Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Mapunda ataka mabanda ya Sabasaba yakamilike kabla ya Juni 28

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, akikagua mabanda ya maandalizi ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), kuhakikisha yanakamilika kwa wakati kuelekea ufunguzi rasmi wa maonesho hayo.

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amewataka wadau wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kukamilisha mabanda yao kabla ya Juni 28 ili kuhakikisha maadhimisho ya miaka 50 ya maonesho hayo yanaonekana kwa hadhi ya juu.

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amewataka wadau wenye mabanda katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kukamilisha maandalizi yao kabla ya Juni 28 mwaka huu ili kuhakikisha wageni wanakutana na mandhari yenye hadhi ya maadhimisho ya miaka 50 ya maonesho hayo.

Akizungumza leo Juni 12, 2026, baada ya kukagua maendeleo ya maandalizi ya maonesho hayo, Mapunda amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa, lakini amesisitiza kasi iongezwe kwa wale ambao bado hawajakamilisha mabanda yao.

“Tunataka kabla ya Juni 28, 2026, mabanda yote yawe yamekamilika na kupambwa vizuri ili wageni wetu waone wazi kwamba haya ni maonesho maalumu ya kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake,” amesema.

Amesema maonesho ya mwaka huu yataambatana na vivutio mbalimbali ikiwemo fursa za utalii, bidhaa za ndani na nje ya nchi pamoja na bidhaa adimu, hivyo akawahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Trade Development Authority (TanTrade), Dk Latifa Khamis, amesema maandalizi ya maonesho ya mwaka huu yamefikia hatua kubwa na yanatarajiwa kuwa ya kipekee kutokana na maadhimisho ya Golden Jubilee.

Amesema hadi sasa nchi 23 zimethibitisha ushiriki, huku makampuni 256 ya nje na zaidi ya 2,700 ya ndani yakijihakikishia kushiriki, hatua inayoonesha mwitikio mkubwa uliosababisha baadhi ya maeneo ya maonesho kujaa mapema.

“Tunasherehekea miaka 50 ya maonesho haya. Tumejipanga kuhakikisha yanakuwa makubwa zaidi na yenye kuvutia wageni wa ndani na nje,” amesema.

Dk. Latifa amesema maonesho hayo yatakuwa na programu mbalimbali zikiwemo usiku wa fasheni, matembezi ya maadhimisho ya miaka 50 na usiku maalumu wa Golden Jubilee utakaofanyika Julai 6, ambapo wadau mbalimbali watatambuliwa kwa mchango wao.

Amesema pia kampeni ya Made in Tanzania imepewa kipaumbele ili kuendeleza bidhaa za ndani katika masoko ya kimataifa, akibainisha kuwa jitihada za serikali zimeanza kuleta matokeo chanya katika soko la dunia.

Mapunda amesema maonesho hayo yanatarajiwa kuwa zaidi ya jukwaa la biashara, yakihusisha pia burudani, uwekezaji, ubunifu na ujenzi wa mitandao ya kibiashara kwa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi.