Hoteli ya nyota saba kujengwa Pemba

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Seleman Jafo akifungua kitambaa kuashiria uwekaji jiwe la msingi hoteli ya Tembo Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Inatajwa kuwa ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki. Itajulikana kwa jina la Montuli
Unguja. Zanzibar ipo mbioni kujenga hoteli ya nyota saba ambayo inatajwa itakuwa ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki.
Hoteli hiyo itakayojulikana kwa jina la Montuli itajengwa kisiwani Pemba ambapo imeelezwa tayari safari ya ujenzi wake imeanza.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi mradi wa Tembo Hotel and Beach Resort Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja Januari 6, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Sharif Ali Sharif amesema wamejipanga kukuza uwekezaji.
“Mipango ya baadaye ni mingi lakini kuna kitu kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki kinakuja, itajengwa hoteli ya kwanza ya nyota saba kisiwani Pemba, tumpongeze Rais Hussein Mwinyi kwa maono yake,” alisema
Pia, amesema kitajengwa kituo cha mikutano kitakachochukua watu 2,500 maeneo huru ya uwekezaji Fumba, huku kukitarajiwa pia kujengwa kwa viwanja vya michezo mchanganyiko ambapo miongoni mwa wawekezaji wake ni wanamichezo maarufu duniani.
Kwa mujibu wa Zipa, kipindi cha miaka mitatu miradi 296 yenye ajira 17,000 imesajiliwa ikiwa na thamani ya Dola za Marekani 4.5 bilioni sawa na Sh11.5 trilioni. Kati ya miradi hiyo, 112 sawa na asilimia 38 ni ya utalii.
Kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuna miradi 71 ambayo itatoa ajira 5830 sawa na asilimia 24 ya miradi yote ikiwa na mtaji wa Dola za Marekani 1.85 bilioni sawa na Sh4.6 trilioni.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Seleman Jafo amesema uwekezaji wowote lazima ulinde na kutunza mazingira ili kuepusha mabadiliko ya tabia nchi.
Mbali na kuepusha athari za mabadiliko ya tabia nchi, Dk Jafo amesema iwapo mazingira yatatunzwa, pia yatawashawishi watalii wakiondoka warejee tena lakini wakikuta mazingira mabovu hawawezi kurudi tena.
“Uwekezaji wowote lazima ulinde mazingira, tusipokuwa tayari na mabadiliko ya tabianchi, tutajikuta hata hizi fukwe nzuri ambazo watalii wengi wanakuja kutembelea zitajazwa na kina cha maji, kwa hiyo nduzu zangu tukumbuke sana jambo hili,” amesema
Pia amewasihi kulinda utamaduni wa Kizanzibari kwani wageni wengi wanakwenda Zanzibari kwa ajili ya utamaduni.
Amesema Serikali imewekeza katika miradi ya maji, barabara na hospitali hivyo watalii watakuwa na ujasiri kutembela kisiwa hicho, wakiamini huduma zote muhimu zinapatikana hawawezi kuhangaika.
Kauli ya mwekezaji wa hoteli
Mwekezaji wa hoteli hiyo, Hussein Muzamir alisema ameweka mtaji wa Dola za Marekani 8 milioni (Sh20.1 bilioni) na itaajiri watu 200 ikikmilika.
Amesema wanavutiwa kuwekeza kutokana na sera na mazngira wezeshi yaliyomo kisiwani humo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid alisema katika mkoa huo kuna hoteli 255 zinazotoa ajira 11,290 kati ya hizo 71 zimejengwa kipindi cha Serikali ya awamu ya nane.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamza Chillo alisema ipo haja wawekezaji wawe wanatenga fungu maalumu kwa ajili ya kuiwezesha jamii katika utunzaji wa mazingira na usafi katika maeneo husika.
Hata hivyo, alisema ajira zitakazotolewa katika hoteli hiyo, kipaumbele cha kwanza kiwe kwa vijana wanaotoka katika eneo hilo.