Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukatili wa kijinsia watajwa chanzo baadhi ya wanawake kuishia gerezani

New Content Item (4)
New Content Item (4)

Muktasari:

  • Vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii, hususan dhidi ya wanawake, vinatajwa kuwafanya baadhi yao kujikuta mikononi mwa sheria wanapochukua hatua za kujitetea.

Moshi. Imeelezwa kuwa baadhi ya wanawake wanaojikuta wakihukumiwa vifungo mbalimbali gerezani, chanzo chake ni vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa katika jamii, hali inayowafanya baadhi yao kujitetea au kuchukua hatua ambazo baadaye huwafanya kujikuta wakikabiliwa na mkono wa sheria.

Hayo yamesemwa leo Machi 11, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Ex-Prisoners Foundation, Rose Male, wakati alipokabidhi zawadi mbalimbali kwa wanawake wafungwa katika Gereza la Karanga lililopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Male amesema wameamua kukabidhi zawadi hizo kwa wanawake hao wafungwa kwa njia ya kipekee ikiwa ni pamoja na kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na namna unavyoweza kuwapelekea baadhi ya wanawake kuingia magerezani.

Amesema ni muhimu jamii kushirikiana kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kulinda haki na usalama wa wanawake, pamoja na kuzuia matukio yanayoweza kusababisha migogoro inayofikia hatua ya kuvunja sheria.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za ukatili huo na kuwahimiza wanawake wanaokumbana na changamoto hizo kutafuta msaada kupitia vyombo na taasisi husika badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuwaingiza kwenye matatizo ya kisheria

“Tumeona tusherekee siku ya mwanamke duniani kwa namna tofauti kwa kufikisha ujumbe kwa jamii kwamba ukatili wa kijinsia unaweza kuwapelekea wanawake kwenda gerezani na wengine kufungwa kifungo cha kunyongwa hadi kufa,” amesema Rose

Aidha, amesema kumekuwepo na matukio mengi katika jamii ambayo yamepelekea wanawake kujikuta magerezani huku chanzo kikubwa kikiwa ni ukatili waliokuwa wanafanyiwa.

New Content Item (4)
New Content Item (4)

“Kwa mfano, kuna kesi ambapo mwanamke alikuwa akipigwa sana na kunyanyaswa.Siku alipojitetetea mwanaume akafariki na mwanamke huyo akajikuta anakabiliwa na kesi ya mauaji na hatimaye kufungwa kifungo cha kunyongwa hadi kufa,” amesema Rose.

Rose ameongeza kuwa, madhara ya ukatili wa kijinsia ni makubwa kwa kuwa huathiri pia afya ya akili na kusababisha migogoro ya kifamilia pamoja na watu kushindwa kutimiza majukumu yao.

“Tunashuhudia watu wanakimbia majukumu ya kulea familia, wengine wanaachana na wenza wao na migogoro ya mahusiano inaongezeka, haya yote yanaathiri ustawi wa jamii,” amesema Rose

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava ameipongeza Taasisi hiyo, kwa juhudi zake za kuelimisha jamii kuhusu madhara ya uhalifu na kuwasaidia waliotoka magerezani kurejea katika maisha ya kawaida bila kurudia makosa.

“Tunawapongeza Tanzania Ex-Prisoners kwa kuwa kinara katika kuielimisha jamii kuepukana na vitendo vinavyoweza kupelekea watu kuingia magerezani na pia kuwasaidia waliotoka gerezani wasirudi tena kwenye uhalifu,” amesema Mnzava.

Aidha, amesema licha ya kuwepo kwa wachache wanaorudia uhalifu na kurejea magerezani, bado jitihada za taasisi hiyo zinasaidia kuwabadilisha wengi na kuwafanya kuwa raia wema.

“Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wakati wote na pale ambapo panahitajika kuchukua hatua za kisheria tutaendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria kwa kushirikiana na vyombo vinavyosimamia haki na sheria,” amesema DC Mnzava

Naye, Mkuu wa dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Kilimanjaro, Asia Matauka amesema matukio ya ukatili bado ni changamoto kubwa katika jamii hususani katika mkoa huo.

Amesema wakati mwingine wazazi wamejikita zaidi katika kutafuta kipato na kusahau wajibu wa malezi ya watoto na jamii yao kwa ujumla.

“Akina mama wengi wako 'busy'sana katika kutafuta fedha  na wamesahau suala la malezi au wameyaacha kwa dada wa kazi,  lakini ni muhimu kujiuliza unamtafutia nani kama humthamini na kumpa muda wa kutosha mtoto wako, ” amesema Matauka

Matauka amesema baadhi ya watu wanaojikuta magerezani walipitia maumivu ya ukatili katika familia zao hali iliyowasukuma kufanya vitendo vya ukatili na hatimaye kujikuta wanakabiliwa na sheria.

Amesema katika Mkoa wa Kilimanjaro matukio mengi ya ukatili yanatokea ndani ya familia, huku baadhi yakihusisha wazazi kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto wao.