Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muhali bado kikwazo vitendo vya udhalilishaji

Wadau wa masuala ya ukatili wa kijinsia wakiwa katika kikao cha pamoja kuandaa mikakati mipya ya Kupambana na vitendo vya udhalilishaji katika Mkoa wa Kaskazini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Hata hivyo, kinachotia moyo ni hatua zinazochukuliwa ikiwamo utoaji elimu, wadau wa kupinga vitendo hivyo kuongezeka na Serikali kuanzisha Mahakama maalumu ya udhalilishaji.

Unguja. Wakati Serikali na wadau mbalimbali wakiendelea na juhudi za kupambana na vitendo vya udhalilishaji, bado muhali na hofu ya kuripoti matukio hayo yameendelea kuwa kikwazo kikubwa katika kutokomeza tatizo hilo. Hali hii imesemwa leo Jumapili, Mei 25, 2025, katika kikao kilichoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake (UN Women), kilichowakutanisha wadau wa kupinga udhalilishaji Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika kikao hicho, wadau wamesema licha ya kuanza kuonekana kwa mabadiliko kidogo kutokana na juhudi za elimu na hatua za Serikali, bado kuna haja kubwa ya kuendelea kuelimisha zaidi hasa kwa makundi yanayoonekana kuchangia kwa kiwango kikubwa vitendo hivyo. Miongoni mwa makundi hayo ni waendesha bodaboda na vijana wanaokusanyika maskani au vijiweni, ambao wanatajwa kama wahusika wakuu katika matukio mengi ya ukatili.

Asia Fadhil Makame, Msaidizi wa msaada wa kisheria Wilaya ya Kaskazini A, amesema muhali ndani ya jamii umekuwa chanzo cha watu kushindwa kutoa ushahidi, hali inayokwamisha kesi za udhalilishaji.

“Kesi hukaa muda mrefu bila kusikilizwa kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi, jambo linalovunja moyo wa waathirika,” amesema Asia. Hata hivyo, amepongeza ongezeko la wadau wanaopinga vitendo hivyo pamoja na hatua ya Serikali kuanzisha Mahakama maalumu za kushughulikia kesi za udhalilishaji.

Omar Ali Khamis, msaidizi wa sheria Wilaya ya Kaskazini B, ameongeza kuwa mara nyingi wahusika wa vitendo hivyo ni watu wa familia, hali inayowafanya wanandoa au wazazi kuona aibu kuripoti na kuamua kumaliza matatizo kienyeji. Pia amesema talaka holela zimeendelea kudhoofisha uimara wa familia, na baada ya wazazi kutengana, watoto hukosa malezi bora na kujiingiza kwenye hatari mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Madrasa na mjumbe wa kamati ya hifadhi ya mtoto, Muhamed Suleiman Juma, amesema tatizo linaanzia pale wazazi wanaposhindwa kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto, kuanzia wakiwa tumboni hadi wanapokua.

“Huduma zinapokosekana mapema, mwisho wake kinachojitokeza ni matukio ya udhalilishaji,” amesema Muhamed.

Mratibu wa Mradi wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kutoka UN Women, Lucy Tesha amesema mradi wao wa miaka mitatu unalenga kukabiliana na changamoto zinazowakumba watu wanaoishi kwenye mazingira magumu, ambao ndio waathirika wakuu wa ukatili.

“Watu maskini hukumbwa zaidi na ukatili, kwa sababu ya changamoto za kipato na chakula. Mradi huu unaweka mkazo katika kubuni mikakati ya kupunguza umaskini na kuondoa udhalilishaji,” amesema Tesha, akisisitiza umuhimu wa kuwa na kauli moja katika mapambano hayo.