Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinachoendelea Mangapwani atakapozikwa Mzee Mwinyi

Shughuli za kupanga jukwaa kuu zikiendelea Mangapwani atakapozikwa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.

Muktasari:

  • Mwili wa aliyekuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi utazikwa nyumbani kwake, Mangapwani, Unguja visiwani Zanzibar leo Jumamosi. Alifariki dunia Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Unguja. Wakati taratibu za kuaga mwili wa aliyekuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi zikiendelea katika Uwanja wa Aman, shughuli za kukamilisha maandalizi atakapozikwa Mangapwani nazo zinaendelea.

 Mzee Mwinyi aliyefariki dunia Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam, atazikwa leo Machi 2, 2024 Machi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja katika shamba la familia Mangapwani ambalo aliliandaa kwa ajili ya maziko ya familia yake.

Mpaka sasa katika eneo hilo kuna kaburi moja la mtoto wake, Hassan Ali Mwinyi aliyefariki dunia Agosti, 2022 ambapo Mzee Mwinyi atazikwa pembeni mkono wa kushoto mwa kaburi la mtoto wake.

Shughuli za uchimbaji wa kaburi tayari zinaendelea chini ya Usimamizi wa askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

LIVE: Mwili wa hayati Mwinyi ukiagwa Zanzibar

Mbali na shughuli za uchimbaji wa kaburi, pia askari wa JWTZ wanaendelea na mazoezi mbalimbali jinsi watakavyojipanga, kuupokea mwili na kutembea nao hadi eneo la kaburi.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid, kaburi limechimbwa leo Jumamosi, Machi 2, 2024 kwasababu ya taratibu za dini. Kwa kawaida dini ya Kiislamu kaburi linachimbwa siku ambayo maiti inazikwa na si vinginevyo.

Rashid amesema maandalizi yamekamilika kwa asilimia kubwa na wapo tayari kuupokea mwili wa kiongozi huyo.

Pia, Mwananchi Digitali imeshuhudia malori sita ya JWTZ yaliyobeba mizinga yakiingia na kuanza kuishusha mbali kidogo ya eneo hilo ambalo limezungukwa na minazi na asili ya majani marefu.

Mizinga hiyo itapigwa wakati wa shughuli za maziko zitakapokuwa zikiendelea kama ulivyo utaratibu wa viongozi wakuu kupigiwa mizinga 21 wakati wa maziko yao wanapofariki.

Katika eneo hilo ambalo kuna msikiti uliokuwa unajengwa na Mzee Mwinyi ambao haujakamilika, imendaliwa jukwaa dogo kwa ajili ya viongozi wakuu wa kitaifa wakiongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan watakaohudhuria mazishi hayo.

Kazi nyingine inayondelea ni kutandika mabusati katika matenti ambayo yatatumika kuisalia maiti baada ya kuwasili katika eneo hilo kabla ya kupelekwa kaburini. Eneo hilo lipo umbali wa takribani mita 200 kutoka ilipo kaburi.

Wakati hayo yakiendelea tayari wananchi wa kutoka maeneo mbalimbali Mkoa huo wameanza kuwasili katika eneo hilo kwa ajili ya kushiriki mazishi hayo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kassim Ali amesema amefika kumuaga Mzee Mwinyi kwasababu ya ukarimu na busara alizokuwa nazo Marehemu.

"Mimi nimetoka Kama, nimesema lazima nifike ili nikamsindikize Mzee wetu katika safari yake ya milele, ni kutokana na busara na mambo mengi aliyolifanyia taifa hili," amesema

Mwingine Abdulla Masoud amesema atamkumbuka Mzee Mwinyi kuruhusu biashara huria kwani wakati wa Utawala wake ndio kipindi ambacho mfumo wa kufanya biashara ulirahisishwa na kila aliyekuwa na uwezo kufanya biashara akifanya bila vikwazo.

Mzee Mwinyi aliagwa jana Ijumaa jijini Dar es Salaam, kisha mwili wake ulisafirishwa na ndege ya Jeshi hadi Zanzibar.

Katika Uwanja wa ndege wa Amein Abeid Karume, ulipokewa na viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Rais Samia na Dk Mwinyi kisha ukapelekwa kulala nyumbani kwake Bweleo Mkoa wa Mjini Magharibi.

Kwa mujibu wa ratiba, mwili utawasili Mangapwani saa 9:00 alasiri, utakapowasili utaibwa wimbo wa Taifa kisha wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Baada ya nyimbi hizo, saa 10:00 yataanza mazishi ya Kiserikali, yatafuata mazishi ya Kidinii kisha utasomwa wasifu wa Marehemu. Wasifu huo utasomwa na Katibu Mkuu Utumishi, Juma Mkomi na huo utakuwa mwisho wa na viongozi kuanza kuondoka eneo hilo.

Kwa hatua ya sasa, hairuhusiwi kupiga picha ama video.