Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kanisa Katoliki Zanzibar lawezesha wanawake mikopo isiyo na riba

Wanawake wajasiriamali Wilaya ya Kaskazini B wakifuatilia mafunzo ya kujiendeleza na kuwa na  nidhamu ya fedha yanayotolewa na Idara ya Maendeleo ya Jamii Kanisa katoliki jimbo la Zanzibar shule ya Msingi Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Mbali na kupewa elimu, wanakopeshwa mikopo isiyokuwa na riba na kutengenezewa katika na fomu za mikopo inayohidhishwa na sheha katika shehia tano Wilaya ya Kaskazini B Unguja.

Unguja. Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar limeanzisha mpango wa kuwawezesha wanawake wajasiriamali wa Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali na mikopo isiyo na riba, likilenga kuwaongezea uwezo wa kiuchumi na kupunguza utegemezi katika familia.

Kupitia mpango huo, wanawake wanapatiwa elimu ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, uwekaji wa akiba, uendeshaji wa vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na namna ya kukuza mitaji kupitia benki za jamii.

Wanufaika hao wamesema hayo leo Jumapili, Julai 19, 2026, baada ya kushiriki mafunzo yanayotolewa kupitia mradi wa Community Empowerment in Justice and Good Governance (CEJG Phase V) unaotekelezwa na Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar.

Mjasiriamali wa kushona shuka na vitambaa vya makochi kutoka Misufini, Amina Alfred Mhana amesema mafunzo hayo yamewapa wanawake uelewa wa kujitegemea kiuchumi badala ya kutegemea kila kitu kutoka kwa waume zao.

"Mbali na kuwezeshwa mikopo, tumejifunza umuhimu wa nidhamu ya fedha. Mwanamke anatakiwa kujishughulisha na kazi itakayomwezesha kutimiza mahitaji yake ya kila siku," amesema.

Amesema mafunzo hayo pia yamewasaidia kuelewa umuhimu wa kuthamini hata kipato kidogo na kukitumia kwa malengo ili biashara iweze kukua.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa mbogamboga kutoka Shehia ya Mkataleni, Selima Juma, amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni kuyumba kwa bei za mazao, hali inayosababisha wakati mwingine kuuza bidhaa chini ya gharama ya ununuzi.

"Unaweza kununua tenga la nyanya kwa Sh80,000 au Sh120,000, lakini ukifika sokoni ukauza kwa hasara hadi kushindwa kurejesha mtaji," amesema.

Hata hivyo, amesema elimu waliyoipata pamoja na fursa ya mikopo isiyo na riba itawasaidia kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi.

Selima ambaye anawalea watoto watano, amesema hakuwahi kujiunga na vikundi vya kuweka na kukopa, hivyo amekuwa akijitafutia mtaji peke yake.

Naye Jamila Hamad Haji wa Shehia ya Mahonda, amesema aliingia kwenye biashara ndogondogo baada ya mume wake kuugua na kushindwa kuihudumia familia.

Amesema kabla ya mafunzo hayo hakuwa na utamaduni wa kuweka akiba kwa sababu aliamini kipato chake cha kila siku, ambacho wakati mwingine ni Sh5,000, hakitoshi.

"Tumefundishwa kuwa hata fedha kidogo inaweza kuwekwa akiba na baadaye ikawa mtaji unaosaidia kukuza biashara," amesema.

Kwa upande wake, Zaina Mohamed Bakari kutoka Shehia ya Donge Majenzi amesema biashara ya chipsi za muhogo ndiyo inayomwezesha kuwasomesha watoto wake wanane pamoja na kugharamia masomo yao ya madrasa.

Ofisa wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Msafiri Thomas, amesema lengo la mradi huo ni kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini kupata mitaji na kuboresha maisha yao.

Amesema mikopo inayotolewa haina riba na hutolewa kupitia vikundi vya watu 10 hadi 15, ambapo wanachama wanaweza kukopeshana na kuongeza kiwango cha mkopo kulingana na uaminifu wao katika urejeshaji.

"Tumeshaunda vikundi katika shehia tano za Mahonda, Misufini, Kitope, Mkataleni na Majenzi. Pia tumewaandalia katiba, fomu za uanachama na mikopo ambazo zimeidhinishwa na masheha wa maeneo husika," amesema.

Mwezeshaji wa mafunzo ya benki za jamii na mikopo ya vikundi, Joseph Mushi amesema changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wengi ni ukosefu wa elimu ya biashara na kutokuwa na malengo ya muda mrefu.

"Wengi wanafanya biashara kwa mazoea bila mipango wala nidhamu ya fedha. Ukiweka malengo na ukasimamia biashara yako kwa muda mrefu, matokeo mazuri yanapatikana," amesema.

Naye Sheha wa Shehia ya Bumbwini Misufini, Khamis Ussi Mlinde, amesema wananchi wameupokea mradi huo kwa matumaini makubwa kutokana na mchango wake katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Amesema tayari elimu inayotolewa imeanza kuleta mabadiliko kwa baadhi ya wanufaika na kuwataka wananchi kuitumia fursa hiyo kuboresha maisha yao badala ya kuipuuzia.

"Huu ni mradi utakaowasaidia wanawake kujitambua kiuchumi na kuongeza kipato cha familia zao. Tunawahimiza wananchi kuutumia kikamilifu kwa manufaa yao," amesema.