Mapinduzi yawakutanisha viongozi Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, amekutana na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda, Ikulu Zanzibar leo Januari 11, 2024. Picha na Mpigapicha Maalumu

Muktasari:

  •  Januari 12 ya kila mwaka, Wazanzibari wanasherehekea maadhimisho ya Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964

Dar es Salaam. Viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wameanza kuwasili visiwani Zanzibar kwa ajili ya sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964 na kuuondoa utawala wa Sultan.

Sherehe hizo zitakazofanyika kesho Januari 12, 2024 katika Uwanja wa Amaan, zitaongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa, wadau wa maendeleo na wananchi kwa jumla.

Tayari Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan yuko visiwani humo na amekuwa akishiriki shughuli mbalimbali  na jana alihutubia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kwenye shamrashamra za kulekea kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi.

Mawaziri wengine pia wako visiwani humo wakitekeleza majukumu yao huku wakitarajiwa kuwa sehemu ya maadhimisho hayo yatakayowakutanisha pamoja maelfu ya watu kutoka Bara na Visiwani.

Januari 8, 2024, Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko alifungua jengo la ofisi za mamlaka ya Mamlaka ya maji Zanzibar (Zawa) lililoko Madema, Zanzibar na siku hiyohiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alifungua kongamano ya kitaaluma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo.

Leo, Januari 11, 2024, Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, amekutana na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda, Ikulu Zanzibar.

Kwa kujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Zanzibar, Makonda amempongeza Rais Mwinyi kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya kwa kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 katika kipindi cha miaka mitatu kwa miradi mbalimbali ya maendeleo Zanzibar.

Kwa upande wake, Rais Mwinyi ampongeza Makonda kwa kuteuliwa kwake na kuanza kazi vizuri ya ujenzi wa chama hicho kwa umma.

Mwananchi itaendelea kukuletea yatakayojiri kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi. Endelea kufuatilia tovuti na mitandao yetu ya kijamii.