Maambukizi ya Ukimwi yaongezeka Pakistan
Wataalam wa afya nchini Pakistan wameishauri serikali kuchukua hatua kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi, wakidai kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, wataalam hao wakiwemo madaktari wamenukuu Shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi (UNAIDS) lililoionya Pakistan mara kwa mara kuhusu kuongezeka kwa maambukizi na kuitaka kuboresha sera yake ya afya.
‘’Kwa zaidi ya miongo miwili nchi yetu imekuwa na ongezeko la maambukizi..., mbali na mambo mengine, hivi karibuni ilibainika uwepo wa madaktari feki zaidi ya 300 ambao unaweza kusema nao wanahusika katika kuongezeka kwa maambukizi,’’
‘’Tulifuatilia na kubaini uchomaji wa shindano usiozingatia taratibu, sindano inatumika kwa mtu zaidi ya mmoja, hii ni hatari,’’ ilieleza sehemu ya taarifa yao iliyosainiwa na Dk Shariff Shah.
Shah alidai Pakistan kwa sasa inashika nafasi ya pili kwa maambukizi ya Ukimwi katika nchi za barani Asia huku maambukizi zaidi yakitajwa kuwepo katika mji wa Karachi.
‘’Pamoja na mambo mengine, ukuaji wa takwimu hizi unatokana na taarifa za uwepo wa madaktari feki, uchomaji wa sindano usiozingatia taratibu na watu kuongezewa damu kienyeji,’’ alisema Shah.
Taarifa hiyo wa wataalam wa afya Pakistan inabainisha kuwa mwaka huu watoto 3,995 wamaripotiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, idadi waliyoeleza kuwa inaakisi ukubwa wa maambukizi.
‘’Utupaji wa taka pia unatakiwa kuzingatiwa, sindano zinazotupwa hutumika tena mitaani hivyo kuongeza wasiwasi zaidi wa maambukizi,’’ inaeleza sehemu ya taarifa hiyo na kubainisha mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu uhifadhi salama wa taka.