Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwinyi alivyowaaga wakazi wa Mkuranga

Muktasari:

  •  Mfanyakazi shambani kwake aeleza atakavyomkumbuka

Mkuranga. Mariam Abdallah, mkwe wa Hayati Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema miezi minne iliyopita aliwaaga akiwaeleza anaenda kupata matibabu nje ya nchi.

Mariam ni mkazi wa Kijiji cha Binga, wilayani Mkuranga ambako pia yako makazi ya Mwinyi.

Akizungumza na Mwananchi leo Machi mosi, 2024 kuhusu kifo cha Mwinyi kilichotokea Februari 29, Mariam amesema: "Alikuwa anafikia nyumbani kwa sababu pale ni kwa mwanawe, yaani baba yake mume wangu na baba yake hayati Mwinyi walizaliwa na baba na mama mmoja."

Mariam amesema miezi minne iliyopita alienda kijijini hapo na aliwaaga.

"Alituambia kwaherini naenda kupata matibabu nje ya nchi, Mungu akipenda nitarudi," amesema Mariam.

Amesema pia, alimuasa mwanawe Maulid Magandi kwamba ahakikishe anasimamia mali na wafanyakazi wote.

"Alimwambia mimi naondoka naomba uwasimamie hawa wanangu (wafanyakazi), hakikisha wanaendelea na kazi na wanakuwa na amani. Alimwambia aangalie na mashamba pia," amesema.

Mariam Abdallah

Mariam amesema Hayati Mwinyi aliwataka wahakikishe wanaishi kwa amani na kumpenda kila mmoja.

"Alitwambia yeye hakugombana na watu nasi tusigombane na yeyote tuishi kwa amani na watu," ameeleza.


Mfanyakazi wake

Mmoja wa wafanyakazi katika nyumba yake, Gerald Boaz amesema kila alipofika kijijini hapo, Hayati Mwinyi hakuacha kutembelea maeneo matatu.

Maeneo hayo ni yalipo makaburi ya bibi na babu yake, shambani kwake na yalipokuwa makazi ya baba yake.

Kati ya mashamba aliyokuwa akiyatembelea, Boaz amesema zipo ekari takribani 30 za korosho katika eneo la Vikalakala pembezoni mwa kijiji hicho.

"Kila akija alitembelea maeneo hayo akawa anatuuliza maendeleo ya mashamba yake mawili," amesema.

Kisima cha maji kilichopo Kijiji cha Binga, wilayani Mkuranga.

Atamkumbuka kwa haya

Boaz aliyeanza kazi kwa Hayati Mwinyi Julai, 2022 amesema hatasahau pale alipokuwa akipewa fedha nje ya mshahara kila hayati Mwinyi alipofika nyumbani hapo.

"Alikuwa akinipa fedha ananiambia nikanunue sabuni, hiyo ni nje ya mshahara wangu. Alikuwa mkarimu sana," amesema Boaz.

Amesema anakumbuka mazungumzo yake ya mara kwa mara na Hayati Mwinyi kila alipofika kijijini hapo.

"Alikuwa ananiuliza kuhusu maendeleo ya shamba, ananishauri niwe napanda mbogamboga ili niuze kupata hela za ziada kwa ajili ya matumizi yangu.

"Alikuwa ananiambia mshahara anaonilipa haunitoshi na hata anaolipwa yeye haumtoshi inabidi tutafute vyanzo zaidi. Kwa hiyo akawa ananishauri nipande mbogamboga  nipate hela nje ya mshahara anaonilipa," amesema Boaz.

Maulid Omary, mkazi wa kijiji hicho amesema hayati Mwinyi alijenga madrasa msikiti, kisima kirefu cha maji na nyumba ya kukaa sheikh.

Omary, sawa na mkazi mwingine Hamza Bazoka wamesema aliwaahidi kujenga shule ya sekondari na hospitali.

Kwa sasa wanafunzi wa sekondari wanalazimika kusafiri kwa saa mbili hadi Kijiji cha Dondo ilipo shule.

Kwa upande wa huduma za afya, wamesema wanaenda Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga umbali wa takriban saa tatu kupata huduma zikiwamo za kujifungua wajawazito.