Kihongosi awataka vijana kulinda Amani, kujiepusha kutumika kisiasa
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akizungumza baada ya kuzuru kaburi la baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere wilayani Butiama.
Muktasari:
- Kihongosi amesema vijana wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha taifa lao linakuwa salama muda wote kwa maelezo kuwa usalama wa taifa unawategemea vijana ambao watatanguliza mbele uzalendo kwa nchi yao badala ya maslahi yao binafsi
Tarime. Vijana nchini wametakiwa kushirikiana kwa pamoja kulinda taifa dhidi ya viashiria vyote vinavyoweza kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa nchi.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa, Mei 15, 2026 mjini Tarime na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, alipohutubia mkutano wa hadhara katika ziara yake ya siku nne mkoani Mara yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Kihongosi amesema vijana wana jukumu kubwa la kuhakikisha taifa linabaki salama muda wote, akisisitiza kuwa usalama wa nchi unategemea zaidi uzalendo wa vijana badala ya kuendeshwa na maslahi binafsi.
Amesema baadhi ya watu wenye tamaa ya madaraka wako tayari kufanya lolote bila kujali madhara yake, hivyo amewataka vijana kuwa makini na kuepuka kutumika katika mikakati inayoweza kuhatarisha amani ya nchi.
“Vijana taifa linawahitaji sana, msikubali kutumika kwa maslahi ya baadhi ya watu ambao wako tayari kufanya lolote ili mradi wapate madaraka bila kujali usalama na amani ya nchi yetu,” amesema.
Akizungumzia maendeleo ya Wilaya ya Tarime, Kihongosi amesema Serikali ya CCM imeweka mipango mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha miundombinu ya maji, barabara na kukamilisha miradi mbalimbali ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Amesema Tarime katika miaka mitano ijayo itashuhudia mabadiliko makubwa yatakayochochea ukuaji wa uchumi wa familia na jamii kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa Tarime na Rorya wameiomba Serikali kushughulikia changamoto ya uhaba wa nyumba za watumishi, hususan katika sekta za elimu na afya vijijini.
Wamesema ukosefu wa makazi bora kwa watumishi umekuwa ukipunguza ari ya utendaji kazi, wakipendekeza ujenzi wa nyumba hizo uendane na miradi ya shule na vituo vya afya.
Akijibu hoja hiyo, Kihongosi amesema atalifikisha suala hilo katika mamlaka husika, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki ujenzi wa maboma ambayo yanaweza kukamilishwa na halmashauri kupitia mapato ya ndani.
Aidha, ameahidi kufuatilia tuhuma za upungufu wa dawa katika vituo vya afya, licha ya kuelezwa kuwa upatikanaji wa dawa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime umefikia asilimia 96.8.