Serikali yalaani unyanyasaji watu unaoendelea mwezi wa Ramadhan

Muktasari:

  • Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetoa msimamo wake na kulaani vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea kufanyika wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetoa msimamo wake na kulaani vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea kufanyika wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Machi 30, 2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Charles Hillary imesema kuvumiliana kidini, ndio msingi wa mshikamano hivyo haitamvumilia mtu yeyote anayeonekana kuashiria uvunjifu wa amani kwa misingi ya kidini.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kuibuka matukio kadhaa yanayoonyesha watu kushambuliwa kwa madai ya kula na kunywa hadharani wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Kutokana na matukio hayo, tayari Jeshi la polisi limewashikilia watu 12 wakidaiwa kukutwa wakinywa na kula hadharani katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa kukiuka utaratibu.

Mbali na watu hao kushikiliwa, pia Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT), imeitoza faini ya Dola za Marekani 500 (Sh1.2 milioni) kampuni ya kutembeza watalii ya Organisateur Francophone Tours and Travel kwa madai ya kuruhusu wageni wake kula hadharani tofauti na miongozo.

Katika taarifa yake Hillary ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, amehimiza wananchi kutenda mema na kudumisha amani, umoja na mshikamano kisiwani humo.

“Serikali inalaani vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea kufanyika sehemu mbalimbali Zanzibar, kadhia hiyo ni kinyume na misingi ya kuvumiliana katika imani za kidini,” amesema.

Amesema Zanzibar ni nchi yenye historia kongwe ya uvumilivu wa kidini ambapo Uislamu na Ukristo ziliingia mapema kuwa sehemu muhimu ya utamaduni uliodumu kwa karne nyingi.

“Hii inatufundisha kuhusu ustaarabu wa Wazanzibari kuvumiliana kidini na ndio msingi wa mshikamano miongoni mwetu,” amesema

Amesema Serikali inawahimiza wananchi kujizuia kwa namna yoyote kuingilia uhuru wa mtu binafsi katika kuabudu.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Serikali, Zanzibar inaongozwa kwa Katiba, hivyo SMZ ina mamlaka ya kulinda Katiba ya nchi na watu wake hivyo hatua yoyote yenye kuhatarisha umoja, amani na mshikamano haitavumilika.

“Serikali itaendela kulinda kudumisha amani na upendo kama mafundisho ya dini zetu yanavyotutaka, tofauti zetu za kidini zisiwe chanzo cha kuvuruga amani, umoja na mshikamano wetu,” amesema.