Shughuli za kushusha, kupakia meli kuhama rasmi Malindi
Mwonekano wa Bandari ya Maruhubi ambayo shughuli zote za meli zinazopakia na kushusha magari yanayotembea yenyewe (RoRo) zinahamia katika bandari hiyo kutoka bandari ya Malindi.
Muktasari:
- Shughuli hizo zinahamia katika bandari mpya ya Maruhubi ikiwa ni hatua ya kupunguza msongamano unaojitokeza katika bandari ya Malindi
Unguja. Huenda ahuweni ya msongamano katika Bandari ya Malindi ikapatikana baada ya huduma za meli zinazopakia magari yanayotembea yenyewe (RoRo) kuhamia katika Bandari ya Maruhubi.
Bandari ya Malindi ambayo hutumika kwa abiria na mizigo, inakumbwa na msongamano kutoka na ufinyu wake.
Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), kwa kushirikiana na Kampuni Zanzibar Ferry Development Ltd (ZF DevCo), zimetangaza kuhamia shughuli za kushusha na kupakia mizigo katika bandari mpya kesho Julai 18, 2026.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Julai 17, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasilaano wa ZF DevCo, Maryam Mansab, amesema imesema huduma za abiria zinatarajia kuhamia katika bandari mpya ya Maruhubi Agosti mwaka huu.
"Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi wa huduma, kuboresha usalama na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa baharini Zanzibar," amesema
Tangu kuanza kwa majaribio ya operesheni Aprili 2026 na kuhamishwa kwa shughuli za meli za Landing Craft (LCT) kwa awamu, kwa mujibu wa uongozi, kituo cha Maruhubi kimeonyesha mafanikio katika kuongeza ufanisi wa huduma.
"Muda wa kuhudumia meli umepungua kwa takribani asilimia 70 ikilinganishwa na kituo cha Kivuko cha Malindi, huku maboresho yote yaliyobainika wakati wa majaribio yakitekelezwa kwa mafanikio," imesema taarifa hiyo
Hata hivyo, licha ya meli hizo kupakia na kushusha magari katika bandari ya Maruhubi, abiria wa meli hizo za RoRo wataendelea kupanda na kushuka kupitia bandari ya Malindi wakati maandalizi ya mwisho ya miundombinu ya abiria katika Kituo cha Maruhubi yakikamilishwa.
Wadau wanashauriwa kufuatilia taarifa rasmi kuhusu ratiba za safari, njia za kuingia kituoni na taratibu mpya za matumizi ya kituo cha Maruhubi.
Hivi karibuni alipotembelea bandari hiyo ya Maruhubi, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla alipongeza hatua zilizofikiwa za ujenzi wa bandari hiyo.
Aliagiza wizara ya Maji, Nishati na Madini kumaliza changamoto iliyotajwa na kampuni hiyo kuhusu kuzuiwa kuingiza mchanga kutoka Tanzania bara hivyo kukwamisha ujenzi wa awamu ya pili ya mradi huo