Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shirika la Bandari latoa gawio la Sh3.6 bilioni kwa Serikali

Muktasari:

  • Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miaka mitatu tangu Seotemba 20, 2023 baada ya Serikali kupitia Shirika hilo kuingia ubia wa uendeshaji wa bandari hiyo na kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) ya nchini Ufaransa kupitia kampuni yake tanzu ya Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT).

Unguja. Ofisi ya Msajili wa Hazina imepokea gawio la Sh3.6 bilioni kutoka Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), ikiwa ni sehemu ya mchango wa shirika hilo katika kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha usimamizi wa uwekezaji wa umma.

Kiwango hicho cha fedha kimeongezeka zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na gawio lililokuwa likitolewa kwa kipindi cha nyuma cha kati ya Sh500 milioni hadi Sh850 milioni.

Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miaka mitatu tangu Seotemba 20, 2023 baada ya Serikali kupitia Shirika hilo kuingia ubia wa uendeshaji wa bandari hiyo na kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) ya nchini Ufaransa kupitia kampuni yake tanzu ya Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT).

Akizungumza baada ya kupokea gawio hilo Julai 17, 2026 Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammd Ibrahim Sanya amesema kupokea gawio hilo inaonesha matokeo ya kuendelea kuimarika kwa utendaji wa Shirika.

“Katika mashirika ambayo yanaisaidia Serikali katika ukusanyaji wa gawio na kuwasilisha serikalini ni ZPC kwani mnafanya vizuri na sivyo mlivyotoka naamini mbele tunapokwenda yatakuwa mazuri zaidi,” amesema.

Alisema kupokelewa kwa gawio hilo pia ni uthibitisho wa mchango wa mashirika ya umma katika kukuza uchumi wa nchi na kuimarisha mapato ya Serikali.

Kwa mujibu wa msajili gawio hilo linaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha mashirika ya umma yanaendeshwa kwa ufanisi, uwajibikaji na misingi ya utawala bora ili yaweze kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ameahidi wataendelea kusimamia kwa karibu uwekezaji wa Serikali katika mashirika ya umma kuongeza thamani ya mitaji ya umma, kuimarisha uwazi katika utendaji na kuhakikisha mashirika yanatoa mchango unaostahili kwa Serikali kupitia gawio na mapato mengine yanayotokana na shughuli na uwekezaji.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Ali Aboud Mzee amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za kuimarisha ufanisi wa shughuli za bandari, kuongeza mapato, kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuendeleza huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara.

“Sisi tunajisikia fahari tunapoona tumepewa majukumu ya kuendesha shughuli za huduma zenye kuleta tija na kuleta gawio serikalini, lakini kufikia kiwango kwamba tunaweza kuendesha shughuli zetu za taasisi na kurejesha faida kwa mmiliki,” amesema.

Alifahamisha kuwa Serikali inawekeza fedha nyingi na ina matarajio makubwa fedha hizo zilete tija katika mashirika hayo hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ZPC, Akif Ali Khamis amesema wanatambua kuwa shirika hilo ni moja kati ya uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar hasa ikizingatiwa ni nchi ya visiwa na moja ya kati ya shirika ambalo Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa na inatarajia kupata tija.

Amesema wanajisikia fahari kuona wameondoka katika miaka ya nyuma ambayo walikuwa wakichangia kiasi kidogo cha fedha kati ya Sh500 milioni na Sh850 milioni, lakini sasa wamefikia uwezo wa kutoa gawio la Sh3.6 bilioni.

Alisema anaamini fedha hizo zitaisaidia Serikali katika kuwekeza miundombinu mengine mbalimbali kwa ajili ya wananchi.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ZPC imeweza kufikia mapato takriban bilioni 44 na kuongeza uwezo wake kwa vianzio vyake vya kukusanya mapato na uwezo wake wa kuvutia miradi,kutoa huduma na udhibiti wa mapato yake.

Amesema wana vianzio vipya vya mapato ambavyo wanavitarajia ikiwemo vya mafuta na gesi, kuanza kurasimisha bandari za jamii bandari bubu ili kupata vianzio vipya vya fedha na mfumo ambao wanashirikiana na E- Goverment kudhibiti mapato kwa huduma wanazozitoa.

Ameahidi kwamba ZPC itaendeleza jitihada za kutoa huduma bora katika miradi mbalimbali ambayo itazalisha mapato mengi zaidi na kuendeleza mashirikiano na wawekezaji wa kimkakati 

Sambamba na hayo amesema shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano na sekta binafsi na kuvutia uwekezaji katika miradi yake ili kuongeza uwezo wake wa kukusanya mapato.