Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri usafi wa mazingira Forodhani, Darajani

Unguja. Mgeni akifika Zanzibar yapo maeneo mawili ambayo anashawishika kwenda, iwapo ataondoka bila kutembelea maeneo hayo ni sawa kama hajafika Zanzibar.

Maeneo hayo ni Darajani na Forodhani ambayo ndio kitovu cha Unguja, kisiwa maarufu kwa utalii. Maeneo haya yanavutia watu wengi kutokana na shughuli nyingi zinazofanyika.

Eneo la Darajani, kunafanyika biashara ya maduka tofauti na soko. Ni katikati ya mji na Forodhani ni eneo linalovutia wengi kutokana na fukwe.

Eneo hilo hutembelewa na watu wengi wakiwamo wageni, pia linatumiwa na watu kama eneo la kustarehe, hivyo shughuli kubwa inayofanyika ni uuzwaji wa vyakula vya aina mbalimbali vitakanavyo na mazao ya bahari.

Ilikuwa ni kawaida kupita eneo la Darajani kuhisi harufu kali kutokana na uvundo wa taka zilizorundikwa bila kuzolewa hata zaidi ya wiki nzima na hakuna aliyejali hali hiyo.

Licha ya baadhi ya maeneo yalikuwapo mapipa ya kutupia taka ngumu, lakini usafi haukuzingatiwa. Hata pale ulipozingatiwa, mapipa hayo yalionekana kuelemewa kulingana na taka zinazozalishwa, hivyo kusababisha zizagae ovyo maeneo hayo.

Kama ilivyo kawaida maeneo yenye mjumuiko wa shughuli nyingi, pia hata mazingira huwa yana utata katika uzingatiaji wa usafi.

Hata hivyo, kwa mgeni aliyekwenda Zanzibar miaka mitatu iliyopita, akifika sasa katika maeneo hayo atashangaaa kuona hatua iliyopigwa katika suala la usafi.

Hali hii imefikiwa baada ya Rais Hussein Mwinyi kuingia madarakani na kuhimiza suala la usafi kila mara, hakusita kueleza hisia zake si tu anavyochukizwa na hali hiyo, bali unaifanya Zanzibar ionekane katika taswira mbaya katika uga wa kimataifa kutokana na kutembelewa na wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Kwa sababu ya uchafu huo, ilifika hatua akawataka watendaji wanaosimamia usafi ikiwa wanaona hawana uwezo wa kusimamia jambo hilo wapishe kwenye nafasi zao akieleza amezungumza kuhusu jambo hilo muda mrefu lakini haoni mabadiliko.

Kuna wakati alitengua uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri zote. Hata hivyo, hakubainisha sababu mahususi, lakini miongoni ilikuwa ni suala la usafi na mapato.


Usafi ni wa kupigiwa mfano

Katika jitihada hizo za kuleta ufanisi, Rais Mwinyi alilazimika kuziondolea manispaa baadhi ya majukumu.

Mfano, elimu na afya alizipeleka Serikali Kuu ili halmashauri zibaki na mambo mawili ya usafi na makusanyo ya ushuru kwa ajili ya kuleta ufanisi.


Siri usafi maeneo hayo

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Manispaa ya Mjini, Ali Khamis anasema siri kubwa ya kuleta mabadiliko hayo ni kujipanga, kuongeza vikundi vya usafi, ufuatiliaji na kusimamia utendaji.

"Haya ndio yamehamasisha angalau sasa kuonekana kuna mabadiliko unayoyaona," anasema.

Pia Mkurugenzi Khamis anasema elimu inayotolewa kwa wananchi licha ya kutofikia asilimia 100, nao wameanza kubadilika kuona kwamba usafi si suala la manispaa pekee.

Anasema wamejizatiti kufanya usafi katika maeneo hayo kuanzia usiku, ili kupunguza kukimbizana kunapopambazuka na hata watu wapate fursa nzuri ya kuendelea na biashara na shughuli zao.

“Hata hivyo, si tu usiku bado wengine wanafanya kazi hizo asubuhi kuhakikisha mazingira yanakuwa safi zaidi," anasema.

Pamoja na hatua hiyo, mkurugenzi huyo anakiri kuwapo uchakavu wa vifaa vya kutunzia taka katika maeneo hayo, lakini wanakusudia kutafuta vingine kukabiliana na uchafu.

