Rais Karume ‘alivyoliamsha’ marekebisho ya Katiba Zanzibar

Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Jana tuliangalia namna Rais Amani Abeid Karume alivyoandika historia ya kisiasa kwa kufanikisha maridhiano ya kisiasa Zanzibar. Leo tunaangalia namna alivyozua taharuki baada ya kufanya marekebisho ya 10 ya Katiba yaliyoitaja Zanzibar ni nchi.

Marekebisho hayo ya Katiba yalizua taharuki na kuzusha mijadala ya kikatiba, lakini wanazuoni walitoa tafsiri ya neno ‘nchi’ kwamba ni dola na hali ikatulia.

Rais Karume na Katibu Mkuu wa CUF kwa wakati huo, Maalim Seif Sharif Hamad walifikia maridhiano ya kumaliza uhasama wa kisiasa kati ya chama tawala CCM na upinzani CUF Zanzibar katika mazungumzo yao ya faragha yaliyofanyika mwaka 2009.

Marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 2010, ilikuwa ni moja ya hatua ya maridhiano hayo, ili kuwezesha kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na kubadili muundo wa Serikali kwa kuondoa cheo cha Waziri Kiongozi na kuweka Makamu wa Rais wawili.

Makamu wa kwanza wa Rais akitoka upinzani na makamu wa pili akitoka kwenye chama tawala.

Hata hivyo, marekebisho hayo ambayo moja ya vifungu vyake ni yale yaliyosema Zanzibar ni nchi ambayo inaweza kujiendesha yenyewe kutokana na rasilimali zilizopo, yalizua mijadala ya kikatiba kwamba yamekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuhatarisha Muungano.

Wakati marekebisho hayo yakieleza hivyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa Tanzania ni nchi moja na eneo lake la mipaka ni kuanzia Tanzania Bara hadi Visiwani.

Marekebisho hayo ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 yalitajwa kuongeza migongano, hasa ibara ya 1(1) inayoeleza kuwa Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyozungukwa na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilikuwa ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Pia, ibara ya 2(a) ya Katiba ya Zanzibar ilimpa uwezo Rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika mikoa na wilaya, kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mjadala mwingine ulioibuka ni kuhusu muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kwamba ni sehemu gani sera ya CCM imesema ikishinda uchaguzi itaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Marekebisho yaliyoonekana kuvutia wengi kwenye Katiba hiyo ni yale ya kuongeza idadi ya viti maalumu kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40, tofauti na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua idadi hiyo kwa asilimia 30.


Profesa Shivji adadavua neno ‘nchi’

Mwanazuoni nguli, Profesa Issa Shivji, mbobezi wa sheria alitoa andiko akidadavua mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar kama kweli yamezaa nchi ya Zanzibar na hivyo kuwepo nchini mbili zenye Serikali mbili.

Kwa mujibu wa Profesa Shivji, mara nyingi katika msamiati wa kawaida maneno Serikali na dola yanachangaywa na kwamba ili kujua tafsiri yake sahihi inabidi kuangalia muktadha wake.

Profesa Shivji alinukuu ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar: “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”

Profesa Shivj alisema neno linalotatiza ni ‘nchi’. “Lakini tujiulize, neno hili 'nchi' inamaanisha dhana ipi? Hoja yangu ni kwamba neno 'nchi' katika muktadha wa Katiba inamaanisha dhana ya ‘dola’ na ndivyo limetumika katika Katiba ya Zanzibar pamoja na Katiba ya Muungano.

Mfano, ibara ya 9(1) ya Katiba ya Zanzibar inasema: "Zanzibar ni nchi ya kidemokrasia na haki za kijamii". Maneno hayo hayo yametumika katika Katiba ya Muungano: Ibara ya 8(1): "Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii.

“Katika hili hakuna shaka kwamba neno ‘nchi’ limetumika kumaanisha dhana ya dola, ambayo ni sahihi kabisa.”

Kwa mujibu wa Profesa Shivj, kama kweli mabadiliko ya 10 yaliitangaza Zanzibar kama nchi kwa maana ya "country", basi Zanzibar wangeuandikia Umoja wa Mataifa (UN) kwamba kwa mujibu wa Katiba yao Zanzibar ni 'sovereign republic' yenye 'international personality'.

“Hii haijafanyika. Katika ngazi ya kimataifa kuna 'sovereign republic' moja tu na ni Jamhuri ya Muungano. Bila shaka, kwa mambo ya ndani, mamlaka yamegawanyika kati ya dola ya Muungano na dola ya Zanzibar (divided sovereignty). Na ndivyo inavyotokea katika muungano na shirikisho,” alisema Profesa Shivj.


Neno nchi ndani ya Katiba

Pia, ndani ya Katiba ya Zanzibar neno nchi limetumika mara nyingi kuelezea masuala mbalimbali yanayohusu Zanzibar kwa kuitaja kama nchi, mfano ibara (9)(i) inataja ‘Zanzibar itakuwa ni nchi ya kidemokrasia na haki za kijamii’.

Ibara ya (9)(2)(a) inataja Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe …ibara ya 10 inataja, kwa madhumuni ya kuendeleza umoja na maendeleo ya watu na ustawi wa jamii katika nchi itakuwa ni wajibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ibara ya 10 (3) inataja …itadhibiti uchumi wa nchi kufuatana na misingi na madhumuni yaliyoelezwa na katiba hii.

Pia, ibara ya 12 (3) inataja haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu yatalindwa na kuamuliwa na Mahakama pamoja na vyombo vya nchi na vinginevyo vilivyowekwa na sheria.

Ibara ya 21 (i) inataja, kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi na ibara ya 23 (2) inataja, kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili ya Zanzibar, mali ya nchi pamoja na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi.

 Itaendelea Jumatatu ambapo kutakuwa na simulizi ya utawala wa Rais wa saba, Dk Ali Mohamed Shein.