Mapya sakata la pombe Zanzibar, latinga kortini

Unguja. Wamiliki wa makontena 25 na magari manane ya pombe yaliyokwama katika Bandari ya Malindi visiwani Zanzibar, wamefungua kesi mahakamani dhidi ya mkurugenzi mtendaji wa bandari hiyo na Bodi ya Udhibiti wa Vileo Zanzibar (ZLCB).

Wamiliki hao kampuni za ZMMI, Scotch Store na One Stop Company, wamefungua kesi hiyo kwa kile kilichoelezwa katika hati ya kiapo kuwa ZLCB imeidharau mahakama.
Msingi wa kesi hiyo ni hatua ya ZLCB na bandari hiyo kuzuia shehena ya mzigo huo, kwa kile kilichoelezwa kampuni hizo hazikuwa na vibali halali vya kuagiza, kuingiza, kuuza na kusambaza bia visiwani humo.

Februari mwaka huu, ZLCB ilimwandikia barua mkurugenzi wa Bandari ya Malindi, Nicholas Eshalin ikimtaka asitekeleze amri ya awali ya mahakama iliyomtaka aruhusu kampuni hizo ziendelee na biashara zao.

“Bodi ya Kudhibiti na Udhibiti wa Pombe ya Zanzibar inapenda kukujulisha kuwa ZMMI, Scotch Store, One Stop Company hawaruhusiwi kuingiza vinywaji vya pombe kutokana na kutofaulu kupata vibali vya kuagiza vinywaji vya pombe Zanzibar,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Hatua ya ZLCB kuandika barua hiyo, ilitokana na amri ya awali ya Mahakama iliyotaka kampuni hizo ziruhusiwe kuendelea na shughuli zao.

Februari 19, mwaka huu, Mahakama visiwani humo chini ya Jaji Rabia Hussein Mohamed ilitoa amri ya kuondoa zuio la shehena hizo baada ya kuridhishwa na uhalali wa kampuni hizo.

Amri ya Mahakama iliitaka ZLCB kutoingilia shughuli au leseni za waombaji. Hii inahakikisha biashara zao zinaendelea bila kuingiliwa.

Bodi hiyo pia ilitakiwa kutoa leseni za uagizaji, usambazaji na uuzwaji kwa kampuni hizo. Hii inaruhusu wao kuendelea na uagizaji na uuzaji wa vinywaji vya pombe.

Pia iliamuru bodi kuwaruhusu waombaji kuendelea na shughuli zao za awali ambazo ni pamoja na kununua, kusambaza, kusafirisha, na kuuza vinywaji vya pombe mara moja.
Kutokana na mazingira hayo, kampuni hizo zilifungua kesi zikiituhumu ZLCB kuidharau Mahakama na kukiuka utawala wa sheria kwa ujumla.

Shitaka hilo linadai ZLCB licha ya kupokea amri ya Mahakama kupitia kwa maofisa wake kwa makusudi imepuuza.

Katika hati ya kiapo, kampuni hizo zinadai ZLCB imeidharau Mahakama: Matendo yao yaliiweka Mahakama katika fedheha" na "kushambulia maadili" ya mfumo wa kisheria.

Pia kampuni hizo zinadai kilichofanywa ni ukiukwaji wa utawala wa sheria kwa kutokukubaliana na amri ya Mahakama, ZLCB ilidaiwa kudhoofisha utawala wa sheria, ambao unategemea uadilifu na sifa ya Mahakama.

Hati hiyo inasisitiza mkurugenzi wa bandari, bodi na wengine walizuia utawala wa haki kwa kuzuia uwezo wa mahakama kuhakikisha haki inatendeka.

Waagizaji, kupitia hati hiyo, wanatataka Mahakama iwashitaki maofisa wa ZLCB kwa kudharau Mahakama ambayo inaweza kutoa adhabu mbalimbali, ikiwemo faini au hata kifungo.

Hata hivyo, kampuni hizo zitalazimika kusubiri muda zaidi, ili maombi yao yafanyiwe uamuzi baada ya kubainika kuwa jaji anayesimamia kesi hiyo yuko nje ya kituo cha kazi kwa sasa.