Algeria yatoa tani tisa vifaa vya elimu kumwenzi mwasisi wa taifa
Wanafunzi sekondari ya wasichana Benbella wakipokea sehemu ya tani tisa za vifaa vya elimu vilivyotolewa na Serikali ya Algeria katika shule hiyo Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Ahmed Benbella alikuwa mmoja wa wapigania uhuru wa Algeria, akawa Rais wa kwanza wa taifa hilo na mtetezi wa Umoja wa Afrika.
Unguja. Serikali ya Algeria imetoa tani tisa za vifaa vya elimu vyenye thamani ya Dola 250,000 za Marekani, sawa na Sh658.7 milioni kwa sekondari ya wasichana Ben Bella, Unguja Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kusherehekea uhuru wa nchi hiyo.
Vifaa hivyo vya uchambuzi wa takwimu, vifaa vya bweni na vya stadi za ufundi, vimetolewa kupitia Wakala wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Algeria (AICA) kwa shule hiyo inayobeba jina la mwanamapinduzi na Rais wa kwanza wa Algeria, Ahmed Ben Bella.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo vilivyotoka moja kwa moja nchini Algeria Julai 14, 2026, Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Ghalib Zermane amesema vifaa hivyo vilitengwa mahsusi kwa sekondari hiyo, ili kuimarisha uwezo wake wa kielimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na walimu wake.
“Mpango huu wa kibinadamu uliamuliwa na Rais Abdelmadjid Tebboune kama uthibitisho wa dhati wa kujitolea kwa Algeria kusaidia elimu, kukuza maendeleo ya binadamu na kuimarisha ushirikiano na nchi dada za Afrika,” amesema.
Pia, amesema ni sehemu rasmi ya sherehe za shughuli zilizopangwa na Ubalozi wa Algeria nchini katika kuadhimisha miaka 64 ya uhuru wa nchi hiyo ambao huadhimishwa Julai 5 kila mwaka.
Balozi huyo amesema uchaguzi wa shule hiyo ya sekondari kwa ajili ya msaada huo si wa bahati mbaya.
“Shule hii ina nafasi maalumu katika historia ya Zanzibar na Tanzania. Kwa karne nyingi imekuwa taa ya elimu na ubora. Mwaka 2024, shule hii ilisherehekea miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, ikitimiza miaka 100 ya kutoa huduma bora za elimu.
Amesema katika historia yake, sekondari ya Benbella imefundisha vizazi vya wanafunzi ambao baadaye wakawa watumishi waandamizi wa Serikali, wafanyabiashara, wataalamu na watu mashuhuri ambao wamechangia katika maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Amesema kusaidia taasisi kama hiyo yenye heshima kubwa, ni sawa na kuwekeza katika mustakabali wa Tanzania yenyewe.
Amewasihi wanafunzi hao kusoma kwa bidii, kuwa wadadisi, wenye ndoto kubwa na kamwe wasiruhusu malengo yao yakwame, kwa kuwa elimu ndio utajiri mkubwa.
“Leo ni siku yenu, na kila kitu tunachokisherehekea ni kwa ajili ya mustakabali wenu. Vifaa hivi vimeletwa kutoka Algeria kwa sababu tunaamini akili zenu, uwezo wenu na mustakabali wa Zanzibar, Tanzania hata Afrika upo mikononi mwa vijana kama ninyi,” amesema balozi huyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa amesema kuleta vifaa hivyo vyote kutoka Algeria hadi Zanzibar, kunaonesha wazi kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili sio urafiki tu bali ni udugu na udada.
“Tunaahidi kuvitunza vifaa hivi na tutahakikisha vinakuwa chachu ya kuongeza ufaulu katika shule hii,” amesema Lela.
Naibu Katibu Mkuu wa Taaluma, wa wizara hiyo, Dk Mwanahamisi Adam amesema vifaa hivyo vimegawanyika katika maeneo makuu matano; vikiwemo vya kujifunzia teknolojia, samani, vifaa vya bweni yakiwemo magodoro ya kisasa yanayojazwa upepo kwa mashine na vifaa vya michezo.
“Kwa hiyo ni jambo la kushukuru sana, na hili tunaomba kwa wao isiwe ni mwanzo, bali liwe ni suala endelevu, kwasababu tayari tumeshakuwa marafiki,” amesema
Naye, mkuu wa shule hiyo, Asha Mkubwa Khamis amesema ni siku ya furaha kwa shule kupata msaada huo na kwamba vitawasaidia katika shughuli za uendeshaji wa shule hiyo.
Amesema wanashirikiana katika mambo mbalimbali na Algeria ikiwa ni pamoja na kuwapa fursa za masomo kwa wanafunzi na walimu kwenda nchini humo kujifunza mambo mbalimbali ya kitaaluma.
Rais wa shule hiyo, Rayyan Hassan Bushir amesema watahakikisha wanatumia vifaa hivyo kujisomea na kuongeza maarifa wanafunzi ili kufikia ndoto zao.