Tamasha la Kizimkazi laja kivingine, kuongeza utalii, kuvutia uwekezaji
Mwenyekiti wa Tamasha la Kizimkazi, Mahfoudh Said Omar akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tamasha la Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.
Muktasari:
- Tamasha hilo lililoanzishwa mwaka 2016 sasa limegeuka kutoka jukwaa la utamaduni na kuwa kichocheo cha maendeleo, utalii na uwekezaji Zanzibar.
Unguja. Baada ya kuahirishwa mwaka jana kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya miradi ya maendeleo, Tamasha la Kizimkazi linarejea mwaka huu likiwa na ajenda ya kuzindua miradi tisa ya maendeleo sambamba na kutangaza fursa za uwekezaji na utalii Zanzibar.
Tamasha hilo litafunguliwa Agosti 12, 2026 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, na kufungwa Agosti 14 na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa miradi itakayozinduliwa ni kituo cha amali, mradi wa maji, kiwanja cha michezo na burudani kwa watoto, nyumba za makazi, tawi la CCM pamoja na mabweni mapya ya Shule ya Asnuu Makame.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Julai 8, 2026 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Mwenyekiti wa Tamasha la Kizimkazi, Mahfoudh Said Omar, amesema kuanzia Agosti 11 hadi 14, 2026 kutakuwa na shughuli mbalimbali za maendeleo, maonesho na programu za kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Amesema tamasha hilo lilianzishwa mwaka 2016 na wazee pamoja na wananchi wa Kizimkazi kwa lengo la kuhifadhi na kuenzi utamaduni, mila na desturi za eneo hilo, lakini sasa limekua na kuwa jukwaa muhimu la maendeleo.
"Fursa zinazopatikana kupitia tamasha hili zinahusisha sekta za utalii, hoteli, uchumi wa buluu, uvuvi, biashara, huduma mbalimbali pamoja na miradi ya maendeleo," amesema Omar.
Amesema vivutio vinavyotangazwa kupitia tamasha hilo ni pamoja na fukwe za bahari, maeneo ya kihistoria, vyakula vya asili, pamoja na mila na desturi za Kizimkazi.
Kwa mujibu wa Omar, tamasha hilo linatarajiwa kuongeza idadi ya watalii, kuvutia wawekezaji, kuchochea biashara, kuongeza ajira na mapato ya wananchi pamoja na Serikali, hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
"Tunawakaribisha wawekezaji, wadau wa utalii, washirika wa maendeleo na wasanii kushiriki katika tamasha hili na kujionea fursa zilizopo Kizimkazi," amesema.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: "Kizimkazi Festival si tamasha la burudani pekee, ni jukwaa la maendeleo linalounganisha utamaduni, utalii na uwekezaji kwa manufaa ya Zanzibar na Tanzania."
Baadhi ya wananchi wamesema tamasha hilo limekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mshikamano wa jamii na kukuza uchumi wa wananchi.
Mkazi wa Kizimkazi, Salha Mussa Haji, amesema kipindi cha tamasha huwapa wajasiriamali fursa ya kuuza bidhaa na huduma zao, jambo linaloongeza kipato cha familia nyingi.
"Tunapata soko la bidhaa zetu, uchumi wa wananchi unaimarika na maendeleo yanaongezeka," amesema.
Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Paje, Mohamed Rajab Makame, amesema tamasha hilo limekuwa chachu ya umoja na ushirikiano miongoni mwa wananchi huku likiendelea kuitangaza Zanzibar kupitia utamaduni wake.
"Mbali na burudani, tamasha hili linatangaza utamaduni, mila na desturi za Kizimkazi. Tumeona mabadiliko makubwa ya maendeleo tangu lilipoanzishwa," amesema.
Tamasha la Kizimkazi lilianzishwa mwaka 2016 wakati Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Awali lilihusisha zaidi wananchi wa Kizimkazi, lakini sasa limepanua wigo na kuwa tukio linalowakutanisha washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Katika tamasha la mwaka 2024, Samia alisema Tamasha la Kizimkazi limevuka hadhi ya kuwa tamasha la kijiji na kuwa jukwaa la kitaifa linalochochea maendeleo ya wananchi.
Mwaka huu, tamasha hilo litakuwa na maonyesho, burudani, shughuli za kijamii na programu mbalimbali zinazolenga kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha utalii, uwekezaji na urithi wa utamaduni.