea wa chama hicho mkoani humo.

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi mkoani Mbeya imesema itafanya kampeni za nyumba kwa nyumba kusaka kura na kusikiliza kero za wananchi ili itakaposhinda iweze kufanyia kazi changamoto zote.

Mbeya. Chama cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Mbeya kimeanza kampeni ya nyumba kwa nyumba na kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii kuomba kura na kusikiliza kero zao, huku kikiahidi kukutanisha wagombea na wananchi.

Kampeni hiyo ya nyumba kwa nyumba imeanza leo Septemba 16,2025 kwa wilaya ya Mbeya mjini, ambapo inatarajia kufanyika maeneo yote yenye wagombea ngazi za kata na majimbo.
Akizungumza katika mkutano wake na waendesha bajaji, bodaboda, mamalishe na machinga, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho Taifa (MNEC), Ndele Mwanselela amesema lengo ni kusikiliza kero zao ili kujua pa kuanzia iwapo watashika dola.

Amesema katika ziara hiyo ya kukutana na makundi mbalimbali, CCM Mkoa wa Mbeya itawakutanisha na wagombea wote ambao ndio watakuwa watekelezaji iwapo watachaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

"Zipo njia 10 tutakazotumia kusaka kura, lakini natangaza mbili za kukutana na makundi mbalimbali na kutembea nyumba kwa nyumba, leo nimeanza Mbeya mjini na nitahitimishia Chunya.”

"Nilichofurahishwa ni mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza na kutusikiliza lakini kuwasilisha kero zao, nia ya CCM ni kuwatumikia makundi yote na mgombea urais Samia Suluhu Hassan ameshaahidi mambo makubwa kwa siku 100 za kwanza," amesema Mwanselela.

MNEC huyo ambaye pia mwenyekiti wa chama hicho mkoa huo kwa sasa, ameongeza kuwa ameamua kujipa jukumu hilo kuhakikisha CCM inaendelea kubaki madarakani akieleza kuwa lazima washinde kutokana na maendeleo yaliyofanyika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha waendesha bajaji mkoani humo, Lucas Mwakyusa amesema watatoa ushirikiano kwa wagombea wanaotanguliza uzalendo, kwani hitaji lao ni kufanya kazi kwenye amani.
"Hatutakuwa tayari wanaopinga amani ya nchi kwa kuwa bila hivyo, hakuna maendeleo, tunaipongeza Serikali na tutaendelea kushirikiana nayo na kuwachagua wenye uzalendo,”amesema Mwakyusa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa waendesha bodaboda, Aman William amesema wakati huu wa uchaguzi wataendelea kuhamasisha watu kufanya kazi na kujitokeza kupiga kura.

Amesema shughuli ya bodaboda ni kazi kama nyingine hivyo kila mmoja lazima aithamini na kuipenda kwani inaendesha maisha ya wengi, kuiingizia Taifa pato na kuchochea uchumi wa mtu mmojammoja.

Felista Juma ambaye ni mama lishe amesema wanaomba kufanya kazi katika mazingira rafiki akieleza kuwa wanaridhishwa na uongozi wa awamu ya sita.