Anasema wamepeleka vizolea taka zaidi ya 10 eneo la Forodhani, japo havitoshi lakini wanaendelea kuchukua hatua zaidi na kwamba wameweka kwenye mipango ya bajeti yao kuongeza vifaa hivyo.

Anasema licha ya kuwa usafi ndio kazi zao za kawaida, wamejipanga na kuongeza vikundi vya usafi kuleta tija zaidi.

Anabainisha adhabu zinazotolewa kwa watu wanaokiuka kanuni za usafi ikiwa ni pamoja na kutozwa faini, adhabu za papo kwa papo au kupelekwa Mahakama ya Mwanzo ikiwa suala itakuwa gumu.


Kauli ya wafanyabiashara

Hamdan Adam, mfanyabiashara katika eneo la Forodhani, anasema kitu cha kwanza wanachoangalia ni kufanya usafi kabla mtu hajaanza kufanya shughuli zake.

“Kama unavyoona hapa ni eneo linalokutanisha watu wengi, wageni kutoka mataifa mbalimbali wakija Zanzibar lazima wafike hapa, kwa hiyo suala la usafi lazima lizingatiwe na kila mmoja anahakikisha analizingatia kwenye eneo lake la biashara,” anasema.

Naye Husna Makame, mfanyabiashara mwingine eneo hilo anasema kila mtu akifika lazima aangalie chini ya meza yake kama kuna uchafu utolewe na kutupwa maeneo maalumu.

Katika eneo la Forodhani, shughuli za biashara zinaanza kupungua saa 5:30 usiku hapo hapo na kazi ya usafi huanza.

Katika eneo la Darajani, usafi unaanza kufanyika saa 1:00 jioni baada ya kupungua haraka za biashara, hivyo asubuhi biashara zinaendelea katika mazingira ya usafi.

“Bila usafi hata wateja huwezi kuwapata, maana kwanza kazi kubwa za hapa zinahitaji usafi hata wateja wanahamasishwa wanapomaliza kula vyakula vifaa wanavyotumia wanatakiwa kuvitupa kwenye vyombo vya taka," anasema Rashid Abdulla.


Uongozi Jiji la Zanzibar

Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Muhammed Mussa anasema kuna mabadiliko makubwa ya usafi, lakini bado hawajaridhika kwa hiyo jitihada zaidi zinafanyika ili Zanzibar iwe na ziro (sifuri) taka.

“Tumefanya, lakini hatujaridhika, usafi ndio kipaumbele chetu," anasema.

Anaeleza mikakati iliyopo ni kuwa na vifaa vya kufanyia kazi tena vya kisasa zaidi.

Ili kufanikisha hilo, anasema wameunganisha halmashauri zote chini ya mwanvuli wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Zanzibar kudhibitiana wenyewe kwa wenyewe kuhakikisha mji unakuwa safi zaidi.

Anasema tatizo kubwa bado lipo kwa wananchi ambao baadhi yao hawajataka kukubali kwamba usafi ni suala la wote wakidhani mwenye jukumu kufanya hivyo ni manispaa.

“Tunashirikiana na kampuni kubwa za kimataifa kuweka mikakati kabambe kuona Zanzibar inakuwa mji wa kupigiwa mfano," anasema.

Kampuni hizo ni kutoka Nairobi Kenya, Afrika Kusini, Uphilipino, Morocco na maeneo mengine kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha wanafanikiwa.

Pia anasema wameandaa utaratibu wa kuufanya Mji wa Zanzibar kuwa safi zaidi ikiwa pamoja na kuvisogeza karibu vikundi vya usafi ili wafanye kazi pamoja.

“Kwa speed (mwendo) tunayokwenda nayo tuna matumani ndani ya miezi sita tutakuwa tunazungumza mambo mengine, usafi Zanzibar tutakuwa mbali zaidi,” anasema

Meya Mussa anasema wanataka wafanye vizuri zaidi kuiridhisha Serikali Kuu. "Tupo tayari kupokea mawazo fikra na misaada ili kufikia huko."

Hata hivyo, Burhan Said ambaye ni mdau wa usafi anasema ipo haja nguvu hizo kuzielekeza katika maeneo mengine ya viunga vya mji huo.

Anasema ukienda maeneo ya ndani ya mji utunzaji taka hauzingatiwi, kwani watu bado wanatupa taka ovyo na wafanyabiashara wanaendesha biashara zao kwa mazoea bila kuzingatia usafi.