Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh5.7 bilioni zapeleka kicheko kisiwa cha Songosongo

Ujenzi wa kivuko katika chelezo ya Malindi Mkoa wa Mjini Magjaribi Unguja kitakachotoa huduma zake katika kisiwa cha Songosongo Kilwa Kivinje Mkoa wa Lindi. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Imeelezwa tangu kupatikana kwa uhuru mwaka 1961 kisiwa hicho licha ya kuwa na rasilimali muhimu ya mafuta lakini hakijawahi kupata usafiri wa uhakika wakati mwingine wananchi kuzama na kupotea baharini.

Unguja. Baada ya miaka mingi ya kukabiliwa na changamoto za usafiri wa majini, wananchi wa Kisiwa cha Songosongo, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, wameanza kuona mwanga wa matumaini baada ya kuanza kwa ujenzi wa kivuko cha kisasa kitakachoboresha usafiri na kuchochea biashara katika eneo hilo.

Kivuko hicho chenye thamani ya Sh5.7 bilioni kinajengwa kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kama sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa kurejesha kwa jamii (CSR). Ujenzi wake unafanywa na kampuni ya Qiro Group Ltd.

Akizungumza leo Julai 15, 2026 wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa kivuko hicho katika chelezo cha Bandari ya Malindi, Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema mradi huo utakuwa faraja kubwa kwa wananchi wa Songosongo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za usafiri.

Amesema licha ya kisiwa hicho kuwa na umuhimu mkubwa kiuchumi kutokana na uzalishaji wa gesi asilia na shughuli za utalii, usafiri wa majini umekuwa changamoto kutokana na kutegemea vyombo ambavyo havikuwa na uhakika wa kutosha.

Mkurugenzi wa kampuni ya Qiro Group, Yang Hao, akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zaina Telack ujenzi unaoendele wa kivuko cha Songosongo, Kilwa Kivinje wakati wa uzinduzi ujenzi huo leo katika chelezo ya Malindi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

“Kisiwa hiki ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Kuna gesi inayozalishwa pale, pia ni eneo la utalii lenye hoteli kubwa. Sasa kivuko hiki kitasaidia wananchi na hata watalii kufika kwa urahisi, jambo litakaloongeza shughuli za kiuchumi,” amesema Telack.

Amesema kuimarika kwa usafiri wa majini kutafungua fursa zaidi za utalii na biashara, hivyo kuongeza manufaa kwa wananchi wa Songosongo na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Songosongo, Hassan Mbai amesema ujenzi wa kivuko hicho ni kama kuzaliwa upya kwa kisiwa hicho chenye wakazi takribani 5,600, ambao tangu uhuru mwaka 1961 wamekuwa wakitegemea vyombo visivyo na uhakika.

Amesema changamoto za usafiri zimekuwa zikifanya hata wataalamu wa Serikali na taasisi mbalimbali kupata ugumu wa kufika kisiwani humo kutekeleza majukumu yao.

“Kwa niaba ya wananchi wa Songosongo na Kilwa, tunayo furaha kubwa. Tunaamini usalama wa safari zetu utaimarika baada ya kupata kivuko hiki,” amesema Mbai.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TPDC, Fransis Mwakapalila amesema shirika hilo linatambua mchango wa Kisiwa cha Songosongo katika uchumi wa nchi kupitia uzalishaji wa gesi asilia.

 “TPDC imetenga Sh5.76 bilioni kwa ajili ya mradi huu. Fedha hizo zinatokana na usimamizi madhubuti wa mapato ya ndani na kuhakikisha rasilimali za nishati zinawanufaisha wananchi,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Vivuko wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), Lukombe King’ombe amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa vivuko vingine sita vitakavyotoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa kivuko katika chelezo ya Malindi Mkoa wa Mjini Magjaribi Unguja kitakachotoa huduma zake katika kisiwa cha Songosongo Kilwa Kivinje Mkoa wa Lindi. Picha na Jesse Mikofu

Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na kivuko cha Kisiwa cha Mafia-Nyamisati na vivuko vitano vitakavyotoa huduma katika Ziwa Victoria.

Mshauri elekezi kutoka Taasisi ya Bahari Dar es Salaam (DMI), Lazaro Isaac, amesema kivuko hicho kitakuwa na urefu wa mita 28.8 na upana wa mita nane, kikiwa na uwezo wa kubeba abiria 154, magari madogo mawili na mizigo yenye uzito wa tani 10.

Amesema mradi huo utatekelezwa ndani ya miezi minane na unatarajiwa kukamilika Februari 2027. Tayari mkandarasi amelipwa Sh1.5 bilioni na utekelezaji umefikia asilimia 31.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Qiro inayotekeleza mradi huo, Yang Hao, maarufu Makame Mchina, amesema kampuni yake itahakikisha kivuko kinakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa.