Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zitto aja na mpya kwa wananchi Kigoma Mjini

Muktasari:

  • Mgombea ubunge Kigoma mjini, Zitto Kabwe amesema endapo wananchi hao watamchagua atahakikisha anatetea wananchi wake bungeni na kuendeleza miradi yote aliyoianzisha wakati wa kipindi chake cha ubunge.

Kigoma. Mgombea ubunge Kigoma mjini, Zitto Kabwe amewaomba wananchi wa Kigoma kumchagua ili aweze kukamilisha miradi aliyokuwa ameianzisha katika kipindi chake alipokuwa mbunge mwaka 2015 hadi 2020.

Akizungumza leo Jumatano, Septemba 17, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Kagera, Zitto amesema miradi mingi imesimama na kusuasua baada ya yeye kuwa nje ya ubunge wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano.

Kabwe amesema wataifanya kata ya Kagera kuwa ya kimkakati endapo watamchagua kuwa mbunge na madiwani wake ili waweze kuwaendesha halmashauri hiyo.

Amesema gharama za kujifungua ni kubwa hivyo amewaahidi kuwa wakisikia amekuwa mbunge ataondoa gharama zote za kujifungua.

“Mkinichagua mimi kama mbunge na kunipa diwani wa kata hii ya Kagera nitaanzisha mfumo wa hifadhi ya jamii kwa kila mwananchi kuwa na bima ya afya,” amesema Kabwe.

Ameahidi wananchi hao endapo watamchagua kuwa mbunge wa jimbo hilo atakomesha mikopo ya riba kubwa maarufu kama kausha damu kwa kuanzisha mfuko ambao ataweka Sh1 bilioni na wananchi watakopa bila riba.

“Mikopo ya kausha damu imekuwa tatizo kwa wananchi wa jimbo hili imefikia hatua watu wanakimbia familia zao kwa sababu ya mikopo hiyo, hivyo nikiwa mbunge nitahakikisha nakomesha hilo,”amesema Zitto

Ameahidi akichaguliwa kuwa mbunge akifika bungeni jambo la kwanza kulishughulikia ni fidia kwa wananchi ambao hawajalipwa fedha zao katika eneo la kituo cha uwekezaji cha Kigoma (Kises).

Mgombea udiwani kata ya Kigoma, Hussein Kalyango amesema wananchi waliwapa nafasi ya kuongoza mji   wa Kigoma mwaka 2015-2020 hivyo wamefanya mengi ikiwemo miundombinu ya barabara na mambo mengine. Hivyo ni muhimu wakarudisha mji huo kwa chama chao Oktoba 29, 2025

Katibu wa Mipango na uchaguzi wa ACT Wazalendo, Ali Mbwiga amesema uchaguzi wa mwaka huu ni wa kimkakati, hawatakuwa tayari kuzuiliwa kumchagua mtu wanayemtaka.

“Kwenye swala la ubunge hatuhitaji mtu kutuchagulia hivyo tutampigia mgombea wetu Zito Kabwe ambaye anatosha na atatuletea maendeleo katika mji wetu, niwasihi msifanye makosa ndugu zangu,” amesema Mbwiga.