Grumeti yatumia Sh370 milioni kuboresha shule, afya na maji Mara
Kamishna Msaidizi Mwandamizi kutoka Tawa, Omari Msangi (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco moja ya kompyuta iliyotolewa na Shirika la Grumeti Reserves kwaajili ya jamii zinazunguka Mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti wilayani Bunda na Serengeti. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Msaada huo unajumuisha madawati 3,014 kwa shule za msingi, vitanda 16 ikiwemo sita vya kujifungulia, kompyuta 19 na uwekaji wa maji kwa shule moja ya msingi.
Serengeti. Kampuni ya Grumeti Reserves Limited imetumia takriban Sh370 milioni kununua vifaa vya elimu, afya na maji kwa jamii zinazozunguka mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti katika wilaya za Serengeti na Bunda, mkoani Mara.
Msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba uliosaini kati ya Grumeti Reserves na Mamlaka ya Uhifadhi Wanyamapori Tanzania (Tawa) baada ya kampuni hiyo kupewa kitalu cha kuhifadhi na kuendeleza maendeleo ya jamii.
Akizungumza Februari 27, 2026, wakati wa kukabidhi msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Grumeti Reserves, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Grumeti Fund, Frida Mollel, amesema msaada huo ni matokeo ya uhifadhi bora. Aliahimiza wananchi kuendeleza jitihada za uhifadhi na kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu mazingira ya hifadhi.
Msaada huo unajumuisha madawati 3,014 kwa shule za msingi, vitanda 16 ikiwemo sita vya kujifungulia, kompyuta 19 na uwekaji wa maji kwa shule moja ya msingi.
“Tumezitoa madawati 1,534 kwa wilaya ya Bunda na 1,480 kwa Serengeti, vitanda 12 kwa Bunda na vinne kwa Serengeti pamoja na vifaa vya tehama kwa wilaya zote,” amesema.
Ameongeza kuwa, kupitia msaada huo, jamii inatakiwa kuelewa umuhimu wa uhifadhi na kushiriki kikamilifu katika jitihada za kuhifadhi. Aidha, Grumeti imepanga kushiriki katika maendeleo ya kijamii katika maeneo yote ya hifadhi kwa kipindi cha miaka 20 ya mkataba.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Tawa, Omari Msangi, amewahi kuziomba mamlaka husika kuhakikisha vifaa vilivyotolewa vinatumika ipasavyo ili kuleta tija kwa jamii. Pia alisema mamlaka yake itaendelea kuimarisha ulinzi wa hifadhi na kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.
“Sekta ya wanyamapori bado inakabiliwa na ujangili na uvamizi wa ardhi ndani ya hifadhi. Tunapaswa kuhakikisha tunalinda uhifadhi endelevu kwa kuacha vitendo vinavyohatarisha usalama wake,” amesema Msangi.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Kaminyoge, amesema msaada huo utawanufaisha zaidi ya watoto 4,600, huku akibainisha kuwa vitanda vya kisasa vya kujifungulia na vifaa vya ICT pia vinaongeza huduma za kijamii.
Ameongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuacha kilimo, ufugaji na ukataji wa miti ndani ya hifadhi ili kuendeleza uhifadhi endelevu. “Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marko, amesema matokeo ya uhifadhi yana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhifadhi rasilimali hizo.
“Tuna jukumu kubwa la kusaidia Rais kuboresha maisha ya wananchi, na hili linafanyika kupitia huduma za kijamii katika sekta za maji, afya na elimu, kama inavyofanywa na Grumeti leo,” amesema Marko.