Tazara kuadhimisha nusu karne, ikijipanga kwa mageuzi mapya
Muktasari:
- Tazara, iliyoanzishwa kutokana na maono ya pamoja ya viongozi waanzilishi wa Tanzania, Zambia na China, itaadhimisha hatua hiyo muhimu kwa kutafakari historia yake ya mafanikio huku ikielekea katika enzi mpya ya uhuishaji, mageuzi na uboreshaji wa utoaji huduma.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), imeandaa maadhimisho ya mwezi mzima kuadhimisha miaka 50 tangu kuanza rasmi shughuli zake za kibiashara, sambamba na uzinduzi wa ajenda ya mageuzi itakayoiongoza taasisi hiyo katika kipindi cha miaka 50 ijayo.
Tazara, iliyoanzishwa kutokana na maono ya pamoja ya viongozi waanzilishi wa Tanzania, Zambia na China, itaadhimisha hatua hiyo muhimu kwa kutafakari historia yake ya mafanikio huku ikielekea katika enzi mpya ya uhuishaji, mageuzi na uboreshaji wa utoaji huduma.
Uzinduzi rasmi wa maadhimisho hayo utafanyika Julai 14, 2026, ukiambatana na matukio mbalimbali yatakayofanyika katika kipindi chote cha maadhimisho. Matukio hayo ni pamoja na wiki ya ushirikiano na umma, mashindano ya gofu yatakayofanyika Dar es Salaam na Lusaka, pamoja na mihadhara ya kitaaluma itakayojadili historia, mchango na mustakabali wa Tazara
Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, Bruno Ching’andu, ametoa wito kwa wafanyakazi, wateja, washirika wa taasisi hiyo, waliowahi kuwa wafanyakazi wake na wananchi wanaoishi kandokando ya reli kushiriki kikamilifu katika kuadhimisha tukio hilo la kihistoria.
“Tunapoadhimisha miaka 50 ya Tazara, hatuadhimishi urithi wa ukombozi, kujitoa na mshikamano wa kikanda pekee, bali pia tunafungua ukurasa mpya wa mageuzi kupitia uhuishaji. Huu ni wakati wa kutafakari, kusherehekea na kuungana katika kuunga mkono kuzaliwa upya kwa Tazara kama njia ya fursa,” amesema Ching’andu.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano wa Umma, Ching’andu amesema tangu kukamilika kwake mwaka 1976, Tazara imekuwa na mchango mkubwa katika kuwaunganisha watu, kuwezesha biashara, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kutoa kiunganishi muhimu kati ya Bandari ya Dar es Salaam na nchi za bara la Kusini mwa Afrika.
Amesema reli hiyo, inayojulikana pia kama “Reli ya Uhuru”, ni miongoni mwa miradi mashuhuri barani Afrika iliyojengwa katika mazingira yenye changamoto kubwa kwa lengo la kuondoa vikwazo vya biashara vilivyotokana na ukoloni na kuimarisha uhuru wa kiuchumi wa mataifa ya ukanda huo.
Maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu yatafanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Tazara@50: Kutoka Ukombozi hadi Mageuzi,”.
Tazara ni reli ya pamoja inayomilikiwa na Serikali za Tanzania na Zambia. Reli hiyo ilijengwa kati ya mwaka 1970 na 1976 kwa msaada wa Serikali ya China na kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kapiri Mposhi nchini Zambia, huku ikifungua fursa za biashara na kuimarisha uunganishaji wa masoko ya COMESA na SADC.
Julai 16, 2026, Tazara itatimiza rasmi miaka 50 tangu kuanza shughuli zake za kibiashara. Kwa sasa, mamlaka hiyo ipo katika hatua za mageuzi makubwa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), kufuatia kutiwa saini kwa Mkataba wa Uendeshaji kati ya Tazara na Shirika la China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) Septemba 29, 2025.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa reli, kuboresha huduma za usafirishaji na kuimarisha nafasi ya Tazara kama mhimili muhimu wa biashara na maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.