Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bei ya dizeli, petroli yazidi kupaa Zanzibar

Unguja. Bei ya petroli na dizeli imeendelea kupanda Zanzibar sababu kubwa ikitajwa ni kupanda kwa gharama ya Dola ya Marekani.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), bei ya petroli imeongezeka Sh186, kutoka Sh3,001 hadi Sh3,187 sawa na asilimia 6 huku dizeli ikiongezeka kwa Sh41 kutoka Sh3,282 hadi Sh3,323 sawa na asilimia moja.

Akitangaza bei hizo leo Novemba 8, 2023 zitakazoanza kutumika kesho Novemba 9, 2023 Meneja Uhusiano wa Zura, Mbaraka Hassan Haji ametaja sababu za kuongezeka kwa bei hizo ni pamoja na kuongezeka gharama za mafuta katika soko la dunia.

"Gharama za uingizaji wa mafuta, uamuzi wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani (OPEC+) kupunguza uzalisha na vikwazo vya kiuchumi ambavyo nchi ya Urusi imewekewa na nchi za Magharibi," amesema Mbaraka.

Katika hatua nyingine mafuta ya ndege yatauzwa kwa Sh2,976 kutoka Sh2,768 sawa na asilimia saba, huku mafuta ya taa yakipanda kutoka Sh2,921 Hadi Sh3,300 sawa na asilimia 13.

Bila kutaja kiasi, amesema Zanzibar yapo mafuta ya kutosha ambayo yanatosheleza na hakuna uhaba wa rasilimali hiyo kwa sasa.

Alitaja sababu zingine kuwa nikuongezeka Kwa bidhaa hizo katika soko la dunia na kuongezeka gharama za uingizaji wa Nishati hiyo.

"Kinachoangaliwa kingine katika upangaji wa bei za mafuta ni pamoja na gharama za uingizaji mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, thamani ya shilingi ya Tanzania kwa Dola za Marekani, gharama za usafiri, bima na premium hadi Zanzibar, kodi za serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja," amesema.

Baadhi ya wananchi wakiwemo madereva wanaotumia mafuta hayo kwa wingi wameoiomba Serikali kuendelea kufidia Nishati hiyo kama ilivyokuwa ikifanya awali kupunguza makali hayo.

Rashid Khamis amesema, "Kila mwezi sasa mafuta yanapanda bei, zamani serikali ilipunguza makali kwa kufidia ingekuwa vyema ikaendelea kufanya hivyo maana watu wataumia sana,” amesema.

Kwa kipindi kirefu Serikali ya Mapiduzi Zanzibar ilikuwa ikifidia bei za mafuta kuwapunguzia adha wananchi za kupanda gharama za maisha. Hata hivyo kwa miezi kadhaa sasa bei za mafuta hayo zinatangazwa kutokana na uhalisia wake bila kuwekewa fidia.