Stanbic yazidi kusogeza elimu ya bima mitaani
Ofisa wa Bancassurance wa Stanbic Bank Tanzania, Naphtal Ntangeki (kushoto), akimueleza Benedict, dereva wa bodaboda, jinsi bima inavyoweza kumlinda na kulinda kipato chake cha kila siku, wakati wa kliniki ya uhamasishaji wa bima iliyofanyika katika Stendi ya Kabwe jijini Mbeya hivi karibuni.
Muktasari:
- Kupitia kampeni hiyo ya Stanbic Bank Tanzania kwa kushirikiana na kampuni za bima, wananchi wakiwemo madereva wa bajaji na wafanyabiashara wadogo wameelezwa umuhimu wa bima katika kulinda maisha na mali.
Mbeya. Wakaazi wa jiji la Mbeya wamepata fursa ya kujifunza kwa undani kuhusu umuhimu wa bima katika maisha yao ya kila siku kupitia kampeni ya uhamasishaji iliyofanyika katika Stendi ya Kabwe, ambapo wengi wao wameibuka na uelewa mpya kuhusu namna bima inavyoweza kulinda maisha na mali zao.
Kampeni hiyo ya kitaifa ya elimu ya bima, iliyoendeshwa na Benki ya Stanbic Bank Tanzania kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali za bima, imelenga kuwafikia wananchi wa kawaida ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima katika kulinda maisha, mali na shughuli za kiuchumi.
Katika zoezi hilo, wananchi, wafanyabiashara na madereva wa vyombo vya usafiri walipata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu namna bima inavyofanya kazi na faida zake katika maisha ya kila siku.
Akizungumza wakati wa kampeni hiyo, Ofisa Benki Bima wa Stanbic, Naphtal Ntangeki, alisema lengo ni kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wananchi moja kwa moja bila vikwazo vya umbali au gharama.
Alisema bima ni nyenzo muhimu ya ulinzi wa kifedha, lakini kwa muda mrefu imekuwa haieleweki ipasavyo kwa wananchi wengi, hususan walio katika sekta isiyo rasmi.
“Tunataka kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wananchi mahali walipo. Ulinzi wa kifedha unapaswa kuwa rahisi kueleweka na kupatikana kwa kila mtu,” alisema.
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa kampeni hiyo, Benezeti, dereva wa bajaji, alisema elimu hiyo imemsaidia kubadilisha mtazamo wake kuhusu bima, akisema awali alikuwa haioni kama ni muhimu kwa watu wa kipato chake.
“Kabla ya leo nilidhani bima ni ngumu na haimhusu mtu kama mimi. Sasa nimeelewa kuwa ni muhimu sana, hasa kwa sisi tunaotegemea kazi zetu za kila siku kuendesha maisha,” alisema.
Wananchi wengine walioshiriki walieleza kufurahishwa na namna elimu hiyo ilivyotolewa kwa lugha rahisi na ya moja kwa moja, wakisema imewasaidia kuelewa nafasi ya bima katika kupunguza athari za majanga ya ghafla.
Kampeni hiyo ya Mbeya ni sehemu ya mwendelezo wa shughuli kama hizo zilizofanyika katika mikoa ya Tanga na Mwanza, ikiwa ni mkakati wa kitaifa wa kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika huduma za bima nchini.