Wanafunzi wafichua siri umahiri kwenye Kiingereza
Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyabulogoya ya jijini Mwanza akiwasilisha mada wakati wa mdahalo ulioshuhudiwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz (katikati).
Muktasari:
- Wadau wa elimu wanaamini kuwa kuimarishwa kwa programu za mijadala kunaweza kuwa suluhisho muhimu la kuboresha umahiri wa lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi hasa wa shule za umma nchini, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mbinu shirikishi za kujifunza.
Mwanza. Wanafunzi kutoka shule za umma na binafsi jijini Mwanza walioshiriki mdahalo kwa lugha ya Kiingereza wamefichua siri ya umahiri wao kuwa ni kujijengea utaratibu wa kutumia lugha hiyo muda wote wawapo shuleni na hata majumbani.
Wakizungumza baada ya kushiriki mdahalo Machi 30, 2026 uliowawezesha kujenga na kutetea hoja mbele ya hadhira, wanafunzi hao wamesema ushiriki wa mara kwa mara katika midahalo pamoja na kujiunga na klabu za Kiingereza umekuwa msingi mkubwa wa mafanikio yao.
Mdahalo huo ulihudhuriwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, ambaye alivutiwa na kiwango cha ufasaha, mbinu na ujasiri walio onesha wanafunzi hao.
“I'm really impressed with their English (Nimevutiwa sana na kiwango chao cha Kiingereza),” amesema huku akiwahimiza kuendelea kujifunza na kukuza uwezo wao.
Mkurugenzi wa Bright House of Change Organization, Godlove Shem (kushoto) akiwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz (kulia) alipotembelea ofisi za American Corner kujionea mdahalo wa wanafunzi wanufaika wa programu ya Pan African Debate.
Mdahalo huo ulifanyika katika ukumbi wa American Corner, Rocky City Mall jijini Mwanza, ukiandaliwa na Bright House of Change Organization kwa kushirikiana na Tanzania English Language Teachers Association kupitia Programu ya Pan African Debate inayolenga kukuza uwezo wa kufikiri kwa kina, mawasiliano na uongozi.
Mwanzilishi wa programu na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Godlove Shem amemwambia Balozi Lentz matokeo ya programu hiyo yanaonekana wazi kitaaluma.
Amesema wanafunzi wote walioshiriki programu hiyo jijini Mwanza walipata daraja la kwanza katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka jana, jambo linaloonyesha mafanikio ya mbinu hiyo.
Naye, Balozi Lentz ameahidi kuangalia namna ya kuunga mkono programu hiyo ili iendelee kuwa chachu ya mafanikio kitaaluma, kibiashara na kiuongozi.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata Nyabulogoya, Janeth Richard amesema mafanikio yao yanatokana na mazoea ya kuizungumza lugha ya Kiingereza katika mazingira yote.
“Tunazungumza Kiingereza muda wote tukiwa shuleni na hata nyumbani, na tunawahamasisha wenzetu kufanya hivyo,” amesema.
Mkurugenzi wa Bright House of Change Organization, Godlove Shem akiongoza mdahalo ulioudhuriwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz (kulia).
Naye Ester Kivishe amesema matumizi ya lugha hiyo katika masomo pamoja na kushiriki mijadala kumemsaidia kujenga ujasiri mkubwa wa kujieleza.
“Kiingereza kimenisaidia kushiriki mashindano mbalimbali ya speech and debate kwa miaka mitatu mfululizo,” amesema.
Mwanafunzi Joseph Fransisco amesema programu hiyo imewapa wajibu wa kuwafundisha wengine.
“Ukishajifunza unatakiwa uende shuleni kwako ukawasaidie wengine wawe kama wewe,” amesema.
Mnufaika wa Programu ya Pan African Debate, Aventina Peter amesema programu hiyo imemsaidia kukuza uwezo wa kufikiri kwa kina na kupanga hoja zenye mashiko.
“Imenisaidia kufikiri kwa upana na kujiamini zaidi hata darasani..naomba iendelee kwakuwa si tu tunajiaminj lakini tunapata fursa za kukutana na makundi mbalimbali ndani na nje ya nchi," amesema.
Mwalimu wa Kiingereza, Shadrack Richard amesema changamoto kubwa kwa wanafunzi wengi ni mabadiliko ya lugha kutoka Kiswahili hadi Kiingereza wanapoanza sekondari, hivyo kupitia programu hiyo wanatumia mbinu mbalimbali kuwafundisha wanafunzi kiingereza.
“Ndiyo maana midahalo imekuwa mbinu muhimu ya kuwasaidia wanafunzi kuondoa hofu na kujifunza kwa vitendo,” amesema.
Meneja wa fedha wa Bright House of Change Organization, Witness Mauki amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa elimu kuendeleza programu hiyo ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiamini, uongozi na matumizi ya teknolojia.