Ziara ya Rais Romania na fursa za uchumi Tanzania

Rais wa Romania, Klaus Iohanni.

Muktasari:

  • Katika harakati za kuikuza diplomasia ya uchumi ambayo ni moja ya ajenda kuu katika Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ujio wa Mkuu huyo unatazamwa kwa mrengo wa kuimarisha uhusiano wa biashara kati ya Tanzania na Romania.

Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kupokea ugeni wa Rais wa Romania, Klaus Iohanni, atakayewasili nchini kesho kwa ziara ya kitaifa ya siku nne.

Ziara ya mkuu huyo, inatazamwa kama tumaini jipya la kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Romania ambao ulipungua miaka ya hivi karibuni.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imebainisha kushuka kwa mauzo ya Tanzania katika taifa hilo kwa karibu mara mbili mwaka 2021 na 2022.

Kulingana na taarifa hiyo, mwaka 2021 Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 7.9 milioni (takribani Sh19.7 bilioni) ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo iliuza Dola za Marekani 4.06 milioni (takribani Sh10.14 bilioni).

Manunuzi ya Romania kwa bidhaa za Tanzania yalipungua pia, ikinunua bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 11.6 milioni (takribani Sh28.97 bilioni) huku mwaka 2022 ikinunua zenye thamani ya Dola za Marekani 2.4 milioni (takribani Sh5.9 bilioni).

Taarifa iliyotolewa leo, Novemba 15, 2023 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inabainisha ziara ya mkuu wa taifa hilo ni mwitikio wa mwaliko aliopewa na Rais Samia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ziara ya Iohannis ni ukurasa mpya wa kuimarika kwa ushirikiano wa nchi hizo ulioanza mwaka 1964 katika sekta za afya na elimu.

Taarifa hiyo inasema maeneo mapya ya ushirikiano yanatarajiwa kupatikana katika ziara hiyo, ambayo ni uwekezaji, elimu, utalii, afya na utamaduni.

“Kwa sasa uhusiano wa Tanzania na Romania unahusisha uwekezaji na biashara ya minofu ya samaki aina ya sangara, chai, tumbaku na parachichi.

“Tanzania inanunua bidhaa za mshine za umeme, vifaa vya matrekta, magari na vifaa vya matibabu kutoka Romania,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Siyo biashara pekee, hata uwekezaji na sekta ya utalii inatarajiwa kuimarika kutokana na ziara hiyo, kwani kwa sasa Romania imewekeza nchini katika miradi ya usafirishaji, viwanda na utalii yenye thamani ya Dola za Marekani 6.04 milioni na kuzalisha ajira 89.

Kwa upande wa Zanzibar, miradi mitatu yenye thamani ya Dola za Marekani 7.5 milioni kwa mwaka huu na kuzalisha ajira 64.

“Ziara hiyo ni fursa muhimu kwa Tanzania kuvuna soko la utalii kutoka taifa hilo, ambalo kwa sasa watalii kutoka Romania wameongezeka kutoka 6,418 mwaka 2018 hadi 12,148 mwaka 2022,” imeeleza taarifa hiyo.


Ziara itakavyokuwa

Mkuu huyo wa taifa hilo la Ulaya, anatarajiwa kuwasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNICC) na atapokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.

Novemba 17, mwaka huu kiongozi huyo atapokewa rasmi Ikulu ya Dar es Salaam na atafanya mazungumzo na Rais Samia yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Romania.

Baada ya shughuli hiyo, wawili hao watashuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano kati ya Tanzania na Romania katika sekta za kilimo, mifugo, misitu, chakula na uokoaji wakati wa dharura.

Siku inayofuata, Iohannis atasafiri kwenda visiwani Zanzibar kwa mazungumzo na Rais wa visiwani humo, Dk Hussein Mwinyi na akiwa huko atatembelea kivutio cha utalii cha Mji Mkongwe.