Sheria, tume ya ulinzi wa taarifa binafsi mbioni Zanzibar
Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga akizungumza na waadishi wa habari kuhusu Tamasha la Data Afrika 2026 linalotarajia kufanyika kwa mara ya kwanza Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Hatua hiyo inalenga kuhakikisha taarifa za watu zinawekewa ulinzi kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ambayo pamoja na manufaa yake makubwa lakini inakua katikati ya changamoto.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema ipo mbioni kuanzisha sheria na tume ya ulinzi wa taarifa binafsi ili kuhakikisha usalama wa taarifa kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi, Juni 25, 2026 na Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu Tamasha la Data Afrika 2026 linalotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza Zanzibar.
“Kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia kwa sasa tupo kwenye mipango ya kuunda tume ya ulinzi wa taarifa binafsi na sheria yake, hii ni kutokana na ukuaji,” amesema.
Soraga amesema Zanzibar inaelekea kuwa kitovu cha masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutokana na juhudi zinazoendelea ikiwemo kuimarisha miundombinu ya kidijitali, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi yanayochochea uwekezaji katika sekta ya teknolojia na kuimarisha matumizi ya data na mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi na maendeleo ya uchumi wa kisasa.
“Maendeleo tunayoyaona leo katika sekta ya Tehama ni matokeo ya dhamira ya serikali ya kuhakikisha Zanzibar inakuwa sehemu muhimu ya mapinduzi ya kidijitali katika ukanda huu, tunataka kuona data na teknolojia vinatumika kama nyenzo za kuongeza tija, uwajibikaji na maendeleo endelevu,” amesema.
Kuhusu Tamasha la Data Afrika 2026, amesema litawakutanisha wataalamu wa data, wabunifu wa teknolojia, watafiti, watunga sera, wawekezaji na wadau kutoka ndani na nje ya nchi kubadilishana uzoefu, kuonesha ubunifu na kujadili namna bora ya kutumia data katika kuchochea maendeleo.
Soraga amesema tamasha hilo pia linatoa fursa kwa Zanzibar kujitangaza kimataifa kama kitovu cha ubunifu wa kidijitali na matumizi ya teknolojia za kisasa na kuchangia kuvutia uwekezaji katika sekta za Tehama, elimu, biashara na huduma za umma.
“Kuwepo kwa matukio makubwa kama hayo Zanzibar inaendelea kujiweka katika nafasi nzuri kwenye ramani ya dunia kuwa kitovu cha Tehama,” amesema akiwataka wabunifu, watafiti, wanafunzi na wadau wengine kujumuika ili kupanua uelewa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Tanzania Data Lab, Dk Mahadia Tunga amesema katika tamasha hilo washiriki watajadili matumizi ya akili mnemba (AI), usimamizi wa data, usalama wa mifumo na uchumi wa kidijitali na nafasi ya teknolojia katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.
“Ulimwengu unavyokwenda hasa katika nchi zinazoendelea kufanya uamuzi sahihi ni jambo la kimkakati kwani wana vyanzo vichache hivyo ni lazima kujua wapi vyanzo vyao wanaweza kuvitumia kupitia takwimu,” amesema.
Mkurugenzi wa Ubunifu Wizara ya Mawasiliano Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Samora Chacha amesema jukwaa hilo lina umuhimu Zanzibar kwani litaitangaza kimataifa kama kitovu cha ubunifu na teknologia na kuunga mkono ajenda ya Taifa ya kujenga uchumi wa kidijitali wenye ushindani.
Tamasha la Data Afrika 2026 linatajwa kuwa moja ya majukwaa muhimu yanayochangia kukuza matumizi ya data na teknolojia barani Afrika, linatarajiwa kufanyika Agosti 19 hadi 21 Zanzibar na kushirikisha washiriki zaidi 250 kutoka ndani na nje ya nchi.