Rushwa ya ngono yatajwa tishio ajira hotelini

Baadhi ya wananchi waliopatiwa vitu kwa ajili ya mama na watoto katika Kituo cha afya PwaniMchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani. Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Waajiri wametakiwa kutotumia rushwa ya ngono dhidi ya wanawake wanaotafuta ajira, badala yake wazingatie elimu, ujuzi na ufanisi wa kazi.

Unguja. Changamoto ya rushwa ya ngono kwa wanawake wanaohitaji kazi mahotelini imetajwa kuwa ni kikwazo cha kutofikia malengo ya wengi katika kazi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa mwajiri wa hoteli ya Melia Zanzibar, Sabra Omar Hussen leo Machi 8, 2024 katika Kituo cha Afya cha Pwanimchangani, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

"Wanawake wanakutana na manyanyaso makubwa ya ngono wakati wanahitaji kuajiriwa katika sehemu hiyo ya kazi. Hapo ndipo yule mwajiri anatumia nafasi hiyo ya kumuomba kulala naye kwanza na wakati mwingine anafanya hivyo na kazi hapatiwi, hii si sahihi kwa kweli," amesema Sabra.

Ameeleza akiwa mwanamke aliyekaa miaka 10 kwenye kazi hiyo ya hoteli, hapendi kuona aina hiyo ya unyanyasaji ukiendelea kufanyika kwa wingine.

Amesema, mwajiri yeyote anapaswa kuangalia uwezo wa mtu na vigezo vya kazi kwa kuzingatia zaidi cheti cha mtu, kwani ndicho kitakachomfanya kuajirika na si ngono wala aina nyingine ya rushwa.

Sabra amesema wanawake wana mchango mkubwa katika kazi hiyo, hivyo hawana budi kujiamini na wala wasiwe na hofu zinapotokea fursa hizo wazichangamkie.

Meneja Mkuu wa Hoteli ya Melia Zanzibar, Nicolas Konig amesema jamii inapaswa kuondokana na unyanyasaji wa wanawake hasa katika maeneo yao ya kazi ili kuonyesha uwezo wao wa kiutendaji.

Amesema uongozi wa hoteli hiyo unajitahidi kuwapa kipaumbele wanawake kwa kuwalinda na kuwatetea kwa hali yeyote ili kutimiza haki zao.

"Nikiwa kiongozi katika hoteli hii, sipendi kuona mwanamke yeyote ananyanyasika katika hoteli ambazo ninazimiliki, ninajitahidi kuweka miongozo na mikakati ya kuhakikisha kila mtu anapata haki sawa na mwenzake," amesema Konig.

Amesema leo ikiwa siku njema duniani kwa wanawake wote, wameungana na wenzao kuadhimisha siku hiyo muhimu ikiwa lengo ni kuthamini mchango na juhudi wanazozifanya katika kuleta maendeleo.

Sambamba na hayo, Subra amesema kituo hicho cha afya kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kufanyia usafi, magamba (kadi) ya kliniki ndio maana wamefanya juhudi za kuwasaidia baadhi ya vitu ikiwemo sabuni, mopu, pampasi na mafyagio.

Naye mtaalamu wa maabara katika kituo hicho, Seif Abdulla Seif amesema ndani ya mwaka mmoja wanaweza kutumia mopu moja kwa ajili ya kufanyia usafi, jambo ambalo ni hatarishi kwa afya zao na wagonjwa wanaofika katika kituo hicho.