Wasanii wanne wa Tanzania waandika historia Venice Biennale
Venice, Italia. Wasanii wanne wa Tanzania wameandika historia mpya katika tasnia ya sanaa baada ya kushiriki Maonesho ya 61 ya Kimataifa ya Sanaa ya La Biennale di Venezia, moja ya majukwaa makubwa na yenye heshima zaidi duniani ya sanaa na utamaduni.
Wasanii hao, Turakella Editha Gyindo, Amani Abeid, Lazaro Samuel na Valerie Asiimwe Amani waliwakilisha Tanzania kupitia banda la taifa lililopewa jina “Minor Frequencies: The Inner Life of a Nation”, ambalo limezinduliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Rangi Gallery na Gervasuti Foundation.
Maonesho hayo, ambayo Tanzania inashiriki kwa mara ya pili pekee katika historia yake ndani ya Biennale, yalizinduliwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mbarouk Nassor, katika hafla iliyosheheni uzinduzi wa fahari ya taifa na mvuto wa kimataifa.
Tanzania iliwakilishwa pia na Kamishna Leah Elias Kihimbi, Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa kutoka wizara hiyo, pamoja na waratibu Lorna Benedict Mashiba na Martina Cavallarin kutoka Italia, walioshirikiana kuhakikisha maonesho hayo yanabeba viwango vya kimataifa huku yakihifadhi simulizi za Kitanzania.
Maonesho hayo yamejengwa kwenye dhana ya “kile kidogo kinaweza kubeba maana kubwa”, yakigawanywa katika sehemu nne za tafakuri: Mwili (The Body), Ishara (The Gesture), Kumbukumbu (The Archive) na Akili (The Mind), ambapo kila msanii amewakilisha eneo moja.
Turakella Editha Gyindo ameibeba dhana ya Mwili kupitia kazi yake “Testimonials from the Body”, akitumia lufa zilizolimwa na kuchakatwa na wanawake wa Morogoro pamoja na rangi za asili za udongo kuonesha uhusiano wa mwili, ardhi na kumbukumbu za utambulisho.
Kwa upande wake, Valerie Asiimwe Amani ameangazia Kumbukumbu kupitia kazi shirikishi inayokusanya ndoto zilizosahaulika au kupotea, ambapo wageni wanahamasishwa kuandika ndoto zao na kuziweka katika simulizi la pamoja linaloendelea kubadilika.
Lazaro Samuel amewakilisha Ishara kupitia michoro ya kihisia inayochochewa na maisha yake ya awali jijini Dar es Salaam, ikibeba simulizi za mapambano, uvumilivu na matumaini kupitia alama za rangi zisizopangiliwa kwa kanuni kali.
Naye Amani Abeid ameangazia Akili kwa kuchanganya motifu za utamaduni wa Kimaasai na ishara za usasa, akionesha mvutano kati ya urithi wa kitamaduni na ushawishi wa dunia ya kisasa katika kujenga utambulisho.
Ushiriki huo umeelezwa kuwa hatua muhimu kwa Tanzania katika kujiimarisha kwenye ramani ya sanaa ya kimataifa, huku ukisisitiza nafasi ya wasanii wa Kitanzania katika majukwaa makubwa ya kimataifa.
Maonesho hayo yanaendelea katika Gervasuti Foundation at Supernova, Venice, Italia, kuanzia Mei 9 hadi Novemba 22, 2026.