Mauly tours wapanda miti zaidi ya 200 kurejesha uoto wa asili Kilimanjaro
Moshi. Wadau wa utalii mkoani Kilimanjaro wamesema wataendelea kushirikiana na serikali katika juhudi za upandaji miti kwenye maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, lengo ikiwa ni kukabiliana na athari za kimazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Wamesema kuwa moja ya maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi ni Mlima Kilimanjaro, ambapo barafu yake imekuwa ikipungua mara kwa mara na kwamba upandaji miti huo utasaidia kuhifadhi mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa shughuli ya upandaji miti katika shule ya Sekondari Uru Community, iliyopo Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro, mdau wa utalii kutoka shirika la Mauly tours, Sharifa Mauly amesema endapo kila mwanajamii atabeba jukumu la kupanda miti katika eneo linalomzunguka itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za kimazingira.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Uru Community wakipanda miti katika eneo hilo la shule
Amesema miti zaidi ya 200 iliyopandwa shuleni hapo leo itakuwa na manufaa makubwa katika suala zima la utunzaji wa mazingira katika mkoa huo na kwamba utasaidia kurejesha uoto wa asili ambao uliopotea kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
"Tujitahidi sana kuotesha miti kwenye maeneo yetu hususani kwenye maeneo haya yanayozunguka hifadhi ya mlima Kilimanjaro. Mwaka jana ukame ulikuwa ni mkubwa sana na ulituathiri sana hususani katika mlima wetu Kilimanjaro ambao barabara yake imekuwa ikipungua kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi,"amesema
Amesema "Tunamshukuru Rais wetu kwa kutupa hamasa ya kuweza kupanda miti, tutaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha tunarejesha uoto wa asili uliopotea katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro.
Naye, Mkuu wa shule ya Sekondari Uru Community, Gift Simle amesema wadau pamoja na serikali wakishirikiana na kuweka nguvu ya pamoja watafanikiwa kwa kiasi kikubwa kukabiliana na athari za kimazingira zinazotokana na ukame.
"Upandaji miti hapa shuleni ni katika kuweka jitihada za kutunza na kuhifadhi mazingira yetu, suala la mabadiliko ya tabianchi ni suala ambalo athari zake tunazishuhudia lakini na jitihada ambazo zinafanywa na serikali, wadau kuhakikisha kwamba tunakabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari, Uru Community wakipanda miti katika eneo hilo la shule
Amesema, ukataji wa miti ovyo ni ushahidi kwamba hatua zisipochukuliwa barafu katika mlima Kilimanjaro itaendelea kupungua siku hadi siku na kwamba athari yake itakuwa ni kubwa
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Erick Lucas, amesema upandaji wa miti wa sasa utasaidia kurejesha uoto wa asili katika mkoa huo ambao ulipotea kutokana na changamoto ya ukame.
"Tunaamini sisi wanafunzi pamoja na jamii nzima tukiweka juhudi za pamoja za kuotesha miti katika maeneo yetu, itatusaidia kutunza mazingira yetu na kurejesha ukijani katika hifadhi zetu za mlima Kilimanjaro,"amesema mwanafunzi huyo