Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau walia danadana sheria ya habari Zanzibar

Mwandishi wa habari mkongwe Salim Salim akizungumza katika maadhimisho ya uhur wa vyombo vya habari ambapo alikuwa mgeni maalumu Unguja Zanzibar

Muktasari:

  • Zanzibar ina sheria mbili kubwa zinazoongoza uandishi wa habari nazo ni sheria usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu namba tano ya mwaka 1988 na sheria namba saba ya Tume ya Utangazaji ya mwaka 1997.

Unguja. Wadau wa habari Zanzibar wameendelea kuhoji sababu za kuchelewa kwa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, mchakato ambao umedumu kwa karibu miaka 20.

Hivi sasa, Zanzibar bado inatumia sera ya habari ya mwaka 2006 na sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 1988.

Wakizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani yaliyofanyika jana Jumamosi Mei 24, 2025, wadau hao wamesema ukimya wa Serikali juu ya suala hilo unaibua wasiwasi kuhusu utayari wake wa kufanya mabadiliko. Mwanahabari mkongwe, Salim Said Salim amesema zaidi ya vikao 30 vimefanyika kujadili marekebisho hayo, lakini hadi sasa haijulikani wapi mchakato huo umekwama.

“Sheria nyingine zaidi ya 100 zimetungwa na zingine kufanyiwa marekebisho mara kadhaa, lakini kwa sheria ya habari imekuwa nongwa, jambo hili halina afya kwa sekta ya habari,” amesema Salim.

Ameongeza kuwa pia kuna vipengele vya sheria ya uchaguzi, ikiwemo kifungu cha 126, vinavyoweka mazingira magumu kwa wanahabari kwa kuzuia kutangaza matokeo yaliyobandikwa kwenye vituo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Idara ya Mawasiliano, Imane Duwe amesema sheria zilizopo hazilingani na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na muswada uliopendekezwa ungeweza kutatua changamoto nyingi.

“Inasikitisha kuona vikao vinaendelea bila matokeo. Serikali isione waandishi wa habari kama maadui, sekta hii inahitaji mazingira bora kisheria kwa maendeleo ya taifa,” amesema Imane.

Ofisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Juma Sanifu amesema ingawa changamoto zipo, kuna maboresho fulani katika utambuzi wa mazingira ya kazi za wanahabari.

Naye Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Salum Ramadhan amesema mchakato wa marekebisho unaendelea na upo karibu kufika mwisho, akiwataka wadau kuwa na imani.

Hata hivyo, licha ya ahadi nyingi na hatua mbalimbali, ukimya wa sasa umesababisha wadau kuhoji hatima ya marekebisho hayo na mustakabali wa sekta ya habari Zanzibar.