Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miche 534,000 ya kahawa yagawiwa kwa wakulima Vunjo, kuinua uchumi

Baadhi ya wananchi wakikabidhiwa miche ya kahawa na mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Moshi. Serikali imetoa miche ya kisasa 534,000 ya kahawa  bure  ya kahawa kwa wakulima Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuendeleza zao hilo na kuimarisha uchumi wa wakulima wa kahawa, Mkoani humo.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa kahawa na kurejesha hadhi ya zao hilo ambalo kwa miaka ya nyuma lilikuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa wakazi wa mkoa huo.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa miche hiyo ya kahawa, uliofanyika kata ya Mwika Kusini , Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo amesema mpango huo ni utekelezaji wa azma ya serikali ya kuwawezesha wakulima kupitia ruzuku ya pembejeo ikiwemo miche bora.

Aidha, Kimaryo amesema zao la kahawa lina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Miche hii tunayogawa leo si mimea tu, ni ahadi ya maisha bora kwa mkulima. Leo hii kilo moja ya kahawa imefikia wastani wa Sh12,000, hivyo uzalishaji ukiongezeka, kipato cha mkulima kitaimarika,” amesema Kimaryo. 

Baadhi ya wananchi wakikabidhiwa miche ya kahawa na mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Amesema  kuwa,  kwa mujibu wa wataalamu wa kilimo, mkulima anatakiwa kuwa na angalau miti 540 ya kahawa ili kupata tija inayoweza kumsaidia kumudu gharama za maisha ikiwemo kusomesha watoto pamoja na maendeleo mengine.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Koola amesema wameanza mkakati wa makusudi wa kufungua upya kilimo cha kahawa kwa kuwa ni zao la kimkakati.

“Kahawa ni dhahabu ya kijani. Tumedhamiria kuhakikisha inakuwa uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi wetu. Tunawaomba vijana wajitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hii,” alisema Koola.

Aliongeza kuwa kuelekea Dira ya Maendeleo 2050, zao la kahawa linatarajiwa kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati yatakayochangia ukuaji wa uchumi.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amepiga marufuku ukataji wa miti ya kahawa na kuwataka wakulima kupokea miche hiyo ya kisasa na kuitunza ili kuongeza uzalishaji.

Aliwataka pia wataalamu wa kilimo kushuka mashambani badala ya kubaki ofisini ili kuwasaidia wakulima kuongeza ujuzi.

“Wakulima wengi wanakata tamaa kutokana na ukosefu wa utaalamu, hivyo ni muhimu wataalamu wakawafikia moja kwa moja,” alisema Babu.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Godfrey Mnzava amesema ugawaji wa miche hiyo ni sehemu ya jitihada za viongozi wa mkoa kuhakikisha zao hilo linafufuliwa na kurejesha hadhi yake.

Alisema kahawa ni zao la kihistoria kwa wananchi wa Kilimanjaro na lina uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya kiuchumi endapo litapewa kipaumbele.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwika Kusini, John Tarimo amesema kushuka kwa uzalishaji wa kahawa kulisababisha kudorora kwa uchumi wa wananchi wengi wa eneo hilo.

Amesema hapo awali zao hilo lilikuwa uti wa mgongo wa maisha ya wananchi kwa kuwawezesha kugharamia elimu na shughuli nyingine za maendeleo.

“Naamini hatua hii itarejesha matumaini ya wakulima na kuchochea kurejea kwa kilimo cha kahawa kwa tija zaidi,” amesema Tarimo.