Dk Mwinyi aikaribisha Romania kuwekeza uchumi buluu
Muktasari:
- Dk Mwinyi amemthibitishia Rais huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kufanya kazi na watu wa Romania kwa faida ya pande zote mbili.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ameiomba Serikali ya Romania kuja Zanzibar kuwekeza katika sekta ya uchumi wa bluu, utalii na sekta nyingine ili nchi iendelee kupiga hatua za kimaendeleo.
Dk Mwinyi alieleza hayo katika hafla ya chakula cha mchana na Rais wa Romania, Klaus Lohannis iliyofanyika leo Jumamosi Novemba 18, 2023 Ikulu mjini hapa baada ya kuwasili kwa ziara ya siku moja.
Amesema ukuaji wa nchi na ustawi wa baadaye unategemea uwekezaji na biashara katika uchumi wa bluu na utalii.
Ameikaribisha serikali hiyo na kampuni za nchi hizo kuja kufanya kazi na Zanzibar katika biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu, utalii na sekta nyingine kwa maslahi mapana ya pande zote mbili katika ajenda ya maendeleo.
"Ujio wa Rais Klaus umetoa fursa ya kutafakari juu ya uhusiano na mikakati ya ushirikiano zaidi kwa nchi hizi ili zieweze kuendelea kupiga hatua za kimaendeleo," amesema Rais Mwinyi.
Rais Mwinyi akizungumzia lengo la kukutana pamoja na ujumbe huo, ni kuthibitisha nia ya dhati ya serikali ya kuimarisha ushirikiano zaidi na nchi ya Romania.
Hivyo, amepongeza utayari wake wa kufanya kazi na Zanzibar katika ukuaji wa ustawi huo na hatua kubwa iliyofikiwa na nchi hizo mbili kutokana na historia kubwa ya kidemokrasia iliyowekwa na kuhakikisha nchi zao zinaendeleza mashirikiano yao ya karibu.
Dk Mwinyi amemthibitishia Rais huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kufanya kazi na watu wa Romania kwa faida ya pande zote mbili.
Naye Rais wa Romania, Klaus Lohannis amesema nchi hizo zina ushirikiano na urafiki wa muda mrefu ambao mwaka ujao unatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake kidiplomasia.
Amesema Zanzibar imekuwa sehemu ya pendwa kwa wawekezaji na Romania kwa kampuni zake na ushirikiano huo usingewezekana bila ya ukarimu, maono na tamaduni zao ambazo pia ni fursa kwao.
“Ushirikiano wetu unazidi kukua kwa sababu kuna muingiliano wa watu wa Romania na Tanzania licha ya kuwa na changamoto ya kijiografia na masuala ya utamaduni lakini changamoto hizi zinaweza kuwa ni fursa kwa nchi zetu,” amesema.
Amebainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuendeleza ushirikiano katika sekta uya utalii lakini pia katika kukuza uchumi na kubadilishana tamaduni kwa kuzingatia ulinzi na usimamizi wa urithi wa kiutamaduni.
Rais huyo amefurahishwa na Dira ya Mawendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 na muelekeo wake wa mawazo mazuri juu ya siku zijazo kwa maendeleo ya nchi yao.
Amepokea wazo la kuhusisha kampuni za Romania katika mpango wa Silicon Zanzibar (Fumba) na uchumi wa bluu ambapo ni moja miongoni mwa sababu yake kuwa Zanzibar kuhamasisha na kuunga mkono uhusiano unaokuwa kwa kasi wa uchumi wa Romania na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuendeleza biashara mpya hapa Zanzibar.
Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wa nchi yake kuja kwa wingi Zanzibar ili kujionea fursa mbalimbali zilizokuwepo katika sekta ya uwekezaji.
Mapema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu Jamal Kassim Ali, alisema ujio wa Rais huyo hapa Zanzibar anaamini itakuwa ni fursa kupata wawekezaji kutoka nchini Romania kuja kuwekeza Zanzibar.
“Ujio wake kupitia boti ya Kilimanjaro 8 inazidi kuitangaza Zanzibar katika sekta ya utalii ukizingatia sera ya serikali ni uchumi wa buluu ambapo ndani ya sera hiyo kuna mambo mbalimbali ikiwemo sekta ya utalii,” alisema.
Rais huyo pia amefanya ziara ya kutembelea maeneo ya Mji Mkongwe kwa vijana wanaopiga makachu katika pwani ya Forodhani na Kanisa la Mkunazini.