Serikali yaja na mpango wa kuimarisha uwazi katika miradi ya PPP
Mkurugenzi Mtendaji wa PPP Centre, David Kafulila akizungumza wakati wa kongamano la wadau wa sekta binafsi l wa kujengea uwezo kuhusu miradi ya PPP.
Muktasari:
- Mkurugenzi Mtendaji wa PPP Centre, David Kafulila amesema mfumo huo unaopendekezwa utasaidia kuratibu shughuli za ushawishi wa uwekezaji na kurahisisha mchakato wa uwekezaji, hali itakayowezesha wawekezaji kushiriki kwa urahisi zaidi katika miradi ya kimkakati ya maendeleo.
Dar es Salaam. Serikali ina mpango wa kuanzisha mfumo rasmi wa kuwasajili winga kama sehemu ya jitihada za kulinda wawekezaji, kuongeza uwazi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Hatua hiyo, inayosimamiwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), inatarajiwa pia kusaidia kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali pamoja na kuongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na wa nje.
Mkurugenzi Mtendaji wa PPP Centre, David Kafulila amesema mfumo huo unaopendekezwa utasaidia kuratibu shughuli za ushawishi wa uwekezaji na kurahisisha mchakato wa uwekezaji, hali itakayowezesha wawekezaji kushiriki kwa urahisi zaidi katika miradi ya kimkakati ya maendeleo.
Ametoa kauli hiyo akijibu hoja zilizotolewa na wadau wa sekta binafsi kuhusu changamoto za urasimu katika taasisi zinazosimamia miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP). Alizungumza hayo wakati wa kongamano la kujengeana uwezo kuhusu miradi ya PPP lililokuwa na kaulimbiu Kuelewa Miradi na Mfumo wa PPP nchini Tanzania, lililoandaliwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Mkutano huo pia ulipitia utekelezaji wa Sheria ya PPP Na. 4 ya mwaka 2023 na kutathmini maendeleo ya miradi mbalimbali iliyo katika hatua za maandalizi.
“Mawinga wa uwekezaji wana mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi. Hata katika nchi zilizoendelea kama Uingereza, kuna mifumo rasmi inayosimamia shughuli hizi. Ndiyo maana tunapanga kuanzisha mfumo rasmi wa kuwasajili washawishi wa uwekezaji nchini Tanzania,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa kuna washawishi wengi wanaofanya kazi bila utaratibu rasmi, maarufu kama winga, hasa katika eneo la Kariakoo na sekta mbalimbali, hali inayowaweka wawekezaji katika hatari ya utapeli na kuikosesha serikali mapato yanayoweza kupatikana.
Kafulila pia amebainisha kuwa PPP Centre iko katika hatua za mwisho kukamilisha hati ya makubaliano na TPSF yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje pamoja na kupunguza ucheleweshaji wa taratibu za uwekezaji.
“Hivi karibuni tutasaini makubaliano na TPSF. Ushirikiano huu utasaidia kupunguza urasimu. Sisemi kwamba kuna mapungufu makubwa, lakini bado kuna baadhi ya vibali ambavyo wakati mwingine huchelewesha maamuzi ya uwekezaji,” amesema.
Amefafanua kuwa maboresho yanayoendelea yanaelekezwa katika kuondoa vikwazo vya kisheria na kiudhibiti, ikiwemo kufanya marekebisho yatakayorahisisha taratibu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya PPP.
“Pia tunaendelea kuongeza uelewa kuhusu taratibu za PPP na kuhamasisha maandalizi bora ya miradi kutoka sekta ya umma na sekta binafsi,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara Zanzibar, Hamadi Hamadi amesema maandalizi duni ya miradi inayoweza kuvutia uwekezaji bado ni changamoto inayochelewesha utekelezaji wa miradi katika sekta muhimu kama afya na usafiri wa mijini.
“Tunakumbana na changamoto nyingi kwa sababu baadhi ya maeneo ya kipaumbele ya uwekezaji hayaandaliwi ipasavyo mapema. Amesisitiza umuhimu wa kufanya tafiti yakinifu kabla ya kuwahusisha wawekezaji,” amesema.
Ameongeza kuwa wakati wa ziara ya mwaka 2023 nchini Oman iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, baadhi ya wawekezaji walionesha nia ya kuwekeza katika miradi ya reli nyepesi ya juu (monorail) na mabasi ya mwendokasi ya juu jijini Dar es Salaam, lakini miradi hiyo ilikwama kutokana na ucheleweshaji wa taratibu za kiutawala.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Hamis Luvembe amesema bado kuna wawekezaji wengi walio tayari kuwekeza katika sekta mbalimbali, lakini hukatishwa tamaa na ucheleweshaji wa taratibu za taasisi.
“Kuna wawekezaji wengi walio tayari kuwekeza katika sekta tofauti, lakini taratibu za taasisi mara nyingi huleta changamoto zisizo za lazima. Baadhi ya michakato huchukua muda mrefu na kuwakatisha tamaa wawekezaji makini,” amesema.
Ametoa wito wa kuimarishwa kwa uratibu kati ya taasisi za serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati.
Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Meli Tanzania (Tasaa), Abel Uronu, ameitaka serikali kuweka vivutio maalumu katika sekta za kimkakati kama usafiri wa baharini na utalii ili kuongeza ushiriki wa wawekezaji wazawa.
Amesema kuwepo kwa mazingira rafiki ya uwekezaji, ikiwemo kupunguza gharama na kushirikiana katika hatari za uwekezaji, kutachochea mtiririko wa mitaji na kuharakisha mageuzi ya uchumi wa nchi.