Prime
Mambo 10 yanayompa Mwinyi wasifu wa pekee

Muktasari:
- Wakati Mwinyi alipopendekezwa kisha kupitishwa kuwa Rais wa Zanzibar, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais. Kwa maana hiyo, Mwinyi alikuwa msaidizi wa Jumbe. Ni kwa vile Jumbe alikuwa Rais wa Zanzibar, nafasi hiyo pia ilikuwa inampa cheo cha Makamu wa Rais.
Dar es Salaam. Jinsi alivyoingia madarakani ni kitu cha kwanza kinachompa upekee Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi (98). Amefariki dunia leo Alhamisi, Februari 29, 2024, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na kuacha mambo ya kukumbukwa.
Kupanda kimadaraka kwa Mwinyi kulitokana na kuchongewa zaidi barabara kuliko kujichongea.
Mwaka 1984, Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, alipolazimishwa kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, jina la Mwinyi likapendekezwa awe mrithi wa Jumbe, hivyo akapitishwa kuwa Rais wa Tatu wa Zanzibar bila kukivujia jasho kiti hicho.
Wakati Mwinyi alipopendekezwa kisha kupitishwa kuwa Rais wa Zanzibar, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais. Kwa maana hiyo, Mwinyi alikuwa msaidizi wa Jumbe. Ni kwa vile Jumbe alikuwa Rais wa Zanzibar, nafasi hiyo pia ilikuwa inampa cheo cha Makamu wa Rais.
Utulivu wa Mwinyi, haiba na hulka yake ya kutokuwa na makundi, ni sababu inayotajwa kumvutia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuona ndiye mtu sahihi kuiongoza Zanzibar katika nyakati zilizokuwa na mkorogo mkubwa kisiasa, baada ya Jumbe kung’olewa.
Ni urais huo wa Zanzibar uliompa Mwinyi urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na hutakosea ukisema Mwinyi ni Mtanzania mwenye bahati zaidi, kwani vyeo vyake vikubwa vinathibitisha kila kitu waziwazi.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa, chaguo la Mwalimu Nyerere mwaka 1985, alikuwa Waziri Mkuu wa zamani, Salim Ahmed Salim. Hilo la kwamba Salim alikuwa chaguo la Mwalimu Nyerere, limethibitishwa pia na Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, kupitia kitabu chake “My Life, My Purpose” ‘Maisha Yangu, Dhamira Yangu’.
Msekwa, kwa ufafanuzi wake, alisema wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, walimkataa Salim kwa sababu alikuwa waziri mkuu na kwa cheo, Mwinyi alikuwa mkubwa zaidi. Kwa cheo cha Rais wa Zanzibar, Mwinyi alikuwa pia Makamu wa Rais wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Msekwa, wajumbe wa Nec, walimkataa Salim kuwa Rais kwa hoja kuwa kama angepitishwa yeye wakati alikuwa waziri mkuu, ingetoa picha mbaya kwa Mwinyi, ambaye ndiye alikuwa bosi. Hiyo ni tafsiri kuwa Mwinyi hakupigania urais, wala hakupeleka jina, isipokuwa watu walimtaka na kumpigania. Akawa Rais.
Kitu cha pili cha upekee wa Mwinyi tofauti na marais wengine ni namna alivyoshughulika na kero za wananchi.
Kipindi akiwa madarakani, kila Ijumaa, Mwinyi aliweka utaratibu wa kuwasikiliza moja kwa moja wananchi wenye matatizo mbalimbali na kuwatatulia papo hapo au kwa mchakato. Mikutano hiyo na wananchi aliifanyia ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam.
Upekee wa tatu wa Mwinyi upo kwenye hotuba zake. Wakati marais wengine hotuba zao za Kiswahili zikichanganywa na Kiingereza, kwa Mwinyi, alitumia zaidi Kiarabu. Ni mara chache mno, Mwinyi alipokuwa Rais, alichanganya Kiingereza na Kiswahili.
Mwinyi, ndani ya hotuba zake, alikuwa mahiri katika kufanya rejea kupitia aya zilizomo kwenye kitabu kitakatifu cha Quraan na mara chache alifanya marejeo kwenye Biblia. Hilo ni eneo ambalo linafanya hotuba za Mwinyi ziwe na ladha ya kipekee. Nasaha nyingi, ukumbusho wa Mungu na maelekezo ya utii kwa nchi.
Katika marais wanne wanaume ambao wameshaiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni Mwinyi pekee aliyekuwa na wake wawili katika miaka yake 10, Ikulu, Magogoni, Dar es Salaam. Wake hao ni Sitti na Khadija. Hata hivyo, Sitti ndiye aliyetambulika kama mwanamke namba moja (first lady), kipindi chote cha urais wa Mwinyi. Hilo ni la nne.
Jambo la tano la upekee wa Mwinyi ni kuzaliwa na kukua kwake. Mwinyi, alizaliwa Mkuranga, Pwani, Tanganyika, kisha akakulia Unguja, Zanzibar. Hadi sasa, ndiye Rais pekee wa Tanzania mwenye sifa hiyo. Maisha yake yalijenga tafsiri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kabla ya kuzaliwa Tanzania.
Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Nyerere, alizaliwa na kukulia Tanganyika, kama ilivyo kwa Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, wa nne, Jakaya Kikwete, vilevile wa tano, Dk John Magufuli. Wakati Rais wa sita, Samia Suluhu Hassan, alizaliwa na kukulia Zanzibar.

Sita ni uamuzi wa Mwinyi kujiuzulu uwaziri wa Mambo ya Ndani mwaka 1977, baada ya Polisi mkoani Shinyanga kupiga watu kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya uchawi.
Sifa hiyo inamfanya Mwinyi kuwa Rais pekee wa Tanzania kuwahi kupata misukosuko ya uongozi alipokuwa waziri mpaka kulazimika kujiuzulu, halafu kurejea kupanda ngazi hadi kufikia urais wa Zanzibar na baadaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jambo la saba ni kuwa Mwinyi alipokuwa Rais wa Tanzania, hakutaka wananchi wasumbuliwe barabarani kwa sababu ya msafara wake. Mwinyi aliwazuia askari wa usalama barabarani, kufunga barabara na kuzuia magari kwa muda mrefu kusubiri yeye apite na msafara wake.
Mwinyi ndiye Rais wa kwanza wa Tanzania kumzika aliyempokea kijiti cha uongozi, akamzika pia anayemkabidhi kijiti. Alimpokea Mwalimu Nyerere mwaka 1985. Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999. Alimkabidhi kijiti Mkapa Novemba 1995. Mkapa alifariki dunia Julai 24, 2020.
Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, naye alimzika mtangulizi wake (Mkapa), pia aliyempokea mikoba, kwa maana ya Dk John Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17, 2021. Hilo ni la nane.
Tisa ni ruhusa ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. Angalau hili linabaki kuwa alama ya Mwinyi kuwa ndiye Rais wa Tanzania aliyeruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Ni baada ya kufutwa mwaka 1962 na Mwalimu Nyerere.
Kumi Mwinyi ni alama ya uhuru wa vyombo vya habari, kwani vyombo binafsi vilianza Mwinyi akiwa Rais, kisha vikawa vingi wakati wa Mkapa. Hilo la vyombo binafsi inaingia kwenye mwamko wa sekta binafsi ambayo ilipata njia salama wakati wa Mwinyi.