Kamati ya maadili ya uchaguzi yazinduliwa

Muktasari:
- Wajumbe wa kamati hii ni vyama vyote vya siasa vyenye usajili, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca), Msajili wa Vyama vya Siasa, Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ.
Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji Aziza Suwedi, amezindua rasmi kamati ya maadili ya uchaguzi ya kitaifa ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha uchaguzi wa baadaye mwaka huu unakuwa huru, haki na wa amani.
Uzinduzi wa kamati hiyo ni sehemu ya mchakato wa kushirikisha wadau wa uchaguzi hususan vyama vya siasa kuandaa kanuni ya maadili ya uchaguzi 2025, kama inavyoelekezwa na sheria ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Maadili hayo yatapitishwa na vyama vya siasa kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za uchaguzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Julai 10, 2025, Jaji Aziza Suwedi amesema kuanzishwa kwa kamati ya maadili ya uchaguzi ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018.
“Lengo likiwa ni kuwashirikisha wadau wa uchaguzi kikamilifu na kutoa maoni yao kwa kamati hiyo ili kusaidia mambo mbalimbali ikiwemo kutungwa kwa kanuni madhubuti za Uchaguzi Mkuu 2025, na kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa maadili wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi,” amesema.
Kwa mujibu wa Jaji Aziza kamati hiyo ni kiungo muhimu kati ya wadau wa uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama, wananchi na lengo ni kuhakikisha kuwa maadili yanazingatiwa hasa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina amesema kamati hiyo ndio inayoshughulikia maadili yote wanayoipangia kwa hiyo kinapotokea chama kikaenda kinyume wanajipangia adhabu.
“Hii ni wanasiasa wanajiandalia maazimio wao wenyewe ili wakikosea wanajiadhibu wenyewe, mfano mtu kafanya kampeni mpaka saa moja usiku, mtu katukana afanywe hivi, kwa hiyo maadili hayo wanatakiwa wayasaini kabla ya kuanza kampeni,” amesema.
Mjumbe wa kamati hiyo, Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CCM Zanzibar, Khamis Mbeto amesema uwepo wa kanuni hizo utasaidia katika kuongoza mchakato wa uchaguzi kuwa sawa kwa kila upande.
Amewasihi wadau wa kisiasa kuzikubali na kuzisimamia kwa pamoja kama watakavyokubaliana na kusaini, huku akipongeza hatua hiyo kwani ni madhubuti ya kuimarisha uwajibikaji na kushughulikia changamoto za uchaguzi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea, Ali Makame Issa amesema hatua hiyo inaonyesha dhamira njema ya kuhakikisha kila chama kinasimamia maadili, ili uchaguzi uwe wa amani na mshikamano kwa masilahi ya Taifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Makini, Amir Hassan Amir amesema makubaliano hayo yanatoa mwanga wa kinachotakiwa kufanyika kwa kila chama bila kuwa na upendeleo wowote, hivyo kikitokea chama fulani kikakengeuka lazima hatua zichukuliwe bila kuangalia nafasi na ukubwa chama.
“Hii kamati ina wajumbe wote wa vyama vya siasa kwa hiyo, kinachokubaliwa hapa ni kwa ajili ya wote, tunataka na iwe hivyo kuzingatia maadili kwa kila ngazi inayopitiwa,” amesema Amir.
Uzinduzi wa kamati hiyo ni sehemu ya mchakato wa kushirikisha wadau wa uchaguzi hususan vyama vya siasa kuandaa kanuni ya maadili ya uchaguzi 2025, kama inavyoelekezwa na sheria ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar, maadili hayo yatapitishwa na vyama vya siasa kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za uchaguzi.