Soko la Sh40 bilioni laliza wafanyabiashara kukosa wateja
Mwonekano wa soko la kisasa Chuini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Wafanyabiashara wanasema mitaji yao inakufa kwa sababu ya kukosa wateja bidhaa zao kuoza kwa sababu hawana mnada Serikali yaagiza mnada wa ndizi kupelekwa pale kuokoa mitaji yao.
Unguja. Takribani mwaka mmoja tangu lifunguliwe soko la kisasa Chuini, Mkoa wa Mjini Magharibi, bado wafanyabiashara katika soko hilo wanalalama kukosa wateja wakidai mitaji yao kufa.
Soko hilo lililogharimu zaidi ya Sh40 bilioni, lilizinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi Septemba 20, 2025 lengo ni kusogeza huduma za bidhaa karibu na wananchi na kuongeza vipato vya wafanyabiashara.
Hatua ya kukosa wateja inaelezwa ni kutokana na soko hilo kukosa aina yoyote ya mnada badala yake wananchi hukimbilia katika masoko mengine.
Wakizungumza mbele ya Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla alipotembelea soko hilo leo Julai 18, 2026 wamesema bidhaa zao zinaoza kwasababu ya kutokuwa na wateja wa kutosha.
Fwarda Saidi Ali mmoja wa wajasiriamali wa viungo na bidhaa nyingine amesema licha ya kulipa Sh2,000 kwa siku ambayo ni sawa na Sh60,000kwa mwezi, lakini anadidimia katika biashara kwa kukosa wateja.
"Kuna ndizi zetu zinafika hata hatua ya kuoza nazo zinaharibika kwa sababu ya kukosa mnada tunaomba kuletewa mnada hapa ili itusaidie kuendesha biashara, amesema.
Wafanyabiashara katika soko la kisasa Chuini Mkoa wa Mjini Magharibi wakisubiri wateja sokoni hapo. Picha na Jesse Mikofu
Kauli hiyo imeungwa mkono na mfanyabiashara Said Khamis Said ambaye amesema wapo wanaochukua mikopo, lakini mitaji itakufa na kushindwa kurejesha mikopo hiyo kwa hoja hiyohiyo ya kukosa wateja.
Akitoa ufafanuzi kuhusu hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohamed Abdalla amesema tayari wameshakutana na wahusika wa masoko na kuelekeza namna ya kuendesha minada katika masoko hayo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, katika soko hilo wamepangiwa kuwa na mnada wa ndizi zote zinazozalishwa katika Kisiwa cha Unguja huku soko la Mombasa likiendesha mnada wa ndizi zote zinazotoka Kisiwa cha Pemba ili kuchagiza biashara katika masoko hayo.
Amesema katika miongozo waliyoweka, mnada huo ulitakiwa kuanza leo Julai 18, 2026, lakini inaonekana wahusika wamekaidi agizo hilo hivyo watalazimika kutumia nguvu ili mnada huo ufanyike katika soko hilo.
"Tumeshakaa na kuelekezana cha kufanya, tuliagiza mnada wa ndizi uanze leo, lakini kinachoonekana ni ukaidi kwa hiyo tutakachofanya ni kutumia nguvu na tunaagiza mnada uende na atakayekaidi tutachukua hatua za kinidhamu na kisheria," amesema Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza kuhusu hoja hizo, Hemed amesema Serikali inatumia gharama kubwa kujenga soko hilo kuwainua wananchi hivyo lazima mitaji yao ilindwe.
Amesema masoko yamejengwa na Serikali na lazima masoko yote yatafutiwe mbinu ili yainue wote badala ya kunufaisha ipande mmoja.
"Ninaagiza hapa litafutiwe mbadala, kwa jinsi mazingira yalivyo lazima kuwepo na mnada na hili halitaki mjadala," amesema.
Akiwa katika soko la Jumbi pia Hemed amepokea changamoto za gharama za kodi ambapo wamesema wanashindwa kulipa ambapo kwa mwezi wanalipa Sh40,000.
Pia, wafanyabiashara katika soko hilo wamesema iwapo mnada wa ndizi ukihamishwa na biashara zitazorota hivyo kuomba mnada uendelee.
Mkuu wa madalali, Abdalla Mwanjanga Abdalla amesema kila kiongozi anayekuja anakuwa na mipango yake hivyo kuhamisha mnada huo utazorotesha biashara hizo.
Mkuu wa Mkoa, Abdalla amesisitiza kuwa mnada wa ndizi utahama isipokuwa minada ya bidhaa zingine yakiwemo matunda itaendelea palepale.
Akizungumza kwa niaba ya mama lishe katika soko la Jumbi, Esther Chesa amesema katika mikataba yao waliambiwa kila meza ni Sh40,000 kwa mtu mmoja lakini kwa sasa wanawekewa watu wawili mpaka watatu na kuongezewa kodi tofauti na mkataba.
Akijibu hoja hiyo, Hemed amesema lazima mikataba iheshimiwe kama walielezwa walipie Sh40,000 basi iwe hivyohivyo.
"Kama mkataba unasema ukuta mmoja analipa Sh40,000 basi iwe hivyo hivyo tuheshimu mikataba inavyotaka, halafu ikaja kuleta shida,"amesema
Amesema Serikali imetenga Sh40 bilioni kwa ajili ya wajasiriamali ili wanufaike na mikopo na kuendesha biashara zao hivyo kuwataka wajasiriamali hao.