Othman: Safari ya maridhiano bado ndefu
Muktasari:
- Makubaliano hayo yalisainiwa Julai 9, 2026, Ikulu Zanzibar, mbele ya viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi. Yalihusisha hoja kuu saba, huku moja kati ya hizo ikiwa na vipengele 10.
Unguja. Siku tatu baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo kusaini makubaliano ya kuanza mchakato wa kumaliza mkwamo wa kisiasa Zanzibar, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, amesema safari hiyo bado ni ndefu na ngumu, lakini chama hicho hakitatembea kwa woga.
Othman amesema licha ya changamoto zilizopo, wataendelea kusimamia hoja walizokubaliana kwa lengo la kurejesha imani ya Wazanzibari na kujenga misingi wanayoamini itasaidia kuimarisha mustakabali wa Zanzibar.
Akizungumza leo Jumapili, Julai 12, 2026, katika Ukumbi wa Picca Dily wakati wa mkutano na viongozi wa mikoa na majimbo ya Unguja Nyamanzi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Othman amesema mpaka kufikia hatua ya kusaini makubaliano hayo haikuwa kazi rahisi.
Amesema kuanzia Novemba 9, 2025, hadi Julai 9, 2026, vyama hivyo vimefanya vikao rasmi 14, vikao viwili vya pamoja na vikao viwili vya kamati kabla ya kufikia makubaliano hayo.
Kiongozi huyo amesema hoja kubwa waliyoibeba katika majadiliano hayo ilikuwa kurejesha imani kwa wananchi wa Zanzibar ambao, kwa maoni yake, wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali, hasa wakati wa uchaguzi.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud akizungumza na viongozi wa majimbo na Mikoa saba ya Unguja kichama katika ukumbi wa Dicca Dily Nyamanzi Mkoa wa Mjini Magharibi
“Ndugu zangu, bado hatujafika mwisho wa safari. Kwanza ndiyo safari inaanza, na kwa taarifa yenu, tunapokwenda ndiyo kugumu zaidi kuliko hatua tuliyomaliza. Lakini hatutayumba wala hatutachukulia haya yanayotokea kama sadaka au hisani,” amesema Othman.
Amesema chama hicho hakitaingia katika mchakato huo kwa hofu, bali kitasimamia masuala yanayowagusa Wazanzibari kwa kuzingatia haki na maslahi yao.
“Hii siyo kwenda kuvuruga maridhiano wala kufunika matatizo. Tunataka kusimamia yale yote wanayoyataka Wazanzibari. Hii ni siasa mpya yenye malengo,” amesema.
Makubaliano hayo yalisainiwa Julai 9, 2026, Ikulu Zanzibar, mbele ya viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi. Yalihusisha hoja kuu saba, huku moja kati ya hizo ikiwa na vipengele 10.
Akifafanua baadhi ya vipengele hivyo, Othman amesema vinahusu mageuzi katika mfumo wa utoaji haki, utumishi wa umma na serikali za mitaa, huku wakitaka msimamizi mkuu awe diwani kama inavyoelezwa katika Katiba badala ya masheha.
Amesema pia wamekubaliana kuhusu masuala ya vitambulisho vya Mzanzibari, maeneo maalumu ya kura ya mapema, daftari la wapigakura, uwepo wa Tume ya Maridhiano, kamati ya ushauriano wakati wa uchaguzi, vyombo vya habari vya umma, vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi pamoja na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Othman amesema wakati wa majadiliano walikutana na vizingiti mbalimbali, lakini kila hoja waliyoitoa waliijengea hoja hadi kufikia makubaliano.
Amesema endapo kutakuwa na changamoto katika utekelezaji wa makubaliano hayo, watarejea kwa wananchi na wanachama kuwaeleza hatua iliyofikiwa.
Kuhusu kuingia ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Othman amesema hilo litafanyika baada ya kuundwa kwa kamati ya pamoja kati ya CCM na ACT-Wazalendo.
Viongozi wa matawi, majimbo na Mikoa saba ya Unguja ya Chama cha ACT Wazalendo wakimzikiliza mwenyekiti wa chama hicho taifa, Othman Masoud wakati akizungumza nao katika ukumbi wa Dicca Dily Nyamanzi Mkoa wa Mjini Magharibi
“Tunakwenda kuunda kamati ya pamoja na wenzetu wa CCM. Baada ya hapo tutakaa ndani ya chama kujadili na kuona tunaingia SUK kwa utaratibu gani,” amefafanua.
Amesema pia kutaundwa tume ya utekelezaji itakayokuwa na jukumu la kusimamia makubaliano hayo, huku mchakato wake ukipelekwa Baraza la Wawakilishi ili kutungwa sheria.
Katika hatua nyingine, Othman amemjibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, kuhusu kauli yake ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa, akisema nchi inapaswa kuendeshwa kwa misingi ya weledi na sheria.
Amesema viongozi wanapotoa uamuzi kuhusu masuala ya kisiasa, wanapaswa kuzingatia misingi ya nchi na kutotengeneza migogoro isiyokuwapo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji, amesema ana matumaini makubwa kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayo ikilinganishwa na yaliyopita, kwa sababu yamesainiwa hadharani mbele ya wananchi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, amesema chama hicho kinaamini maslahi ya wananchi ndiyo msingi wa hatua wanazochukua na wataendelea kuwa wastaarabu katika mchakato huo.