Rais Mwinyi ataja mbinu za kuondoa utalii wa msimu Zanzibar

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema ili kuvunja mwiko wa kuwa na utalii wa msimu, Serikali imeamua kwa makusudi kuanzisha utalii wa matukio ili wageni waingine kwa kipindi chote kisiwani hapo.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 29, 2023 wakati akizungumza katika mbio za Zanzibar International Marathon zilizodhaminiwa na Tigozantel Unguja, ambapo amesema kwa kipindi kirefu Zanzibar inategemea utalii wa fukwe na historia na iwapo wakiacha hivyo watalazimika kuwa na msimu mkubwa na msimu mdogo.
“Bado sekta kuu ya uchumi Zanzibar ni utalii ambao unachangia asilimia 30 ya Pato la Taifa kwahiyo lazima tuweke juhudi zote kwenye utalii na miongoni mwa juhudi hizo ni pamoja na kuanzisha matukio kama haya,” amesema Dk Mwinyi
“Zanzibar inategemea utalii wa aina mbili zaidi, utalii wa fukwe za bahari na utalii wa historia lakini tumeona wazi kwamba tukiendela hivyo tutakuwa na misimu ya utalii, msimu mkubwa na msimu mdogo, kwahiyo tunataka kuondokana na hilo na ndio maana tumekuja na kile kinachoitwa utalii wa matukio,”ameongeza.
Amesema watakuwa na matamasha kadhaa ili mwaka mzima wageni wafurike Zanzibar na kwamba matamasha ya michezo yana umuhimu wake wa kipekee tofauti na tamasha mengine kwani yanaleta ajira, kukuza uchumi na kujenga afya.
Ameyataja baadhi ya matukio ambayo tayari yameanzishwa ni pamoja na Tamasha la Mambo ya Filamu (ZIF) linalowakutanisha watu wa filamu, sauti za busara, na sasa matukio mbalimbali ya michezo.
Amesema mbio hizo za marathoni zina faida kubwa zinapunguza maradhani yasiyo ya kuambukiza.
“Mtakumbuka kwamba Zanzibar imepata ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, saratani, moyo kiharusi na moyo sasa moja ya dawa ni mazoezi kwahiyo tukiwa na tabia ya kufanya mazoezi tutapunguza magonjwa hayo,” amesema
Kwahiyo nachukua fursa hii kuipongeza Zanzibar International marathon kwa kukubali kuleta kubadilisha na kupeleka katika miezi hii tunaona
Kuhusu mashindano ya Afcon mwaka 2027, Dk Mwinyi amewataka watendaji na viongozi kujipanga ili wasije kupoteza fursa hiyo maana ni kubwa lazima watoe huduma bora na wanufaike na michezo hiyo mikubwa inayokuja nchini humo
Naye Ofisa Mkuu wa Tigo Pesa, Angelica Pesha amesema wamekuwa mstari wa mbele kuwekeza Zanzibar katika masuala ya mawasiliano kuongeza kasi ya intaneti na inathibitisha kuwa azma yao ya kuwajumuisha Wazanzibar katika mapinduzi ya teknolojia.
Amesema hivi karibuni wamesaini makubaliano ya kimkakati na serikali ya Zanzibar yenye lengo la kupeleka mkongo wa mawasilino kama hatua muhimu kusambaza mtandao wa kidigitali na kuongeza upatikanaji wa intaneti.
“Mkongo huu utawezesha huduma ya miundombinu ya huduma mbalimbali kma CCTV kamera kwa ajili ya usalama na huduma za afya kimtandao na miradi ya kidigitali,” amesema
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Tabia Mwita Maulid amesema michezo inaleta umoja hivyo wananchi na wadau wengine waendelee kuunga mkono jitihada za serikali kuleta mapinduzi.
Mashindano hayo ambayo washiriki wametoka nchi za Afrika Mashariki, yalikuwa na mbio za kilometa 21, kilometa 10 na kilometa tano ambapo washindi ameibuka na zawadi mbalimbalimbali.
Mshindi wa kwanza wanaume kilometa 21 Josephat Kiko kutoka Tanzania amepata zawadi ya Sh3.5 milioni na komputa mpakato na mshindi wa kwanza wa kike mbio hizo Lilian Lele kutoka Kenya naye akipokea zawadi hizo.
Washindi wa kwanza mbio za kilometa 10 wamepata zawadi ya Sh2 na komputa mpakato ambao ni John Naasi na Anastazi Doromoni huku washindi wa kwanza wa kilometa tano wakipata Sh2 milioni.