Gombo, Hamad Masoud kupeperusha bendera ya urais CUF
Muktasari:
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), wampendekeza Samandito Gombo kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Dar es Salaam.Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), wampendekeza Samandito Gombo kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Gombo, ambaye amewahi kuwa mtumishi wa umma akishika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Mkurugenzi wa Wilaya ya Mbinga, amependezwa kwa kupigiwa kura 467 kati ya 545 zilizopigwa, akimshinda mshindani wake Siwale Mkungutila aliyepata kura 78.
Katika uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Lekham, Buguruni Jijini Dar es Salaam, upande wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad amependekezwa kuwa mgombea ursi baada ya kujikusanyia kura 406 kati ya zilizopigwa.
Hamad amewabwaga washindani wenzake wawili Mohamed Habib Mnyaa (128) na Dk Mohamed Khatibu Mikidadi (8).
Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa uchaguzi, Mashaka Ngole amesema kuwa uteuzi wa viongozi hao unaonyesha umoja na ushirikiano wa chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Hivi sasa, Samandito Gombo na Hamad Masoud wanacho subiri ni baraka za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ili waweze kuingia rasmi katika kinyang'anyiro hicho dhidi ya wagombea kutoka vyama vingine 17 vinavyoshiriki uchaguzi huo.
Akizungumza kuhusu uteuzi wa wagombea hao, Katibu Mkuu wa CUF, Husna Abdallah amesema chama hicho kipo tayari kuendelea na mchakato wa uchaguzi na kutoa matumaini kwa wananchi kuwa sera za CUF zitaendelea kuleta mabadiliko chanya katika Taifa hili.