Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi wa dini waombwa kuhimiza tahadhari dhidi ya mvua Mara

Baadhi ya wadau walioshiriki kwenye futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi mjini Musoma.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewataka viongozi wa dini kutumia nyumba zao za ibada kuwakumbusha waumini kuchukua tahadhari wakati wa mvua zinazoendelea kunyesha, ikiwemo kuhama maeneo hatarishi.

Musoma. Viongozi wa dini mkoani Mara wameombwa kutumia nyumba zao za ibada kuwakumbusha waumini kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua, ikiwemo kuhama maeneo hatarishi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Ombi hilo limetolewa leo Machi 13, 2026 mjini Musoma na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Rorya District, Dk Halfan Haule, wakati wa futari aliyoiandaa kwa waumini wa Kiislamu mkoani humo.

Mtambi amesema mvua tayari zimeanza kunyesha na kwa mujibu wa Tanzania Meteorological Authority zinatarajiwa kuendelea, hali inayoweza kusababisha madhara endapo wananchi hawatachukua tahadhari mapema.

“Tusaidiieni kuwaambia waumini wenu wasisubiri majanga yawakute. Wale wanaoishi mabondeni wahame mapema, mvua ni kubwa na bado itaendelea kunyesha,” amesema.

Amesema pia wananchi wanaosafiri wanapaswa kuwa waangalifu na kuepuka kuvuka mito iliyofurika kwa kuwa wanaweza kusombwa na maji.

Ameongeza kuwa endapo wananchi watachukua tahadhari mapema, athari za mvua hasa kwa maisha ya binadamu zinaweza kupunguzwa licha ya uwepo wa mvua nyingi.

Mbali na tahadhari za mvua, Mtambi pia amewaomba viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, umoja, upendo na mshikamano katika nyumba zao za ibada ili kusaidia kujenga jamii tulivu itakayorahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Baadhi ya wadau walioshiriki kwenye futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi mjini Musoma.  Picha na Beldina Nyakeke

“Msichoke kutimiza wajibu wenu wa malezi ya jamii. Tunahitaji kuwa na jamii yenye maadili mema na hilo linawezekana kwa ushirikiano wa wazazi na ninyi viongozi wa dini,” amesema.

Kwa upande wake, Shehe wa Mkoa wa Mara, Kassim Msabaha, amemshukuru Mkuu huyo wa mkoa kwa ushirikiano anaouonyesha kwa waumini wa Kiislamu na madhehebu mengine.

Amesema ushirikiano huo umeimarisha mahusiano kati ya Serikali na viongozi wa dini ndani ya mkoa huo.

“Sisi kila mwaka tunapofunga huwa tunakuja kufuturu hapa. Sio kwamba ni wajibu wako, bali ni kutokana na mapenzi uliyo nayo kwetu na kwa madhehebu mengine. Hakika umepanda mbegu ya upendo na nasi tunaahidi kulipa kwa upendo,” amesema.

Shehe Msabaha pia amewaagiza maimamu wote mkoani humo kuendelea kufanya dua na ibada kwa ajili ya kuombea amani ya nchi pamoja na kuwaombea viongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa maendeleo ya jamii.

Baadhi ya washiriki wa futari hiyo wamesema ni muhimu wananchi kuchukua tahadhari mapema dhidi ya mvua huku wakiiomba Serikali kuwachukulia hatua wale watakaokaidi agizo la kuhama maeneo hatarishi.

Mmoja wa washiriki, Fadhili Iddi, amesema bado kuna watu wanaoendelea kuishi katika mabonde na karibu na vyanzo vya maji licha ya hatari iliyopo.

“Inashangaza kuona watu bado wanaishi kwenye mabonde au karibu na vyanzo vya maji. Wengi wao wakipata majanga huwa wa kwanza kuilaumu Serikali. Ni vyema waondolewe mapema katika maeneo hayo,” amesema.

Naye Noela Maro amesema viongozi wa Serikali kuanzia ngazi za vitongoji hadi kata wanapaswa kusimamia kikamilifu zuio la ujenzi katika maeneo hatarishi.

“Watendaji wa mitaa, vitongoji na kata pamoja na wenyeviti wa serikali za mitaa wanatakiwa kulisimamia hili. Ujenzi holela uzuiwe mapema kabla mvua hazijaanza kusababisha madhara,” amesema.